Familia za Kikristo na Parokia ni wadau wakuu katika azma ya Uinjilishaji Mpya katika
mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo!
Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya katika ujumbe wao kwa Watu wa
Mungu wanakazia kwa namna ya pekee, Familia kama kitovu cha mchakato wa Uinjilishaji
Mpya, jitihada ambazo zinapaswa kuungwa mkono na Mama Kanisa, Wanasiasa na Jamii katika
ujumla wake. Ndani ya Familia, Mababa wa Sinodi wanatambua na kuheshimu mchango na
dhamana ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa.
Familia ni shule ya
utakatifu, haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli. Lakini Familia katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, zinakabiliwa na vikwazo mbali
mbali vinavyolenga kufifisha juhudi za Familia katika utekelezaji wa dhamana yake
ya Uinjilishaji Mpya. Familia zikiwezeshwa kikamilifu, ziwatafute hata wale ambao
wanalega lega katika imani katika Parokia zao, kwani Familia na Parokia ni wadau wakuu
wa Uinjilishaji Mpya.
Wanasikitishwa na hali ngumu wanayokabiliana nayo wanawake
kutokana na nyanyaso za kijinsia, mfumo dume pamoja na talaka zinazowafanya kuchechemea
katika ushiriki wao wa maisha ya Kisakramenti ndani ya Kanisa. Lakini, wanawake wanapaswa
kukumbuka kwamba, licha ya matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha
na utume wao ndani ya Kanisa, kamwe Yesu Kristo, Mkombozi wa Dunia hajawasahau, changamoto
kwao kugundua njia mpya za kuweza kumkaribia Yesu katika hija ya maisha yao kama waamini.
Akihojiwa na Radio Vatican, Askofu mkuu Nikola Etrovic, Katibu mkuu wa Sinodi
ya Maaskofu anabainisha kwamba, Mababa wa Sinodi wamekazia kwa namna ya pekee, umuhimu
wa kuziwezesha Familia na Parokia kutambua, kuthamini na kutekeleza wito na dhamana
yao katika mchakato mzima wa Uinjilishaji Mpya. Mababa wengi wa Sinodi wameguswa na
ushahidi unaotolewa na Wanawake Wakatoliki sehemu mbali mbali za dunia kutokana na
nafasi na dhamana waliyo nayo katika maisha na utume wa Kanisa.
Maadhimisho
haya yamechangia kwa namna ya pekee kuamsha tena changamoto iliyotolewa na Mababa
wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unaolitaka Kanisa kujikita katika majadiliano ya
Kidini na Kiekumene. Wawakilishi kutoka Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo
yameshiriki kwa kutambua kwamba, Wakristo wote wanayo dhamana ya kutangaza Habari
Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, licha ya matatizo, changamoto na fursa zilizopo.
Askofu
mkuu Nikola Etrovic anakiri kwamba, licha ya idadi kubwa ya Mababa wa Sinodi waliokuwa
wanahudhuria kutoa tafakari, mawazo, mchango na changamoto zao, kazi kubwa imekuwa
ni kuhariri na kuratibu mawazo yote haya katika hatua mbali mbali hadi kufikia hitimisho
la Maadhimisho ya Sinodi yenyewe. Ni kazi ambayo imefanyika katika hali ya ukimya,
sala, tafakari na majitoleo ya hali ya juu kutoka katika Sekretarieti ya Sinodi ya
Maaskofu.
Hii si kazi haba, kwani jumla kulikuwa na washiriki mia nne na hamsini,
kila mtu alikuwa na nafasi na mchango wake katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu
juu ya Uinjilishaji Mpya kama mchakato unaopania kurithisha Imani ya Kikristo katika
ulimwengu mamboleo. Anawashukuru na kuwapongeza wadau mbali mbali waliojitoa bila
ya kujibakiza kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho ya Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya.
Kazi kubwa sasa ni kwa Mababa wa Sinodi, Viongozi wa Makanisa Mahalia na Taifa
la Mungu katika ujumla wake, kutekeleza kwa umakini mkubwa mawazo na changamoto zilizotolewa
na Mababa wa Sinodi, kila mtu akijitahdi kusoma alama za nyakati.