SHERIA NA KANUNI ZA NCHI LAZIMA ZIFUATWE, MIHADHARA IMESIMAMISHWA MPAKA HALI ITAKAPOKUWA
SALAMA NA JESHI LA POLISI LIMEJIPANGA VEMA KATIKA KUKABILIANA NA VURUGU ZITAKAZOJITOKEZA.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Said Meck Sadiki amekutana na waandishi wa habari tarehe
19 Oktoba 2012 katika Ofisi yake na kutoa tamko kuhusu vurugu zinazoendelea kujitokeza
katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa kumeibuka vitisho vya
hapa na pale katika Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kukamatwa kwa Sheikh Issa Ponda
ambaye anajulikana kama Katibu wa Baraza kuu na Taasisi za Jumuiya ya Kiislamu. “Mpaka
sasa wametoa taarifa kuwa kutakuwepo na maandamano ya kuelekea Ikulu ili kushinikiza
kuachiwa huru kwa Sheikh Issa Ponda na wafuasi wake”.Alisema Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam.
Maandamano hayo hayana kibali chochote kile ni kutaka kuibua vurugu
na uvunjifu wa amani kwa wana Dar es Salaam,hivyo basi nawaomba wananchi wa Dar es
Salaam kutokushiriki katika maandamano hayo kwani kwa kufanya hivyo sheria kali zitachukuliwa
dhidi ya waandamanaji kwani maandamano hayo ni Haramu na hayana kibali wala tija kwa
Taifa letu.Alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Aidha,Mkuu wa Mkoa alisema kuwa lazima
tufike mahali tuishi kwa kufuata misingi ya taratibu na sheria za taifa letu kwani
Sheikh Ponda hakukamatwa kama Sheikh bali kama mchochezi wa vurugu na kuwashawishi
wafuasi wake kuidharau Serikali na vyombo vya usalama.Hivyo amekamatwa kama mtuhumiwa
mwingine yoyote anayeweza kukamatwa.
Hivyo basi yatupasa tuwe na subira na
kufuata taratibu husika kwani kama Sheikh Issa Ponda hana hatia basi ataachiwa na
kama ana hatia basi atahukumiwa kama ilivyo kawaida kwa mtuhumiwa yoyote yule akipatikana
na hatia.Hivyo basi lazima tujue kuwa nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya taratibu
na sheria na hakua aliye juu ya sheria.Sheria ipo na lazima ifuatwe.
Wakati
huo huo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema Mihadhara yote ya kidini kwa sasa imesimamishwa
kwa kipindi hiki kigumu mpaka hapo hali itakapokuwa shwari.
NAYE SHEIKH WA
MKOA WA DAR ES SALAAM- Sheikh Alhadi Mussa amewataka waumini wa dini ya kiislamu kuwa
na subira katika kulitatua suala hili na wasijipange kufanya vurugu ya aina yoyote
kwani suala hilo limeshafika katika vyombo vya sheria hivyo tuviachie vyombo hivyo
vifanye kazi yake na haki itakuja kujulikana.
Aidha Sheikh huyo amesema kuwa
ameridhishwa na maneno ya maaskofu katika kuwataka waumini wao kuwa na utulivu na
si kulipiza kisasi kwani.Lakini pia amewataka waislamu nao watulie katika hilo.
NAYE
PADRI ANTHONY MAKUNDE –Katibu Mkuu wa Balaza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, amesema
kuwa anaungana na viongozi wengine wa Makanisa katika kuwasisitiza viongozi wa Dini
ya Kikristo kuendelea kuwa na subira katika kipindi hiki kwani njia pekee na sahihi
ya kutafuta suluhu na amani ni njia ya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi.
KWA
UPANDE WA KAMANDA WA POLISI WA MKOA WA DAR ES SALAAM- Suleimani Kova amesema kuwa
Jeshi la Polisi limeungana na Mhe.Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika kukabiliana
na vurugu zitakazojitokeza katika Mkoa wa Dar es Salaam.Aidha mtu yeyote akifanya
kosa anachukuliwa kama mharifu kwa sababu sheria haibagui wala kuchagua yenyewe inakata
kotekote haiangalii kama ni Padri au Sheikh.
Kuhusu maandamano hayo yaliyopangwa
Kamanda kova amesema kuwa Jeshi la Polisi limejipanga vema katika kukabiliana na hilo
hivyo mtu yeyote akitaka kuandamana ajitahidi kutafakari mara mbili mbili itakuwaje
baada ya hapo kwa yeye na familia yake.
Mwisho kabisa kamanda Kova amewataka
watu hawa wajisalimishe wenyewe kwa jeshi la polisi ama sivyo sheria itachukua mkondo
wake. -Mukadam Salehe -Kondo Juma -Saaban Mapeo -Jaffary Mneke -Rajabu
Katimba -Amani Moshi.