Papa afanya mabadiliko makubwa: Seminari za Kanisa Katoliki kusimamiwa na Baraza la
Kipapa kwa ajili ya Makleri: Katekesi itakuwa chini ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji
Mpya!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati akishiriki katika maadhimisho ya
Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya, Jumamosi tarehe 27 Oktoba, 2012 amewashukuru
na kuwapongeza Mababa wa Sinodi kwa kazi kubwa waliyoifanya kama sehemu ya mchakato
unaopania kutangaza Imani ya Kikristo. Maadhimisho haya yamekuwa ni fursa makini kwa
Mama Kanisa kutafakari kwa kina kuhusu nafasi na dhamana ya Seminari na Vyuo vya Katekesi.
Baada ya Sala na Tafakari ya kina, Baba Mtakatifu anasema, ameamua kwamba,
dhamana ya kuangalia Seminari zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki zilizokuwa
chini ya Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kwa sasa zitasimamiwa na Baraza la Kipapa
kwa ajili ya Makleri. Idara ya Katekesi iliyokuwa chini ya Baraza la Kipapa kwa ajili
ya Makleri sasa inahamishiwa kwenye Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya.
Mabadiliko
haya yataanza kutekelezwa baada ya kuchapishwa hati maalum kutoka kwa Baba Mtakatifu
mwenyewe. Anawaalika Mababa wa Sinodi pamoja na waamini kwa ujumla, kuendelea kusali
kwa ajili ya kuombea Mabaraza haya ili yaweze kutekeleza utume huu muhimu kwa moyo
wa ushirikiano kwa ajili ya mafao ya Kanisa zima.
Baba Mtakatifu ametumia
fursa hii pia kuwatakia kheri na baraka Makardinali Wateule, kama sehemu ya mchakato
wa Uinjilishaji Mpya, unaoonesha ile sura ya Kanisa la Kiulimwengu, mahali ambapo
watu kutoka katika kila kabila, lugha na jamaa wanaozungumza lugha ya Pentekosti Mpya
ya Kanisa badala ya kujikita katika mwelekeo wa Kanisa la Kibara. Pentekoste Mpya
ni mwelekeo ambao umejionesha kwa namna ya pekee, wakati wa maadhimisho ya Sinodi
ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya.
Kanisa la Kiulimwengu linaendelea kujionesha
katika: madhulumu, hatari, furaha na matumaini yanayoonesha uwepo endelevu wa Kristo
miongoni mwa Wafuasi wake, hata katika hali ngumu zaidi. Huu ndio ushuhuda uliotolewa
na Mababa wa Sinodi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa linaendelea pia kushuhudia
uwepo wa Roho Mtakatifu anayelionesha mwanga na dira inayopaswa kufuatwa kama Kanisa
Katoliki.
Baba Mtakatifu kwa mara nyingine tena, amewapongeza Mababa wa Sinodi
na wadau mbali mbali waliohusika ili kufanikisha tukio hili muhimu katika maisha na
utume wa Kanisa, wakiwa na ari ya kutaka kutangaza Injili ya Kristo. Anasema, mapendekezo
hamsini na nane yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi ni Waraka unaobubujika kutoka katika
undani wa maisha unaopania kuzaa maisha mapya kwa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji
Mpya.