2012-10-22 11:22:44

Askofu Beatus Kinyaiya anabainisha baadhi ya mambo yanayotiliwa mkazo na Mababa wa Sinodi ya Uinjilishaji Mpya hapa Vatican


Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican ilibahatika kukutana na Askofu Beatus Kinyaiya, Mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika maadhimisho ya Sinodi ya Uinjilishaji Mpya inayoendelea hapa mjini Vatican. RealAudioMP3

Pamoja na mambo mengine anabainisha: Mababa wanaohudhuria, lengo, changamoto kutoka Barani Afrika kuhusiana na dhana ya Uinjilishaji Mpya; mbinu zinazotarajiwa na Mama Kanisa katika azma ya Uinjilishaji Mpya; umuhimu wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo pamoja na wito wake kwa Familia ya Mungu Barani Afrika.

Sinodi hii ambayo Baba Mt. Benedikto XVI amependa ifanyike wakati huu inahudhuriwa na maaskofu 263 kutoa nchi mbali mbali duniani. Pia inahudhuriwa na wawakilishi wa wakuu wa mashirika mbali mbali na baadhi ya wakuu wa vyuo vikuu vya kitaalimungu hapa italia. Vile vile inahudhuriwa na wawakilisha wa makundi mbali mali kama vile waanzilishi wa vyama vya kitume kama Neo katekumenato na wawakilisha wa wa na familia na vijana.

Q 2. Lengo la Sinodi hii ni nini?

Jina la sinodi hii ni Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo
Lengo ni kutafuta mbinu mpya ya kufundisha imani ile le aliyotufundisha Bwana wetu Yesu Krsitu, kwa namna ambayo itakubalika na watu wa kizazi hiki.
Pia Sinodi inalenga kuasha upya na kukazia zaidi umuhimu wa kuishi imani.

Ukitazama historia ya Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican kwa mfano, ambao tumeadhimisha Jubilee yake ya miaka 50 hivi majuzi, utaona kuwa nayo ililenga kuwasaidia watu kiroho ili wamrudie tena Mwenyezi Mungu hasa baada ya kuporomoka kwa maadili na utu wema, kufuatia Vita kuu ya pili ya dunia pamoja na kuenea kwa ukomunisti n.k

Kanisa la sasa limejikuta katika hali kama hiyo;
Kanisa la Ulaya na Marekani kwa mfano Imani imefifia sana. Nyuma ya yote hayo ni watu kupenda mno malimwengu. Na hali hii imechochewa sana na vyombo vya labari – TV, Internet, Radio, nk. Vyombo hivi vinafundisha kuwa kila kitu ni ruksa.

Matokeo yake ni kwamba watu wanaishi na falsafa ya kusema “ upe mwili kitu unapenda” Matokeo yake ni watu kujiingiza katika ulevi, kutumia madama ya kulevya, kujamiiana bila kuishi katika misingi ya maisha ya ndoa na familia. Na yote haya yanakubalika na kuonekana ni sawa. Na asiyefanya hivyo anaonekana mshamba. Huu ni uhuru usiokuwa na mipaka wala nidhamu na utu wema.

Kwa kuwa Kanisa linapinga mambo hayo, hawa watu ambao baadhi yao walikuwa wakristu, wanalikwepa kanisa, hawasali tena, hawapokei tena Sakramenti, na wengine wanafikia hatua ya kukana dini yao.






Q 3. Kwa upande wa Afrika hali ikoje?

Kwa upande wa Afrika hali sio mbaya kama kwa wenzetu. Kanisa barani Afrika linakuwa vizuri na lina nguvu. Watu wanahudhuria ibada na wanashiriki kwa furaha. Lakini yale yaliyopo ulaya nayo pole pole yanakuja Afrika kwa njia ya mtandao pamoja na matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii. Vijana wetu wanaona na wanaiga haraka sana kwani wanaamini kuwa kila kinachofanyika Ulaya na Marekani ndio maendeleo. Kwa hii falsafa ya kusema “ upe mwili kitu unapenda” inaonekana pia kwa baadhi ya viaja wetu, hasa wanaoishi mijini.

Siku hizi tunaona jinsi tatizo la ulevi wa kupindukia likiharibu familia nyingi. Pia madawa ya kulevya yanatumiwa na baadhi ya vijana wetu. Na kuna watu wamejiingiza kabisa kwenye hiyo biashara kwa sababu soko lipo. Swala ya kujamiiana nje ya ndoa nalo ni tatizo. Ndiyo maana janga la Ukimwi linazidi siku hadi siku.

Zaidi ya hayo, tuna tatizo la kuchanganya Ukristu na Upagani: dhana ya uwili katika maisha. Kwa mfano, kama kuna tatizo la ugonjwa au kifo, baadhi ya wakristu wanakimbilia wa waganga wa kienyeji kupiga bao ili wajue ni nani amesababisha hilo tatizo. Au wakati wa uchaguzi baadhi ya watu wakiwemo wakrsitu huenda kwa waganga wa kienyeji ili wasaidie kushinda. Ni mambo ya kipuuzi lakini watu, tena wasomi wanafanya.

Halafu kuna woga wa uchawi. Pia woga wa mizimu kwamba wanaweza kuwadhuru, n.k. Kwa hiyo, kuna wakristu ambao wanaamini katika dunia mbili- dunia ya Ukristu na dunia ya upagani. Vile vile kuna uonevu mwingi katika jamii zetu. Tunaona jinsi akina mama, vikongwe, watoto, na walemavu wanavyonyimwa haki zao za mingi. Hamu ya Sinodi hii ni kuona haya matatizo yanapungua na hata kuisha kabisa ili watu wote waonje uhuru wa kuwa Waana wa Mungu na njia pekee ya kupambana nayo ni kumleta Mungu kati yao.

