SALAAM ZA MAASKOFU WA KKKT KWA WATANZANIA WOTE KUHUSIANA NA MATUKIO YA KUCHOMA MOTO
MAKANISA YA KIKRISTO ENEO LA MBAGALA – DSM.
Wapendwa Katika Bwana,Waumini wa KKKT, Wakristo Wote na Watanzania kwa Ujumla. Neema
na Iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba na Bwana wetu Yesu Kristo, Amina.
Sisi
maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), tumepokea kwa mshtuko
mkubwa taarifa za matukio ya uchomaji wa makanisa katika eneo hili la Mbagala. Tumekuwa
katika mkutano wetu wa Mwaka wa Lutheran Mission Cooperation (LMC) huko Moshi pamoja
na vyama vyote vya Kimissioni vya Ulaya na Marekani. Tumelazimika kukatisha mkutano
huo ili kufika hapa Mbagala.
Tumekuja kwa madhumuni makubwa matatu:
Tumekuja
kuwapa pole na kusimama pamoja nanyi katika uchungu mkubwa mlio nao. Machozi yenu
ni machozi yetu. Machozi yetu ni machozi ya Kristo mwenyewe aliye Bwana wa kanisa
linaloteswa. Jipeni moyo kwa kuwa yeye aliushinda ulimwengu (Yohana 16:33). Tumekuja
kuonyesha majonzi yetu makubwa kwa vitendo vya uvunjifu wa amani, kuporomoka kwa umoja
na mshikamano wa watanzania. Huu ni msiba mkubwa, na wenye msiba ni watanzania wote,
wenye dini na wasio na dini. Tumekuja kushiriki pamoja nanyi kupokea matumaini
ya Tanzania mpya. Katika majivu haya yaliyotokana na kuchomwa kwa madhabahu ya Mbagala,
Tanzania mpya itazaliwa. Majivu haya na machozi yenu ni rutuba ya Tanzania mpya itakayojali
upendo, uvumilivu, ustahimilivu, umoja, mshikamano, uhuru wa kuabudu na dola isiyo
na dini.
Katika ujio huu wa maaskofu hapa Mbagala, hatukuja hapa
kufanya hayayafuatayo:
Hatukuja kuwahukumu hata kama hatukubaliani
na wanaokashifu dini za wenzao, wawe na ruhusa kutoka mamlaka zilizo juu au kama wanajituma
wenyewe. Hatukuja kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaodhalilisha misahafu
ya dini; wawe wametumwa, kutegeshewa na mamlaka zozote au kwa misukumo ya utashi wao
binafsi ili kupata kisingizo cha kugombanisha madhehebu ya dini. Hatukuja kuwahukumu
hata kama hatukubaliani na wanaochoma makanisa na kuiba mali za makanisa kwa kisingizio
cha kumtetea Mungu. Kisasi cha dhambi hiyo tunamwachia Mungu mwenyewe aliyedhihakiwa
na walionajisi madhabahu yake.
Wapendwa wana KKKT na watukuka sana,
wana na mabinti wa Tanzania ya Julius Kambarage Nyerere; kilichotokea Mbagala katika
wiki ya kuadhimisha siku ya Baba wa Taifa, ni kebehi si kwa Baba wa Taifa bali ni
kebehi kwetu sisi wenyewe tunaokalia kiti alichokalia Baba wa Taifa. Yeye amelala
baada ya kazi njema. Apumzike kwa amani na tunu zake zifufuke katika majivu haya yaliyotokana
na kuchomwa kwa amani na mshikamano wa Tanzania aliyoijenga.
