2012-10-20 08:14:41

IMBISA inavyocharuka katika utekelezaji wa mikakati ya kujitegemea kwa: rasilimali watu, fedha na miundo mbinu!


Kardinali Wilfred Napier, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA anasema kwamba, IMBISA iliundwa kunako mwaka 1970, ili kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki Kusini mwa Afrika, hususan katika masuala ya: rasilimali watu, maendeleo ya miundo mbinu pamoja na uwezekano wa kupata fedha kama sehemu ya mchakato wa kujitegemea na kulitegemeza Kanisa Kusini mwa Afrika.

Katika hija ya uhai wake, IMBISA imekuwa ikijikita katika tafakari za kina zinazogusa changamoto walizonazo na kwa namna ya pekee, katika kupambana na baa la umaskini ambalo ni kikwazo kikubwa cha maendeleo kiroho na kimwili, kwa kutumia rasilimali iliyopo katika eneo hili. Kunako mwaka 2001, Maaskofu wa IMBISA walikaa kitako ili kuibua mbinu mkakati wa kichungaji uliolenga: kuibua, kuchanganua hali ya kijamii, kufanya tafakari ya kina kuhusu masuala ya kitaalimungu na hatimaye, kubainisha mikakati ya kichungaji ambayo ingetumiwa na IMBISA ili kukabiliana na changamoto zake.

Kardinali Napier akichangia mada kwenye maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya anasema kwamba, kunako mwaka 2004, wakati wa mkutano wao wa Mwaka, waliibua mbinu mkakati wa kupambana na umaskini pamoja na kujijengea uwezo wa kulitegemeza Kanisa katika masuala ya rasilimali watu, miundo mbinu na rasilimali fedha. Maaskofu wakajiwekea lengo la kupunguza umaskini kwa asilimia kumi na tano ifikapo mwaka 2007.

Matokeo yanaonesha kwamba, Majimbo mengi ya IMBISA yaliweza kujitegemea hasa kutokana na kuwa na utawala bora na kwamba, wakiendelea kuimarisha mikakati yao, kwa kiasi kikubwa wataondokana na saratani ya kutegemea misaada kutoka nchi za nje, kwa kuzingatia utawala bora na maadili ya kazi. Kwa sasa, IMBISA inaendelea kushughulikia na kumwilisha changamoto zilizoibuliwa na Mababa wa Sinodi za Afrika pamoja na Sinodi ya Uinjilishaji Mpya, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yanayopania kwa namna ya pekee, kurithisha Imani ya Kikristo.

Maaskofu wa IMBISA wamejiwekea mikakati ya kuhakikisha kwamba, Familia ya Mungu Kusini mwa Afrika inajenga na kuimarisha urafiki wake na Yesu Kristo sanjari na kutumia kwa ukamilifu Mapaji na Karama walizojaliwa na Roho Mtakatifu. Uchunguzi wa maisha ya kiroho kwa siku za hivi karibuni anasema Kardinali Napier, umebaini kwamba, waamini wamejenga na kukoleza ari na moyo wa sala, tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya huruma na kwamba, Parokia kwa sasa ni chemchemi ya Uinjilishaji wa kina.

Utume huu unafanywa kwa njia ya Katekesi endelevu, majiundo makini kwa wanandoa watarajiwa, maandalizi ya kupokea Sakramenti za Kanisa pamoja na kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili, ili kweli Kanisa Kusini mwa Afrika liweze kuwa ni Familia ya Mungu inayowajibika.







All the contents on this site are copyrighted ©.