2012-10-22 09:52:50

"Iweni mashahidi wa Injili ya Upendo, Haki na Amani Duniani"


Askofu mkuu Francisco M. Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Jumamosi tarehe 20 Oktoba, 2012 aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya shamra shamra za Mahafali ya arobaini na tatu ya Kidato cha Nne kwa Seminari ndogo ya Mtakatifu Petro, iliyoko Jimbo Katoliki Morogoro.

Ibada ya Misa Takatifu ilihudhuriwa na Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro, Mapadre, Watawa na baadhi ya wanafunzi waliowahi kusoma Seminarini hapo ambao wameendelea kuchangia kwa hali na mali katika maisha na ustawi wa Seminari hii kwa ajili ya mafao ya Kanisa na Jamii kwa ujumla wake. Yafuatayo ni mahubiri ya Askofu mkuu Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania.

Wapendwa waseminari na wahitimu wa kidato cha nne,

Tunaadhimisha ibada ya Ekaristi Takatifu leo hii kama ishara ya kumshukuru Bwana Mungu, kwa kuwepo kwa Seminari ndogo ya Mt. Petro, Jimbo Katoliki la Morogoro na hasa kwa wahitimu wa kidato cha nne wa mwaka 2012, ambao wamekuwa hapa kwa muda wa miaka minne wakijiandaa kuungana na kidato cha tano katika michepuo ya taalulma mbalimbali ifikapo mwaka 2013. Napenda niwape moyo wa kuendelea na malezi ya Seminari na mwendelee kutambua wito wa Bwana wetu Yesu Kristu anayewaita “Njooni Mnifuate”

Waseminari wapendwa, kila mnapojitahidi kuitikia wito huo kumbukeni maneno yake: Mimi ni Njia, Ukweli na Uzima” Yoh 14:16 maneno haya ya hekima yana maana thabiti katika hisis za kijamii ya leo. Bwana Yesu Kristu hasemi kuwa yeye ni mmoja miongoni mwa viongozi wengi waliohalalishwa kisheria, la hasha! Yeye ni njia wala hasemi kwa kujithibitisha kwamba analeta moja ya ukweli miongoni mwa kweli nyingine zinazothibitika. Yeye ni Ukweli. Anajitoa siyo kama mmoja kati ya wengi ili achaguliwe afe, kama yalivyo masharti mengi ambao mteja anayanunua dukani kadri ya mapenzi yake. Yesu ni Uzima.

Mt. Thomas ana haya yafuatayo kuhusu maneno hayo yenye uhai ya Yesu; bila njia , hakuna pa kwenda. Bila ukweli hakuna utambuzi na ufahamu, bila uhai hakuna kuishi. Bwana wetu Yesu Kristu aliyasema maneno haya kwa wafuasi wake mwishoni mwa maisha yake. Ni kama vile wafuasi wake wamefikia siku yao ya mahafali waliogopa kwamba Yesu atachukuliwa kutoka kwao mioyo yao ilifadhaika sana.

Wapendwa wahitimu, mnavyomaliza masomo yenu, mtakuwa kama mitume ambao baada ya kufunzwa na kuapata malezi na kuhitimu wakiwa pamoja na Yesu, wakatoka kwenda kuhubiri Neno la Mungu duniani ambako kumejaa matatizo. Mtakuwa mashahidi kwa Neno lake katika matendo yenu na mienendo yenu. Kama washahidi mtajikuta katika upeo mpya ambao utawaogofya na kuwatisha na kuwasumbua. Kwa mfano, wale wanaokwenda Jangwani wanajua kwamba hawawezi kwenda bila kiongozi. Hakuna alama. Kila mahala ni sawa na pengine. Pande hazionekani, kiongozi peke yake anaweza kumwonyesha msafiri katika eneo hilo lisilo na alama.

Kiongozi ni njia kwa sababu huyo msafiri au mtalii hajapita njia ile. Lakini aliyekuwa pale muda mrefu anaijua njia. Kwa hiyo unaposafiri duniani katika safari ambayo njia zake hazijulikani kiongozi wake pekee ni Yesu Kristo, unapo pita katika njia zisizo na uhakika, njia za wasiwasi na mashaka mashaka.

