2012-10-24 08:40:21

Familia ya Mungu inawajibu wa kuwa chachu ya imani na matumaini kwa watu waliokata tamaa na kukengeuka!


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican karibu tena katika makala yetu ya Uinjilishaji wa kina. Juma lililopita tulizungumzia juu ya maeneo muhimu yanayogusa Uinjilishaji mpya kama unavyoletwa kwetu na Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika hati ya Mwongozo wa kutendea kazi juu ya Uinjilishaji mpya. RealAudioMP3

Juma hili tuendelee kutembea pamoja na Baba Mtakatifu katika kushirikishana yale yanayojadiliwa na Mababa wa Sinodi ya Uinjilishaji Mpya, kama njia ya kurithisha imani ya Kikristo.

Mpendwa msikilizaji wa radio Vatican, Baba Mtakatifu, anaendelea mbele kubainisha mazingira halisi wanayojikuta Waumini katika mazingira ya leo ambayo yanabadilika kwa kasi tena bila tahadhari. Wanafamilia ya Mungu sehemu mbali mbali duniani, wanakumbwa na uoga na kuchanganyikiwa wanapotazama ulimwengu wa leo hususan juu ya utu, maadili na maendeleo ya Binadamu kiroho na kimwili.

Katika mataifa yaliyoendelea wanafamilia ya Mungu wanakosa rejea katika kujitafuta wao wenyewe kama viumbe wa Mungu katika umilele. Hii inatokana na ukweli kwamba, ule mchafuko na mporomoko wa kifikra kumhusu Mungu unaotokana na kuibuka kwa utandawazi ambao umegusa jamii nzima hata Kanisa. Katika mazingira hayo anabainisha Baba Mtakatifu kuwa, watu wengi wamepoteza matumaini ya maisha na hivyo kukata tamaa kabisa.

Baba Mtakatifu anawaasa Maaskofu katika Sinodi hii kuona namna mbadala ya kurudisha tumaini hilo miongoni mwa Waamini na hivyo kuimarisha utume wa Kanisa lakini hasa zaidi kuonesha kupitia Uinjilishaji Mpya maana ya maisha kwa watu wa Mungu. Aidha Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, kwa namna hiyo Wanafamilia ya Mungu wataweza kuwa chachu ya matumaini kwa watu wote kupitia majadiliano na kuwashirikisha wengine tumaini lile wanaloamini na kuliishi.

Katika ulimwengu huu wenye dalili zote za kuporomoka kwa maadili na utu wema, kuna uhitaji mkubwa wa kukaa pamoja na kupeana moyo. Wakristo wanaoishi katika tumaini la Kristo: aliyeteseka, akafa na kufufuka wana wajibu wa kuwatumainisha wengine.

Njia pekee anasema Baba Mtakatifu ya kuwarudishia Taifa la Mungu matumaini ni ile ya Wakristo kukaa pamoja na kutathmini kwanza namna wanavyoishudia imani yao kwa wengine, kutathmini mazingira jinsi yalivyo na hivyo kubuni mbinu mkakati wa kupambana na mazingira hayo.

Badala ya kubaki tu kuhubiri Neno la Mungu Kanisani, katika vikundi vya sala; wakati umefika ambapo lazima Kristo ajidhihirishe sasa katika mazingira halisi ya watu wake kama Mponyaji wa wagonjwa, Anayejali walio pweke, wafungwa, wasio na sauti, wakimbizi, wasio na chakula na mazingira yanayofanana na hayo. Hii inawaalika Wakristo kumleta Kristo kwa walio wake katika matendo halisi katika mazingira halisi.

Kanisa linaalikwa kuivalia njuga dhana nzima ya Mungu katika yale maeneo ambayo tuliona hapo kwanza kuwa ni sababu ya kushuka kwa Uwepo wa Mungu katika maisha ya watu. Kanisa kupitia waamini wake lazima kumleta Mungu katika historia ya ulimwengu na vyote viijazavyo akiwapo Mwanadamu na karama zake.

Lazima watu wapambanue matendo ya Mungu yanayoendelea kutendeka kupitia Mwanadamu na sio Mwanadamu kuwa chanzo na mwisho wa mambo hayo. Wanafamilia ya Mungu kama Kanisa watafanikiwa iwapo watashiriki kikamilifu katika maeneo hayo na kutoa mwelekeo halisi na maana ya mambo hayo. Wakristo wawasaidie watu kuelewa mipaka ya tafiti za kibaolojia, madawa na lishe; wawasaidie watu kuelewa kutumia vema vyombo vya mawasiliano, wanasiasa waelimishwe nafasi yao katika kuiunganisha jamii kuishi kwa amani, haki na mapatano.

Watu waoneshwe kutumia vema rasilmali za ulimwengu huu wakiwasaidia wale wanaoshindwa kujikomboa kutokana na mazingira yao kujipatia mahitaji ya maisha kirahisi. Maana yake Wanafamilia ya Mungu wawe mashahidi kwa maisha yao kujenga amani, upatanisho, haki, uwajibikaji, upendo na mshikamano katika jamii.

Baba Mtakatifu Benedikto XVI anamalizia sehemu hii kwa kukazia umoja, mshikamano, maisha ya amani na watu wenye imani tofauti na sisi, na ushuhuda wa maisha yanayomstahili mwanadamu miongoni mwa Waumini ili kutoa mfano hai kwa mataifa. Huku ndio kuangalia na kutasiri vizuri alama za nyakati ili kuweza kuutangaza vizuri ujumbe wa Injili.

Mpendwa msikilizaji nakushukuru sana kuwa nami kwa wasaa wote. Nakutakia Baraka tele toka kwa Mwenyezi Mungu unapojiandaa kutembea pamoja na Maaskofu katika Sinodi juu ya uinjilishaji mpya. Kutoka studio za Radio Vatican ninayekakuaga ni mimi Padre George wa Bodyo mtayarishaji na msimulizi wa kipindi hiki.










All the contents on this site are copyrighted ©.