2012-10-20 10:04:03

Uinjilishaji Mpya unakwenda sanjari na Utakatifu wa Maisha!


Uinjilishaji Mpya na Utakatifu ndiyo tema iliyochaguliwa na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican katika tahariri yake juma hili, kutokana na dhamana kubwa inayoendelea kutekelezwa na Mababa wa Sinodi katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya.

Ni tukio linalowajumuisha Maaskofu, Wageni waalikwa na Watazamaji, kwa pamoja wanashiriki katika sherehe za kuwatangaza watakatifu wapya saba, dhamana iinayotekelezwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Siku ya Kimissionari Duniani, ambayo Mwaka huu inaadhimishwa hapo tarehe 21 Oktoba, 2012. Haya ni matukio ya furaha na mwanga angavu katika maisha na utume wa Mama Kanisa.

Wenye heri hawa wanaotangazwa kuwa Watakatifu ni mfano na kielelezo cha utakatifu wa maisha kwa Kanisa zima. Ni Mapadre, Watawa na Waamini Walei, walioishi: Ulaya, Afrika, Asia, Amerika na Oceania.

Hawa ndio watu waliothubutu kuyamimina maisha yao wakiwa mbali na nchi zao za kuzaliwa kama ilivyojitokeza kwa Myesuiti aliyemwaga damu yake nchini Madagascar; Padre na mwalimu wa vijana waliokuwa wanaishi katika mazingira hatarishi; kwa mgonjwa ambaye alikiona kitanda chake kama Altare ya mahangaiko yake kama thawabu kubwa iliyomwezesha kushiriki mateso yanayokomboa.

Kati yao kuna Katekista kijana kutoka Ufilippini, aliyemwaga damu kwa ajili ya imani yake kwa Kristo pamoja na Mtawa aliyetoa sehemu kubwa ya maisha yake kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa Ukoma, bila ya kuwasahau wale walionesha ushuhuda makini kwa kuwahudumia watoto katika sekta ya elimu na wafanyakazi vijana. Kijana Kateri Tekakwita ni tunda la kwanza kabisa la Uinjilishaji wa awali miongoni mwa Wahindi Wekundu nchini Marekani.

Padre Lombardi anasema kwamba, kwa hakika, tangu mwanzo wa Kanisa, Watakatifu wameendelea kuwa ni mfano hai wa imani ya Kikristo, kielelezo makini cha uwepo endelevu ya roho ya Kristo mfufuka; pamoja na mabadiliko yanayofanyika maisha ya mwanadamu kutokana na kuguswa na Fumbo la Nguvu ya Kiinjili. Bila ya Watakatifu, Kanisa litakufa! na dhamana ya utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu utakuwa ni mgumu hata kukubalika.

Kanisa halina budi kuonesha ile nguvu ya chemchemi ya upendo, furaha na matumaini. Padre Federico Lombardi anahitimisha tafakari yake kwa kusema kwamba, hata dhamana ya Uinjilishaji Mpya katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo inapata chimbuko lake kutokana na Watakatifu wa nyakati hizi.







All the contents on this site are copyrighted ©.