2012-10-29 08:45:44

Familia yote ya Mungu ina wajibu fungamanishi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumapili, tarehe 28 Oktoba, 2012 aliungana na Mababa wa Sinodi, Viongozi mbali mbali wa Kanisa pamoja na Waamini katika ujumla wao, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo.

Baba Mtakatifu wakati wa mahubiri yake amekumbusha kwamba, Injili ya Marko, kimsingi ni hija ya imani inayofuata nyayo za Yesu Kristo na kwamba, Mitume wa Yesu ndio wafuasi wa kwanza kugundua njia hii, lakini walikuwepo na watu kama Bartimayo Kipofu, muujiza wa mwisho uliotendwa na Yesu wakati akiwa njiani kuelekea Yesrusalem.

Kipofu huyu ni kielelezo cha mtu anayehitaji huruma na msaada wa Mungu katika maisha yake, anatambua kwamba, amepoteza uwezo wake wa kuona, lakini bado Imani yake ni hai kabisa ndiyo maana anataka kukutana na Yesu, tukio ambalo lilimkirimia tena uwezo wake wa kuona na kumrudishia utu wake uliokuwa umepotea kutokana na upofu wake, akawa tayari kumfuasa Kristo katika mwanga wa Imani.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Bartimayo ni kielelezo cha utajiri mkubwa wa imani ambayo mwamini anaweza kuupoteza katika hija ya maisha yake, hii ndiyo changamoto ya Uinjilishaji Mpya, inayopania kutoa fursa mpya kwa Waamini kuweza kukutana tena na Yesu Mwana wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Waamini wanahimizwa kumtangaza Kristo kwa ari na nguvu mpya katika maeneo ambayo Imani imefifia, moto unaoonesha uwepo wa Mungu unaanza kuzimika.

Uinjilishaji Mpya ni dhana inayogusa maisha ya Kanisa zima, lakini kwa namna ya pekee, unaigusa Mihimili ya Uinjilishaji inapotekeleza majukumu yake ya shughuli za kichungaji, inapaswa kuwasha moto wa Roho Mtakatifu kwa waamini wanaoshiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa: kwa kulishwa na Neno la Mungu pamoja na Mkate wa uzima wa milele.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Mababa wa Sinodi kwa namna ya pekee, wamekazia umuhimu wa Kanisa kuwa na maandalizi makini kwa wakristo wanaopokea Sakramenti zinazomwingiza Mwamini katika Ukristo, yaani Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu. Waamini wajichotee huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho, kwani ni Sakramenti inayomwonesha mwamini utakatifu wa maisha anaopaswa kuufuata katika hija ya maisha yake na kwamba, Wadau wakuu wa Uinjilishaji ni Watakatifu wanaoendelea kuzungumza lugha inayoeleweka na watu na kwa njia ya maisha na utume wao, wamwefanikiwa kutangaza Injili ya Upendo wa Kristo.

Uinjilishaji Mpya ni dhamana inayokwenda sanjari na Utangazaji wa Habari Njema kwa wale ambao bado hawajabahatika kumfahamu Yesu Kristo Mkombozi wa Dunia. Mababa wa Sinodi wamebainisha kwamba, bado kuna umati mkubwa wa watu wasiomfahamu bado Kristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia, changamoto ya kumwomwomba Roho Mtakatifu ili aweze kumasha ari na moyo wa Kimissionari, unaowajumuisha viongozi wa Kanisa na Waamini katika ujumla wao.

Utandawazi ni dhana ambayo imepelekea mwingiliano mkubwa wa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, changamoto kwa Mama Kanisa kuwainjilisha hata wale ambao walibahatika kusikia Injili ya Kristo lakini leo hii wamemezwa na malimwengu, kwani hawa pia wanayo haki ya kumfahamu Kristo na Kweli za Kiinjili. Familia yote ya Mungu inawajibu fungamanishi katika Uinjilishaji Mpya.

Bado kuna umati mkubwa wa watu wanaotamani kupokea Sakramenti ya Ubatizo na kwa njia hii, wanaweza kukutana na Yesu anayewasaidia kugundua ile furaha ya imani yao, kiasi hata cha kuanza kushiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa ari kubwa zaidi.

Zote hizi zinapaswa kuwa ni jitihada za Mama Kanisa zinazojionesha katika dhana nzima ya utamadunisho, ili kweli imani iweze kuota mizizi yake katika maisha na waamini, wakijenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano na Mwenyezi Mungu ili kukuza urafiki na Mungu ambaye kimsingi ni upendo. Juhudu hizi ziende sanjari na mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji kwa kukuza na kudumisha kipaji cha ugunduzi, ili kuwasaidia waamini waliokengeuka kupata tena maana ya: maisha na furaha ya kweli ambayo kimsingi ni kukutana na Mwenyezi Mungu. Hizi ndizo juhudi zinazofanywa na Kanisa kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya wale wasioamini pamoja na utume wa Mabara.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwamba, juhudi zote hizi zitazaa matunda yanayokusudiwa kwa kupata baraka na neema kutoka kwa Yesu Kristo Mchungaji Mwema. Wainjilishaji Wapya ni waamini ambao wamegundua kwamba, wameponywa na Mungu kwa njia ya Yesu, kutoka katika undani wa maisha yao.

Hata leo hii, Mama Kanisa anamgeukia Yesu Kristo: Mkombozi wa binadamu na mwanga wa mataifa kwa moyo wa furaha na shukrani. Ni mwaliko wa kujivika mwanga wa Ukweli na kuondokana na giza ili kuweza kufanya tafakari ya kina kumhusu Mungu. Ndivyo Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alivyohitimisha mahubiri yake wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya.







All the contents on this site are copyrighted ©.