Papa Benedikto wa XVI, katika mahubiri yake wakati wa misa yake ya kwanza ya kipapa alimnukuu Papa Yohane Paulo wa Pili, ambaye naye alihubiri katika misa yake ya ufunguzi ya kipapa akisema “Usiogope! Fungua milango wazi kwa Yesu Kristu” ukimruhusu Yesu aingie katika maisha yako, hupotezi chochote. Hakuna unachokipoteza ambacho kinayafanya maisha yako yawe huru, mazuri ya kupendeza na yenye umaarufu.

Katika urafiki huo tu na Yesu, milango ya maisha inafunguka na kuwa wazi kabisa. Ndipo katika urafiki huo tu uwezekano wa uwepo wa uhai wako unajidhihirisha kujifunua na kujionyesha. Ndipo katika urafiki huo tu unaonana na kuuzoea uzuri na uhuru wa maisha. Kwa hiyo, katika ibada hii ya Misa Takatifu ya shukrani, ninakuambia: usimwogope Yesu, hachukui chochote kutoka kwako na anakupa kila kitu. Malezi uliyoyapata hapa katika Seminari hii ya Mt. Petro yatakuwa na maana tu kama yatakuongoza kumjua, kumpenda, kumfuata na kumshuhudia Kristu kama Neno na Njia inayotuongoza kwa Baba na kwa maisha ya kweli.

Wakati huu tunaishi katika maisha ambayo kua kijana na kuwa tofauti na wenzako havichangamani. Ni sharti ujiandae kwa yanayojitokea kila saa. Yatakayojitokeza hapo baadae yanawakilishwa na mateso ya mamilioni ya watu, wewe ukiwa mdhamini watoto. Yesu ambaye ni uzima, analeta ukamilisho katika uzima wako katika jamii iliyovunjika na kusambaratika. Binadamu anaweza kuishi kikamilifu tu, iwapo kila sehemu ya maisha yake ya kiroho, ya akili, ya kisaikolojia nay a kifisiolojia au kimwili – yanafanya kazi ipasavyo na kwa mwafaka kamilifu baina ya nyanja hizo na watu wanaomzunguka na mazingira. Hakuna binadamu mwanasaikolojia au daktari anayeweza kuyafikia haya katika ukamilifu wake. Inawezekana tu kama rehema na neema za Yesu Kristu zinafanya kazi ndani yako. Kama haya yatatokea, basi mtaigeuza na kuibadili jamii na tamaduni na kijamii kwa shuhuda za maisha yenu, ambao ni Neno la Mungu lililomsilishwa katika maisha yenu.

Kwa wale ambao wataendelea na malezi ya Seminari, ninataka niwaambie jambo muhimu ambalo Papa Benedikto wa XVI alikazia wakati alipowapa sakramenti ya upadre Mashemasi 14 kwa Jimbo la Roma tarehe 23 Juni 2010: Upadre ni sala na utumishi na wala si heshima na uwezo, kazi na ujumbe wa Padre ni kugundua katika sala uso mpya wa Mwana Mungu, wale tu wenye mahusiano ya kimsingi na Bwana Yesu anawashika na kuwakumbatia, anawasindikiza kwa wengine, anawatoa kwa watu na wanakuwa mashahidi wake.

Kumtii Mungu na kuwa karibu naye lazima kuambatane na uchungaji wa kipadre. Ni lazima iwe sehemu muhimu, hata inapofikia waka mgumu inapodhihirika kwamba vitu vinavyopaswa kufanyika lazima vipewe kipaumbele. Papa aliendelea kusema kuwa Upadre siyo njia ya maisha salama au ya hakika, na ya kupata jina katika jamii. Naomba nisisitize kwamba, ninyi ambao mnajiandaa kuwa mapadre na kwa yeyote anayetaka kuwa Padre ili ajiongezee hadhi yake au awe na cheo katika jamii ameelewa vibaya maana ya kazi za kichungaji na misingi yake.

