Sanaa na Utamaduni ni chanda na pete: Tume ya Kipapa na Utamaduni pamoja na Mambo
ya Kale kuunganishwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kunako tarehe 30 Julai 2012 ametia sahihi
kwenye hati ijulikanayo kwa lugha ya Kilatini Pulchritudinis Fidei inayounganisha
Tume ya Kipapa ya Utamaduni na Mambo ya Kale pamoja na Baraza la Kipapa la Utamaduni
ambalo kwa sasa liko chini ya uongozi wa Kardinali Gianfarnco Ravasi. Uamuzi huu utaanza
kutekelezwa hapo tarehe 3 Novemba 2012.
Kuundwa kwa Tume hii yalikuwa ni matunda
na changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika ile
Hati ya Kichungaji inayozungumzia Kanisa Ulimwenguni, Gaudiu et Spes. Baba Mtakatifu
Yohane Paulo wa Pili wakati wa uongozi wake, aliunda Taasisi mbili ambazo kimsingi
zilipewa jukumu la kuendeleza majadiliano ya kina na tamaduni pamoja na sanaa zinazofumbata
utajiri wa imani na maisha ya Kikristo.
Baraza la Kipapa la Utamaduni, likaundwa
na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili kunako tarehe 20 Mei 1982 na hivyo kulitenganisha
na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini lililopewa dhamana ya kukoleza mchakato
wa majadiliano ya kidini na wale wasioamini.
Tume ya Kipapa kwa ajili ya Utamaduni
na Mambo ya kale iliundwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili kunako tarehe 25
Marchi 1993. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1952 Papa Pio wa Saba alikuwa ameunda
Tume kuu ya Sanaa Takatifu.
Baadaye, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili,
akaifanyia mabadiliko kunako tarehe 28 Juni 1988 kwa kuipatia jukumu la kuwa ni Tume
ya utunzaji wa urithi wa sanaa na historia ya Kanisa na kuiweka chini ya Baraza la
Kipapa kwa ajili ya Makleri. Baba Mtakatifu akahimiza uhusiano wa dhati kati ya Mabaraza
haya kwa ajili ya mafao ya Kanisa.