Q 4. Mbinu gani mnategema kutumia katika Uinjilish Mpya ?

Mbinu ya kwanza ni kumtegemea zaidi Roho Mtakatifu. Yeye amelitunza kanisa karne zote, na tunaamini ataendelea kufanya hivyo. Viongozi kujitazama kwa upya.
Sinodi inatuasa sisi viongozi (Maaskofu na Mapadre) kujitahidi kuishi kile tunachowafundisha watu ili kwa maisha yetu ya utakatifu tuwavute wengi kwa Kristu. Maisha huongea zaidi kuliko maneno matupu

Pia lazima tujitahidi kuwa karibu zaidi na watu. Wale mapadre ambao wanawatembelea Wakristu wao nyumba kwa nyumba wanafanikiwa zaidi katika kueneza Neno la Mungu. Sinodi pia inawakumbusha wahubiri wote kuandaa vizuri mahubiri yao. Wako Wakristu wanaoacha kufika Kanisani kusali kwa sababu ya baadhi ya mahubiri yetu kutokuwa na ujumbe wa kuwafaa. Ili tuweze kuhubiri vizuri tunahitaji kusoma na kujiandaa vya kutosha.

Sinodi pia inawakumbusha Walezi wa Seminari umuhimu wa kuwaandaa vizuri Waseminaristi wakubwa na wadogo. Sio tu kuwajaza elimu kuhusu taalimungu, bali wawasaidie pia kukutana na Yesu ( personal encounter) katika maisha yao.

Kwa upande wa watawa, Sinodi hii inawakumbusha watawa kuishi wito kwa uaminifu mkubwa kwani utakatifu wa maisha yao ndio utakaowavuta wengi kutaka kumjua Mungu.

Kwa upande wa Waamini Walei, Sinodi inawaambia walei kuwa kwa njia ya Ubatizo sisi sote tumeitwa kumtangaza Kristo. Kwa hiyo, wawe tayari kumtangaza Kristo po pote wanapokuwa bila aibu. Wazazi nao wajue wana wajibu wa kuwarithisha watoto wao imani. Wasiache kuwabatiza watoto kwa kisingizio kuwa wataamua wenyewe mbele ya safari. Hii si sawa. Wawe tayari hata kufa mashahidi kwa ajili ya imani yao kwa Kristo. Tangu sasa walei wajue kuwa ile namna yao ya kufikiri kuwa kazi ya kuhubiri ni ya ma padre na makatekista kuwa si sawa.

Kwa vijana, Sinodi inawashauri viongozi wote kuwa na utaratibu mathubuti wa kuwalea vizuri vijana katika maswala ya imani. Vijana wote po pote pale walipo wapewe malezi ya Kikristo, iwe shuleni vyuoni n.k. Na wale wanaoishi katika mazingira magumu, Mapadre waanzishe clubs – vikundi- vya kuwakusanya siku za Jumapili na kuwafundisha imani, kujibu maswali yao kuhusu maishana matarajio yao kwa siku za usoni.

Kwetu sisi sote, tunakumbushwa tena na Sinodi ya Uinjilishaji Mpya kuwa Sala na Sakramenti na hasa Sakramenti ya Ekaristi na Upatanisho ni muhimu sana kwa maisha yetu ya kiroho. Tupende kuzipata mara kwa mara na kwa njia ya uchaji.

Q. 5. Sinodi imezungumza lo lote kuhusu Jumuiya ndogo ndogo?

Sinodi ya Uinjilishaji Mpya pia imezungumzia juu ya Jumuiya Ndogo nndogo za Kikristo. Kwa kuwa Jumuiya ndogo ndogo zimefakiwa sana Barani Afrika katika kuwaleta watu wachache na kusali pamoja na kutafakazi Neno la Mungu kama Familia ya Mungu inayowajibika tumesifiwa sana kwa hilo na wenzetu kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Nasi tumewashauri waanze jumuiya ndogo ndogo ulaya na marekani. Baaadhi ya sehemu wameshaanza kuiga na wanaonja sasa faida yake kama chombo muhimu cha Uinjilishaji mpya unaopania kufufua imani.

Q 6. Mwisho, una wito gani kwa watu wote ?

Napenda kuwakumbusha watu wote kuwa ikiwa sisi sote tutaishi maisha ya kimungu, maisha ya uadilifu, maisha yenye kuongozwa na tunu za kikristu, maisha ya hapa duniani yatakuwa ya haki, ya amani, utulivu na furaha kubwa.

Pili siku tutakapoondoka katika dunia hii, kama tutakuwa tumishi kama tunavyoaswa na viongozi wetu wa dini, na kama Sinodi hii inavyotuasa, hakika tutapata maisha ya furaha kuu yasiyo na mwisho mbinguni kwa Baba.

Lakini kama tutaendelea na ukaidi wetu na kukumbatia yale ya kidunia ambayo hayampi Mungu nafasi, basi siku ya mwisho tutatupwa kwenye mahangaiko makuu yasiyo na mwisho pamoja na yule mwovu shetani.

Kwa kuishi maisha yanayotawaliwa na Imani ya Yesu Kristu, hatupungukiwi na chochote na badala yake, tunafanya dunia yetu iwe mahali pazuri zaidi pa kuishi na wakati huo huo, tunajiandalia mema mengi ya kiroho mbinguni.








All the contents on this site are copyrighted ©.