2012-10-23 10:16:06

Jimbo Katoliki Kondoa laadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Msimamizi wa Jimbo!


Waamini wa Jimbo Katoliki la Kondoa, Tanzania, wametakiwa kuwaombea sana Mapadre wa Shirika la Mateso, “Passionist Fathers” walioanzisha kazi kubwa ya Uinjilishaji wa Imani ya Kikristo katika Jimbo la Kondoa wakati huo likiwa ni Jimbo Katoliki la Dodoma ambapo walijitosa kimaso maso kumtangaza Kristo kwa njia ya Injili ya Upendo.

Wito huo umetolewa na Askofu mstaafu Mathias Isuja Joseph wa Jimbo Katoliki Dodoma, wakati wa ibada maalum ya kumsimika Mtakatifu Paulo wa Msalaba kuwa Somo wa Jimbo hilo na kuongeza kuwa bila kuwaombea mapadre hao waamini watakuwa hawatendi haki kwa waanzilishi hao walioleta mwanga wa Neno la Mungu katika eneo lote la Kondoa na Dodoma.

Askofu Mathias Isuja aliyasema hayo alipokuwa akitoa mahubiri yake kwa maelfu ya waamini waliokusanyika nje ya Makanisa mawili ya Jimbo hilo jipya linalojengwa sasa na la zamani la Roho Mtakatifu ambalo lilijengwa na Wamissionari wa Shirika la Mateso.

Alisema kuwa katika Shamba la Bwana mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache hivyo ni vyema waamini wakaelekeza nguvu zao katika kuiombea miito ili wapatikane watenda kazi wengi, watakatifu na wachamungu katika Jimbo hilo linalokuwa kwa kasi na kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Askofu Bernadine Mfumbusa inayosema “Kondoa Tunaweza”.


Ibada hiyo maalum ilihusisha pia utoaji wa Sakramenti ya kipaimara kwa watoto wapatao 160, taarifa za matoleo ya shukrani kutoka kila Parokia, kumpongeza na kumwombea Askofu Mathias Isuja Joseph kwa kutimiza miaka 40 ya uaskofu sanjari na kumsimika Paulo wa msalaba kuwa msimamizi wa Jimbo Katoliki Kondoa.








All the contents on this site are copyrighted ©.