2012-10-24 15:36:03

Nini maana ya Imani? Na je bado inafaa kusadiki kwa Mungu? Papa ahoji katika Katekesi yake.


Baba Mtakatifu Benedikto XV1, katika mfululizo wa katekesi zake juu ya imani, Jumatano hii, ametazamisha zaidi, katika imani ya Mkristu, hasa kwa wakati huu, wa mapambazuko ya Mwaka wa Imani, ulioanza 11 Oktoba 2012 na utakamilika 24 Novemba 2013.
Papa aliifungua katekesi kwa kuhoji, nini maana ya imani na kama bado ina maana katika dunia ya leo , ambamo sayansi na teknolojia zimejipenyeza katika kila upeo wa maisha na ina maana gani kumwamini Mungu”?
Papa alitoa majibu kwa maswali hayo akisema, katika ukweli wake, nyakati hizi ambamo binadamu anataka kuufinyanga ukweli wa imani, linakuwa ni jambo la lazima, kutazama upya mafundisho ya dini na elimu yake, ili kuweza kutambua ukweli wa matukio ya wokovu , na zaidi sana , yanayojiri baada ya kukutana na Yesu Kristu , Mpendwa aminifu kutoka kwa Baba, mwenye kuwa na uzima wa milele mikono mwake.
Mafundisho ya Papa yaliendelea kusema, kwa imani sisi binadamu tunapata kujua na kumpenda Mungu, ambaye alijifunua Mwenyewe kupitia maisha, kifo na ufufuko wa Mwanae Mpendwa Yesu Kristu, Neno aliyemwilishwa, ili binadamu apate kukombolewa nae. Kwa kufanya hivyo, Mungu aliifunua maana ya kina na ukweli wa uwepo wetu binadamu.
Imani inatoa kwetu sisi binadamu tumaini na mwelekeo, wa namna za kukiishi kipindi hiki kilichojaa hali za kuchanganyikiwa kiroho na katika kupata maana halisi ya maisha katika nyakati zetu.
Papa ameainisha kwamba, zaidi ya yote, imani ni zawadi ya Mungu, inamtaka binadamu, kuufungua moyo wake na akili zake katika Neno la Mungu , na kupitia ubatizo, muumini hushirikishwa katika maisha ya Kimungu, ndani ya jamii ya Kanisa. Pia imani ni utendaji wa kina wa binadamu, kiakili na uhuru wake wa kidhamiri. Pale binadamu anapopokea mwaliko wa Mungu kama zawadi ya maisha, ulimwengu unaomzunguka, hubadilishwa kiroho na kimaisha. .
Papa alimalizia na sala ili kwamba, Mwaka wa Imani, uweze kusaidia waamini kuiishi imani yao kikamilifu, na kuwavutia wengine katika kulisikiliza na kuliishi Neno la Mungu, wakiifunua mioyo yao kwa maisha ya milele yanayoahidiwa kiimani.







All the contents on this site are copyrighted ©.