2012-10-22 09:02:31

Kardinali Pengo asema "Kamwe msitumie kinzani, vurugu na misigano ya kidini kujinufaisha kiuchumi, kisiasa, kijamii na kidini"


Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya inayoendelea hapa mjini Vatican wanasema, kati ya mambo yanayoendelea kukwamisha mchakato wa majadiliano ya kidini ni pamoja na misimamo mikali ya kiimani, watu kutoheshimu sheria za nchi kwa kutaka kujichukulia sheria mikononi mwao pamoja na malumbano ya kidini yanayolenga kuvunja misingi ya amani na mshikamano kati ya watu wa mataifa kwa malengo binafsi: kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidini. RealAudioMP3

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar anabainisha kwamba, choko choko, machafuko na uharibifu wa mali kwa misingi ya kidini, zimeendelea kujionesha kwa namnaya pekee nchini Nigeria na Tanzania. Hii ni kutokana na sababu kwamba, watu wanashindwa kuelewa kwamba, kimsingi hakuna dini inayoshabikia mapigano wala machafuko ndani ya Jamii.

Kardinali Pengo anasema kwamba, kuna watu ambao wanapenda kutumia tofauti za kidini kama njia ya kujijenga: kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidini, kiasi hata cha kuhatarisha amani, usalama, utulivu na mshikamano wa kitaifa. Ni watu wanaogubikwa na ubinafsi, uchu wa mali na kupenda mno madaraka. Watu wa namna hiyo hawataki kusikia ukweli mkamilifu kuhusu masuala ya kidini, kwao jambo la msingi ni kufaidika na migogoro na kinzani za kidini.

Kardinali Pengo anawaalika Waamini wa Dini ya Kiislam na Kikristo kuendeleza moyo wa majadiliano ya kidini, kwa kuheshimiana, kuthaminiana na kujadiliana masuala muhimu ya kidini kwa ajili ya mafao ya wengi na kamwe tofauti zao za kidini zisiwe ni chanzo cha kinzani, vurugu, umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia na uharibifu wa mali ya watu.

Serikali na vyombo vya dola vitekeleze wajibu wake kikamilifu kwa kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria unashika mkondo wake. Anatoa onyo kwa wanasiasa wanaotumia tofauti za kidini kama njia ya kujitafutia umaarufu, ili hatimaye, kujijenga kiuchumi, kisiasa na kijamii, kuacha mara moja kwani wanaweza kusababisha maafa makubwa kwa Jamii. "Kamwe hasiwepo mtu anayetumia dini kama ngao yao katika medani mbali mbali za maisha".

Kardinali Pengo anawaomba watanzania na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba, tofauti za kidini na kiimani zimekuwepo nchini humo miaka nenda miaka rudi, lakini watu wakaheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana. Anajiuliza, kumetokea nini hata leo hii dini iwe ni chanzo cha kinzani, vurugu na machafuko nchini Tanzania?

Anawakumbusha wote wanaotaka kuchochea vurugu, vita na kinzani kwamba, amani ikitoweka, hakuna mtu atakayesamilika kwani matunda ya kuvunjika kwa misingi ya haki kamwe hayawezi kudumu. Ni jukumu la kila mtu kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani na kamwe tofauti za kidini zisiwe ni chanzo cha kinzani, vurugu na umwagaji damu.







All the contents on this site are copyrighted ©.