Huduma za Upasuaji kwa Watoto wanaotibiwa Hospitali ya Mt. Gaspar Itigi kuboreshwa
zaidi baada kuweka mkataba na Hospitali ya Bambino Gesù
Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican imetiliana mkataba
wa Ushirikiano na Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Italia,
unaopania kuboresha huduma za upasuaji zinazotolewa na Hospitali ya Mtakatifu Gaspar
iliyoko Itigi, Singida, Tanzania.
Maboresho haya yanalenga zaidi kwenye Kitengo
cha Watoto wanaohudumiwa na Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, ambacho kwa miaka
mingi, kimekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuokoa maisha ya watoto wanaotoka
katika Mikoa ya Kanda ya Kati nchini Tanzania.
Mkataba huo umetiwa sahihi
na Professa Giuseppe Profiti Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù kwa niaba ya Uongozi
wa Hospitali ya Bambino Gesù pamoja na Mheshimiwa Padre Oliviero Magnone, Mkuu wa
Kanda ya Italia, Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu kwa niaba ya Shirika
na kuhudhuriwa na wafanyakazi wa Hospitali ya Bambino Gesù pamoja na baadhi ya Wamissionari
wa Damu ya Azizi ya Yesu.
Kuanzia mwaka 2013, Kitengo cha Huduma kwa Watoto
Hospitali ya Itigi kitakuwa sasa ni Kituo cha Huduma ya Upasuaji cha Hospitali ya
Bambino Gesù na kitaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Hospitali ya Bambino Gesù na
Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu.
Itakumbukwa kwamba, kwa miaka
kadhaa, kumekuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya Hospitali ya Mtakatifu Gaspar na
Bambino Gesù katika huduma kwa watoto waliokuwa na matatizo ya moyo, ambao walilazimika
kila mwaka kusafirishwa hadi Roma, Italia kwa ajili ya kupata huduma ya upasuaji wa
moyo, sasa huduma hii itaanza kutolewa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, kwa lengo
la kuokoa maisha ya watoto wengi ambao wanapoteza maisha yao kutokana na ukosefu wa
huduma makini ya afya.
Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, inayoongozwa na
kauli mbiu: tibu, fariji na elimisha ilifunguliwa rasmi kunako mwaka 1989 na Rais
Ali Hassan Mwinyi. Tangu wakati huo, Hospitali imeendelea kupanua huduma zake hadi
kufikia hatua ya kupandishwa hadhi na kuwa ni Hospitali ya Rufaa kunako mwaka 2010.
Itakumbukwa
kwamba, kutokana na ongezeko la vifo vya watoto chini ya umri wa miaka kumi kwenye
mikoa ya kanda ya Kati, Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, iliamua kupanua huduma kwa
watoto kutoka vitanda arobaini na tano hadi kufikia vitanda mia moja hamsini, tukio
lililomshangaza Rais Benjamin William Mkapa alipokuwa anafungua Wodi za Watoto hapo
tarehe 23 Novemba 2003.
Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu wanasema, zote hizi
ni juhudi za Mama Kanisa katika kumhudumia mtu: kiroho na kimwili na kwa namna ya
pekee kuendeleza ile kazi iliyoanzishwa na Yesu mwenyewe kwa kuwatibu watu magonjwa
yao kimwili na kiroho kwa kuwaondolea dhambi zao.