Hija za maisha ya kiroho ziendelee kuimarisha na kukuza Imani na Injili ya Upendo
na Mshikamano kati ya watu!
Hija mbali mbali zinazofanyika wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa
na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita hivi karibuni, zinapania
kwa namna ya pekee kuimarisha imani ya waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia
na kama kielelezo makini cha umoja, upendo na mshikamano wa dhati na Makanisa mahalia.
Kutokana na msukumo huu wa kiimani, Wanachama elfu tatu wa Chama cha Kitume
cha Kaburi Takatifu la Yerusalem, wanatarajiwa kutembelea maeneo ya kihistoria na
kiimani yaliyoko mjini Roma kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 15 Septemba 2013. Tukio
hili linakwenda sanjari na maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Chama hiki cha Kitume, unaotarajiwa
kuhitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita.
Hayo yamebainishwa na Kardinali Edwin Fredrick O'Brien, Rais
wa Chama hiki cha Kitume, wakati wa mkutano wao wa Mwaka uliokuwa unafanyika hapa
mjini Roma, mwishoni mwa Juma. Viongozi wa Kanisa kutoka Mashariki ya Kati wameainisha
mipango na mikakati ya shughuli za kichungaji katika sekta ya elimu inayopania kuwanufaisha
wanafunzi elfu kumi na nane kutoka: Israeli, Palestina na Yordani. Wanafunzi hao wanapata
elimu kutoka katika shule za Msingi na Sekondari arobaini na mbili zinazofadhiliwa
na Chama hiki cha Kitume.
Viongozi mbali mbali wa kidini kutoka Mashariki ya
Kati wameonesha hofu na wasi wasi wao kutokana na kuongezeka kwa vitendo vinavyoashiria
misimamo mikali ya kidini pamoja na kinzani na migogoro ya kisiasa na kijamii. Viongozi
hao wakuu wamebainisha kwamba, Nchi Takatifu bado ina utajiri mkubwa katika maisha
na utume wa Kanisa kama ilivyojionesha wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa,
iliyokazia umuhimu wa Waamini kuiga mfano kutoka katika Familia Takatifu ya Nazaeti
katika hija ya maisha yao hapa duniani.
Umoja na mshikamano uliojionesha wakati
wa Karamu ya Mwisho na wakati ule Mitume walipokuwa wanangojea zawadi ya Roho Mtakatifu
ni tema zilizopembuliwa kwa mapana wakati wa Maadhimisho ya Kongamano la Hamsini la
Ekaaristi Takatifu Kimataifa lililofanyika huko mjini Dublin, Ireland mwaka 2012.