2012-10-20 09:17:13

Msiendekeze "nyumba ndogo" na "vidumu" kumbukeni kwamba, Familia ina dhamana ya Kujiinjilisha na Kuinjilishwa!


Askofu mkuu Peter Kairo wa Jimbo kuu la Nyeri, Kenya ni kati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji aliyeonesha kuguswa kwa namna ya pekee na matatizo na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Familia kwa sasa zinakabiliwa na kinzani katika tunu msingi za maadili na utu wema. Matokeo yake ni familia nyingi zinajikuta zinasambaratika hata katika uchanga wake; baadhi ya wanafamia wamejikuta wanaendekeza uchumba sugu kiasi kwamba, wazo la kufunga ndoa kwao ni msamiati mgumu.

Baadhi ya ndoa zinalega lega kutokana na kukosekana kwa uaminifu na utamaduni wa mapendo ya dhati kiasi kwamba, upendo huu unachangiwa kwa kukumbatia dhana ya wake wengi; ukosefu wa uaminifu kwa kuendekeza "nyumba ndogo" au "vidumu". Kutokana na uwepo wa ndoa tenge, baadhi ya wazazi na hasa wanawake wamejikuta wakibeba jukumu kubwa la malezi pamoja na kuziwezesha familia zao.

Askofu mkuu Kairo anasema, ingawa wanandoa ni watu wanaopaswa kuishi kwa pamoja katika maisha yao yote hadi kifo kinapowatengenanisha, lakini wamejikuta mara nyingi hawana maandalizi ya kutosha wala kupata majiundo endelevu mara baada ya kufunga ndoa. Huu ni udhaifu mkubwa unaopaswa kurekebishwa mapema kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya, ili Familia ziweze kutekeleza wajibu na dhamana yake kama mhimili mkuu wa Uinjilishaji ndani ya Kanisa kwa kupania kuyatakatifuza malimwengu.

Masuala ya kiuchumi pamoja na ajira ni mambo yanayoitendea familia katika kujenga na kuimarisha mshikamano wake wa upendo, kwani kuna baadhi ya wanandoa wanajikuta wakiishi mbali na wenzi wao kutokana na sababu za kiuchumi au kikazi, hapa kuna hatari kwa wanandoa "kuteleza na kuanguka majaribuni". Familia za Kikristo wakati mwingine zimeendelea kukumbatia pia mila na desturi za makabila yao kiasi cha kupoteza utambulisho wake wa Kikristo.

Uinjilishaji Mpya uziwezeshe Familia kujenga na kuimarisha utamaduni wa upendo, sanaa ya kusikilizana na kushirikishana, kwa kutambua kwamba, wao ni sehemu nyeti ya maisha na utume wa Kanisa, inayopaswa kupendwa, kuthaminiwa na kuendelezwa. Wakristo wafahamu maana ya ndoa ya Kikristo kadiri ya mpango wa Mungu, Mafundisho ya Kanisa; Utu na Maadili mema.

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani lenye dhamana ya kujiinjilisha ili liweze kuiinjilisha pia. Ili utume huu uweze kukolea katika maisha ya waamini, kuna haja ya kutubu, kuongoka na kuchuchumilia utakatifu wa maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.