Kilichotokea Mbagala
ni mateso ya kimbari, yaani mateso ya Kanisa (Persecution). Mateso haya ni matokeo
ya mbegu ya magugu iliyopandwa katika bustani njema na sasa magugu hayo yanazaa matunda
machungu. Dalili za mateso ya kimbari kama ilivyo kwa mateso ya kanisa; zilianza kitambo
na hazikushughulikiwa na waliomrithi Baba wa Taifa. Dalili hizo ni kama hizi zifuatazo:
Uchochezi wa wazi kuwa taifa hili linaendeshwa na unaoitwa “mfumo
Kristo”, na kuwa Baba wa Taifa alaaniwe kwa yote aliyolitendea taifa hili. Ubishi
usio na tija juu ya idadi ya waumini wa dini mbalimbali hapa nchini na hata kudiriki
kushawishi na kugomea zoezi la sensa ya watanzania. Lengo la ubishi huu ni mbegu inayoweza
kuratibisha na kurasmisha mateso ya kimbari na mateso ya kanisa. Matumizi mabaya
ya baadhi vyombo vya habari, vyenye lengo la kujenga hofu ya kudumu na migawanyiko
ya kidini miongoni mwa watanzania Ukimya wa vyombo vya dola juu ya vitendo vya
uvunjaji wa sheria ya matumizi ya vyombo vya habari. Kwa vyovyote vile, uvumilivu
wa dola hauna maslahi mapana kwa mustakabali wa taifa letu na ni mateso ya kimbari,
mateso kwa kanisa, na kwa wantanzania wote; wawe wengi dhidi ya wachache au wachache
dhidi ya wengi. Madai yasiyo ya kawaida na ya mara kwa mara kwa serikali inayodaiwa
kutokuwa na dini. Madai hayo ni kama:
Kulazimisha
uvaaji wa alama za kidini katika taasisi za umma ili kurahisisha na kuratibisha tofauti
za watanzania. Tunajiuliza: Likitokea la Mbagala katika mashule yetu na vyuo vya umma,
watachomwa wangapi na kuuawa wangapi? Madai yanayojirudiarudia kutaka balozi za
nchi fulani kufungwa hapa nchini. Madai haya yanaashiria kutaka balozi za nchi fulani
tu ndiyo ziwe hapa nchini. Madai na mashinikizo ya Uanzishwaji wa mahakama za kidini
hapa nchini Mashinikizo ya kidini yanayoingilia mifumo ya kitaaluma na kisheria. Mashinikizo
ya kidini juu ya mfumo wa uteuzi wa watendaji wa serikali na katika ofisi za umma, Kuhoji
na kupotosha juu ya ushirikiano wa serikali na mashirika ya dini katika utoaji wa
huduma za kijamii hususan afya na elimu hapa nchini
Wapendwa wana
KKKT na Wapendwa watanzania wote. Hata kama wanaofanya mambo haya ya kusikitisha wametunukiwa
hadhi ya kuitwa kuwa ni “wana harakati”, tofauti na wanaharakati wanaotambuliwa na
watanzania walio wengi, tunawiwa kuonya kwa uvumilivu wote kuwa uana harakati wao
usitumike kuvunja nchi na sheria za nchi. Tanzania yenye amani na mshikamano ni tunda
la dini zote, makabila yote, itikadi zote za vyama, rangi zote na hali zote za kiuchumi.
Hata wasio na dini wanachangia amani ya nchi hii.
Kwa macho na masikio yetu,
tumeendelea kushuhudia vitendo vya uchomaji makanisa huko Zanzibar, Mwanza, Mdaula,
Mto wa Mbu, Tunduru, Rufiji, Kigoma na sasa Mbagala. Wakati wote uvumilivu wa wakristo
huenda umetafsiriwa kuwa ni unyonge na woga. Ikumbukwe kuwa hata wanyonge na
waoga, hufika wakati wakasema “sasa basi” pale wanapodhalilishwa kupita kiasi. Hatuombei
wakristo wafikishwe hapo.
