2012-10-20 08:55:18

Uinjilishaji Mpya ujikite katika: Majadiliano ya Kiekumene, Katekesi makini na uchaji katika Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa


Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya wanabainisha kwamba, majadiliano ya kiekumene ni kati ya hitaji msingi la Kanisa wakati huu, kama njia ya kutolea ushuhuda imani na kweli za Kiinjili; changamoto iliyotolewa kwa namna ya pekee na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, miaka hamsini iliyopita.

Majadiliano haya hayana budi kujitika katika ushuhuda, kama njia ya Uinjilishaji Mpya unaopania kutangaza Imani ya Kikristo na kulijenga Kanisa mintarafu maagizo ya Kristo. Hizi ni juhudi zinazokumbatia pia majadiliano ya kitamaduni kwa lengo la kutamadunisha mila na desturi za watu kadiri ya kweli za Kiinjili; huku waamini wenyewe wakitambua dhamana waliyo nayo inayowadai kuwa ni wadau wa Uinjilishaji.

Ili waweze kutekeleza wajibu na dhamana hii wanahitaji kupatiwa majiundo makini kuhusu: imani ya Kanisa inayoungamwa, adhimishwa, mwilishwa na kusaliwa na waamini katika hija ya maisha yao hapa duniani. Mababa wa Sinodi wanasema kwamba, maadhimisho ya Sinodi ni kielelezo cha ushirikiano kati ya Makleri na Waamini katika maisha na utume wa Kanisa, mfano unaopaswa kujionesha hata katika Makanisa mahalia.

Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, anakabiliwa na changamoto zilizoko ndani na nje ya uwezo wake. Mababa wa Sinodi wanataja changamoto hizi kwamba ni pamoja na kuongezeka kwa madhehebu mbali mbali ya Kikristo yanayoingia hasa Barani Afrika yakiwa na nguvu kubwa ya fedha na ushawishi wa miujiza kama njia ya mkato ya kupambana na ukata na hali ngumu ya maisha na kwamba, kila mtu anaweza kujipatia muujiza wake. Watu wanakimbilia zaidi mifumo na vionjo vya kidini lakini bado wanabaki wakavu katika misingi tanzu ya imani.

Kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la waamini wa dini na madhehebu mbali mbali wenye misimamo mikali ya kiimani, mambo yanayohatarisha: haki, amani, utulivu na mafao ya wengi. Baadhi ya Mashirika ya Misaada Kimataifa yanaendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika maisha ya watu Barani Afrika kiasi cha kutia shaka tunu msingi za maisha adili na utu wema.

Kutokana na Kanisa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, maadili na utu wema, limejikuta likikabiliwa na kinzani na sera za kibaguzi katika masuala ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Mababa wa Sinodi wanakazia kwamba, dini na taasisi zake ni sauti ya kinabii inayopaswa kusikilizwa, katika mchakato mzima wa kulinda na kutetea misingi ya haki, amani, utulivu, maadili, utu wema na mshikamano wa kitaifa.

Mababa wa Sinodi wanasema, pengine wimbi la Waamini Wakatoliki kujiunga na madhehebu mengine ya Kikristo ni dalili za kiu na njaa ya uwepo wa Mungu katika maisha yao. Jambo hili lilete msukumo kwa Kanisa Katoliki kuangalia jinsi ambavyo linaadhimisha Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu na ushuhuda katika uhalisia wa maisha. Parokia na Vyama vya kitume vichangamkie dhana ya Uinjilishaji Mpya, kwani hii ni sehemu ya wito na utume wake.

Wahubiri wajitahidi kuandaa kwa umakini Neno la Mungu na kulitangaza kwa ari na moyo mkuu, lakini zaidi, wajitahidi kulimwilisha katika maisha yao ya kila siku, ili liweze kweli kuwa ni taa katika mapito yao. Maaskofu wanakumbushwa kwamba, wanayo dhamana kubwa katika utekelezaji wa mikakati ya Uinjilishaji Mpya katika Makanisa Mahalia.

Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa iwe ni fursa nzuri ya kutangaza na kumwilisha Imani ya Kikristo. Maadhimisho haya yatanguliwe kwanza kabisa na Katekesi ya kina kuhusu: Imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya Nyakati; Sakramenti za Kanisa; Maisha adili yanayopata chimbuko lake katika Amri za Mungu pamoja na maisha ya Sala yanayojikita katika Zaburi na Sala kuu, yaani Sala ya Baba Yetu, ambao kimsingi ni muhtsari wa Mafundisho Makuu ya Yesu.

Mababa wa Sinodi wanamshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa kuwapatia Waamini wa Makanisa ya Mashariki matunda ya Kazi ya Sinodi ya Kanisa Katoliki Mashariki ya Kati. Hii ni changamoto ya kujikita katika Kutangaza Neno la Mungu, kuendeleza huduma za matendo ya huruma; kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa pamoja na kukuza moyo na ari ya sala katika ngazi mbali mbali.

Umoja na mshikamano wa Kanisa ni changamoto endelevu iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, jambo linalopaswa kujionesha kwa namna ya pekee katika maisha ya na utume wa Kanisa. Kanisa la Mashariki kwa miaka mingi limeendelea kutembea katika hija ya ushuhuda wa maisha unaojikita katika madhulumu na mateso ambayo waamini kwa miaka mingi wamekuwa wakikabiliana nayo, lakini bado wakaendelea kubaki waaminifu katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Mashahidi na wafiadini ni mihimili muhimu katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, kwani wao ni kielelezo makini cha imani isiyoteteleka. Kumbe basi, hija zitakazofanyika wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani katika maeneo ya kihistoria yanayogusa kwa namna ya pekee maisha na utume wa Yesu, iwe ni njia ya kujenga na kuimarisha mshikamano katika maisha ya kiroho, kimwili na kiuchumi.

Kanisa liendelee kujibidisha kuhakikisha kwamba, Kashfa ya utengano miongoni mwa wafuasi wa Kristo inahitimishwa kadiri ya mapenzi ya Kristo mwenyewe, ili kwa pamoja waweze kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu pamoja na kuendelea kuwa waaminifu katika misingi ya Injili. Kwa hakika, waamini wanapaswa kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kuchuchumilia utakatifu wa maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.