Yeyote anayetaka kuweka kipaumbele katika kujipatia hadhi na cheo zaidi katika maisha yake, atakuwa mtumwa wa maisha yake na mtumwa kwa maoni ya jamii. Anataka asifiwe, kwa hiyo atalazimiza kujipendekeza, kusema tu mambo ambayo watu wanapenda kuyasikia na kuyafuata katika mitindo ya mabadiliko badiliko, na mawazo yake ili kuweza kufanikisha matakwa yake. Haya siyo maisha ya shuhuda. Mtu ambaye anapanga maisha yake hivyo, na Padre anayoona uchungaji wake kwa njia hii hampendezi Mungu kwa dhati, wala hawapendezi wengine ila anajipendeza mwenyewe, na kwa kweli mwishoni anajipenda mwenyewe.

Hapa seminarini, unaelekezwa na kulelewa kusema ndiyo kwa Mungu na siyo kwako mwenyewe; ndiyo kwa mwengine katika kujitambua kuwa wewe unakua na kukomaa kila siku kwa kufuata na kujitumbukiza katika matakwa ya Mungu. Kwa njia hii, utu wako hautafutika kabisa, ila kinyume chake utaujua kwa undani zaidi ukweli wa maisha yako na uchungaji wako.

Kanisa la Kristu lina lipania kujenga Jumuia za upendo, haki, amani, kusameheana, huruma, kuwavika walio uchi, kuwalisha walio na njaa, kufungua macho ya wasioona, kuwatembelea wafungwa, kuwatendea wema wale ambao ni tofauti na sisi wenyewe, kuwakumbatia maadui, na kuvumilia bila manungu’niko gharama kubwa zinazoenda na kuwapenda jirani. Vitu vingi sana katika jamii vinataka vibadilishwe kama tunataka tuendeleze fadhila hizo. Ndivyo tunavyovitegemea kutoka kwenu wahitimu wetu wapenzi.
Siku yenu ya mahafali ni siku ya kujifunua kwenu kwa jamii ulimwenguni, mkiwa na furaha tele. Kwa malezi mliyopata, mtakuwa tayari kutoa ushuhuda wa Neno lake, kuonesha uso, siyo uso wetu bali wa Yesu Kristu ambao utatafsiriwa katika utayari wenu katika kuwahudumia maskini, kufanya kazi ili kuweka misingi imara ya elimu kwa wale ambao hawana, kuzungumza na wale ambao tunahitilafiana nao na kujadiliana juu ya amani.

Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI akizungumza Siku ya Vijana Duniani, katika mji wa Cologn, Ujerumani kunako mwaka 2006, alisema, “tukitumia mifano tunayoijua siku hizi ni kama kuwashawishi watu wakubali matumizi ya nguvu ya nuklia – yaani ushindi wa upendo kwa chuki, ushindi wa upendo dhidi ya kifo. Ni huo mpasuko wa mazuri kushinda mabaya unaweza kuwasha moto wa mabadiliko ambayo kidogo kidogo yatabadili dunia. Kazi yenu haitakuwa ya kikristu kama haitaweza kuwajenga watu ili waishi wakipenda jamii zinazopendana katika familia zao, kwa urafiki, udugu, utaifa na kama dunia moja.

Wapendwa wahitimu wangu, ninyi mna uwezo mkubwa na nguvu nyingi zinazoweza kutumika kujenga na kuibadilisha dunia kuwa mahali pazuri zaidi pa kuishi. Majukumu ya Seminari ni kuwasaidia ninyi baada ya kumaliza, kujenga tamaduni zinazomuakisi Yesu Kristu, Njia, Ukweli na Uzima. Natumaini mtamleta Yesu nyumbani kwenu na kazini kwenu. Natumaini ninyi pia mtakuwa njia, ukweli na uzima kwa wale ambao wanamtafuta. Natumaini pia mtaendelea na malezi ya Seminari na kuwania kwa dhati kabisa kuwa Mapadri wazuri na mashuhuda wazuri wa Injili ya upendo na amani.

Mwenyezi Mungu awaimarishe katika safari yenu ya masha na awaongoze katika njia ya kiroho na ushuhuda madhubuti na wa matokea mazuri kwa ajili ya utumishi wa Mungu na wa kanisa Katoliki la Tanzania na kwingine kote, Amen.










All the contents on this site are copyrighted ©.