Tumeshuhudia wizara zetu zikivamiwa mchana
kweupe na kushinikiza kuachiwa kwa watuhumiwa wa uhalifu; tumeshuhudia vituo vya polisi
vikichomwa moto; mahakama zikilazimishwa kufunga shughuli zake, misikiti ikitekwa,
uhai wa viongozi wa dini ukitishiwa hadharani na viongozi wastaafu wakizabwa vibao
hadharani kwa sababu ya zinazoitwa harakati za kidini. Tumefikia kuhoji, watu hawa
wavamie nini ndipo hatua zichukuliwe? Wachome nini ndipo viongozi wenye dhamana ya
kulinda mali na uhai washtuke? Wamwue nani ndipo iaminike kuwa watu hawa ni tishio
kwa usalama wa taifa letu?
Sisi tulioitwa kwa njia ya nadhiri na viapo vitakatifu,
tunawasihi sana waumini wa dini zetu na watanzania kwa ujumla, wenye wajibu wa kututii
na wasiolazimika kututii, kuzingatia kuwa Mwenyezi Mungu analipenda taifa hili na
watu wake. Kamwe hawezi kuliacha liangamie.
Kwa Wakristo wote, huu ni wakati
wa kuendelea kufunga na kuomba kwa ajili ya amani ya taifa hili. Mkristo wa kweli
ni yule aliye tayari kuteswa kwa ajili ya Kristo na kanisa. Wakristo hatuko tayari
kuua, kutesa, kulipiza kisasi ili kumtetea Kristo. Mungu wetu hatetewi kwa kuua wengine
na kuchoma madhabahu ya dini nyingine.
Katika mateso haya, kanisa litaimarika
zaidi; na katika majivu haya ya Mbagala, Tanzania mpya itazaliwa na ukombozi wa kweli
utapatikana. Tunawataka wakiristo wote kusamehe na kuendelea kuwa raia wema. Kushiriki
kikamilifu katika kuleta mabadiliko ya kweli kwa kupitia njia sahihi zilizowekwa.
Wakati wengine wanaweka mikakati ya kuchoma madhabahu, wakiristo tuweke mikakati ya
kuomba na kushiriki vema katika haki zetu za uraia. Pamoja na kuwa wapole kama njiwa,
imetupasa pia kuwa na busara kama nyoka (Mathayo 10:16).
Daima tukumbuke
kuwa, “KUSHINDANA KWETU SISI SI JUU YA DAMU NA NYAMA BALI NI JUU YA FALME NA MAMLAKA,
JUU YA WAKUU WA GIZA HILI, JUU YA MAJESHI YA PEPO WABAYA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO”
(Waefeso 6: 12).
Ni sisi Maaskofu wenu kwa Neema ya Mungu,
Askofu Dr.
Alex G. Malasusa – Mkuu, KKKT na D/Mashariki na Pwani Askofu Dr. Stephen Munga
–Mkuu, D/Kaskazini Mashariki Askofu Dr. Martin Shao – Mkuu, D/Kaskazini Askofu
Dr. Thomas Laizer – Mkuu- D/Kaskazini Kati Askofu Dr. Benson Bagonza- Mkuu, D/Karagwe Askofu
Isaya J. Mengele – Mkuu, D/Kusini Askofu Levis Sanga – Mkuu- D/Kusini Kati Askofu
Elisa Buberwa – Mkuu –D/Kaskazini Magharibi Askofu Andrew Gulle – Mkuu, D/Mashariki
ya Ziwa Victoria Askofu Michael Adam –Mkuu, D/Mkoani Mara Askofu Renard Mtenji
– Mkuu, D/Ulanga-Kilombero Askofu Dr. Israel-Peter Mwakyolile – Mkuu, D/Konde Askofu
Job Mbwilo – Mkuu, D/Kusini Magharibi Askofu Dr. Owdenburg Mdegella- Mkuu, D/Iringa Askofu
Jacob Ole Mameo- Mkuu, D/Morogoro Askofu Zebedayo Daudi – Mkuu, D/Mbulu Askofu
Paulo Akyoo – Mkuu, D/Meru Askofu Charles Mjema – Mkuu, D/Pare Askofu Mteule
Amon Kinyunyu- Mkuu, D/Dodoma Askofu Mteule Dr. Alex Mkumbo- Mkuu, D/Kati