2012-10-26 07:14:44

Yesu ni mwanga unaomwondoa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti


Ninakusalimu Mpendwa msikilizaji unayefuatilia kipindi tafakari Neno la Mungu kutoka katika Studio za Radio Vatican, nikikukaribisha katika kipindi chetu Dominika ya thelathini ya Mwaka B wa Kanisa. RealAudioMP3

Neno la Mungu latufundisha juu ya wema wa Mungu kwa wanadamu, yaani ujio wa Masiha ni heri kwa wote walio wagonjwa na wenye shida mbalimbali kama vipofu na hivi ni mwanga wa kutuondoa katika giza la utumwa wa dhambi.

Katika somo la kwanza Nabii Yeremia anatangaza upendo na uvumilivu wa Mungu anapokuja kuwaondoa wana wa Israeli katika utumwa wao. Katika utume wake huo atawavumilia wote wenye shida mbalimbali, kama vile walio vipofu, wenye mimba na wanaochechemea. Hili mara moja latufundisha kuwa Mungu anawajali wote wenye shida, yaani yeye si kwa ajili ya matajiri au wenye sauti kubwa bali watu wote ni watoto wake.

Anataka kila mmoja wetu ajisikie huru na mtoto wa nyumbani mwenye haki zote, ndiyo kusema kwa nguvu za Mungu sisi tunaweza kupiga safari toka utumwa wa dhambi zetu na kuingia katika uhuru wa wana wa Mungu. Tunaalikwa pia kuwa na moyo wa kuwajali wengine na hasa wale ambao wameachwa nyuma katika jamii kwa sababu mbalimbali, kama vile ukimbizi wa kisiasa, umasikini unaoletwa na ukosefu wa elimu, tamaduni kandamizi na mambo kama haya.

Mwandishi wa Barua kwa Waebrania anataka kuwakumbusha kuwa Yesu Kristo Masiha ndiye Kuhani Mkuu ambaye ni juu ya makuhani wote. Kumbe yale mawazo yao ya kutaka kurudia maadhimisho ya kiyahudi na fikra juu ya Hekalu la Yerusalemu anataka yawekwe pembeni na badala yake Kristo Kuhani Mkuu ndiye achukue ukanda. Jambo jingine ni lile yakwamba makuhani hutwaliwa katika jumuiya kwa ajili ya jumuiya katika mambo yamhusuyo Mungu.

Tena yafaa pia kuelewa hakuna ambaye aweza kujitwalia ukuhani bali hupewa mamlaka hayo na Mungu mwenyewe na hivi atoaye mamlaka ya kikuhani ndiye anayestahili kutumikiwa na si mwingine.

Mpendwa mwana wa Mungu, Mwinjili Marko anatupa tendo la kichungaji ambapo Masiha tuliyemsikia katika somo la kwanza toka katika kitabu cha Nabii Yeremia analitenda. Anamponya kipofu aitwaye Bartimayo. Huyu alikuwa kipofu kwa muda mrefu, akitaabika katika shida yake hiyo, na sasa Bwana anamponya. Ndugu huyu anaponywa na Bwana baada ya sala iliyojaa msisitizo ingawaje kulikuwa na vizuizi vya kutosha mbele yake. Kuwa kipofu ni alama ya kutokuwa na maisha, ni kutoona mwanga wa Kristu, twaweza kusema ni alama ya taabu, ni kukaa mbali na Mungu.

Kumbe, anapolia Mwana wa Daudi Yesu unirehemu, anataka kukaa na Mungu anataka kushiriki upendo wa Mungu. Mpendwa Bwana anapomponya ndugu huyu anatimiza lile aguo la manabii ya kwamba wote watuona wema wa Bwana. Bwana anamrudishia maisha Bartimayo na hivi anarudi katika jumuiya. Katika hali ya kawaida Wapagani ni wale ambao hawajaona mwanga wa Kristu kumbe kuponywa kwa Bartimayo ni alama na nafasi ya wapagani kupiga kelele na kukimbilia huruma na upendo wa Mungu.

Kuzuiliwa kwa ndugu huyu ni alama ya vikwazo mbalimbali katika maisha ya kikristu tunapomwelekea Mungu. Ni lazima kukabiliana na vikwazo hivi bila kukata tamaa kama alivyofanya Bartimayo katika safari yake ya kuelekea mwanga kamili. Bartimayo anaporuka na kuacha vazi lake, maanayake anaacha mambo ya zamani, mambo ya dhambi na kuanza maisha mapya katika Yesu Kristo Mkombozi wake. Mwaliko huu ni kwetu sisi, tunaalikwa kuacha ufalme wa dhambi na kujenga ufalme wa amani. Kumbuka mwaka huu ni mwaka wa Imani na hivi mwaliko nikusadiki kina Yesu Kristu kwa kuacha mambo ya zamani.

Ninakutakia heri na baraka tele za Yesu Kristu mfufuka nikikuomba tukutane tena siku na wasaa kama huu Dominika ijayo. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.









All the contents on this site are copyrighted ©.