2012-10-19 10:39:05

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu kuwatangaza Wenyeheri Saba kuwa Watakatifu


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Siku ya Kimissionari Duniani, hapo tarehe 21 Oktoba 2012, katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Mjini Vatican anatarajiwa kuwatangaza wenyeheri wafuatao kuwa watakatifu:

1. Jacques Berthieu, Padre kutoka Shirika la Wayesuit, Shahidi. Aliishi kunako mwaka 1838 hadi mwaka 1896. Baada ya masomo na majiundo yake ya kipadre, alipadrishwa kunako tarehe 21 Mei 1863. Anakumbukwa sana kutokana na majitoleo yake kwa: maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii. Alikuwa ni mwalim makini wa Katekesi aliyetoa huduma za Sakramenti za Kanisa bila kuchoka huko Madagascar.

Ni Padre aliyepednwa na kuthaminiwa na waamini pamoja na watu waliokuwa wanamzunguka, kutokana na unyofu na matumizi makini ya mali; huduma kwa wahitaji na imani thabiti iliyokuwa na mguso wa pekee kabisa. Alionesha mshikamano wa dhati na wananchi wa Madagascar hasa katika nyakati za shida na mahangaiko.

Kunako mwezi Juni 1896 Padre Berthiu alivamiwa na majambazi, wakimlazimisha kukana imani yake kwa Kristo, lakini alikataa katu katu na kukubali kuyamimina maisha yake kuliko kuisaliti imani yake. Akafariki dunia kunako tarehe 8 Juni 1896 kwa kupigwa risasi kichwani.

2. Pedro Calungsod, Katekista Mlei, Shahidi. Ni katekista kijana kabisa, aliyeishi kati ya Mwaka 1655 hadi mwaka 1672, nchini Ufilippini alikubali zawadi ya imani na kuikumbatia katika ujana wake, lakini baada ya muda mfupi baadhi ya watu walipandikiza chuki za kidini kwa kusema kwamba, Maji ya Ubatizo yalikuwa na sumu, jambo ambalo lilichochea madhulumu dhidi ya Wamissionari.

Katika harakati za kutoa Sakramenti ya Ubatizo Kijijini kwake, watu wenye hasira walimvamia Padre Diego Luis de San Vitores na kumuua. Katekista Pedro Calungsod alikuwa na fursa ya kuwatoroka watesi wake, lakini aliamua kubaki ili kuonesha mshikamano wa imani na Padre Diego, kiasi cha kukubali kupokea kifo kama kielelezo cha imani yake kwa Kristo. Miili ya viongozi hawa wa Kanisa ilitupwa Baharini na masalia yao hayakuweza kamwe kupatikana.

Padre Diego Luis de san Vitores alitangazwa kuwa Mwenyeheri kunako tarehe 6 Oktoba 1985 na Katekista Pedro Calungsod alitangazwa kuwa Mwenyeherui hapo tarehe 5 March 2000 na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili.


3. Giovanni Battista Piamarta, Mwanzilishi wa Shirika la Familia Takatifu ya Nazareti na Masista Wadogo wa Bwana aliyeishi kati ya Mwaka 1841 hadi mwaka 1913. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, alipadrishwa kunako tarehe 23 Desemba 1865. Kwa takribani miaka ishirini na mitano alionesha umahiri mkubwa katika shughuli za kichungaji Parokiani, akajitoa bila ya kujibakiza kuwasaidia vijana waliokuwa wanakumbwa na adha kutokana na mchakato wa maendeleo ya viwanda nchini Italia nyakati hizo.

Kunako mwaka 1886 alianzisha Taasisi ya ufundi ili kutoa ujuzi, elimu, maarifa ya kazi na maisha ya Kikristo, akiwalenga zaidi vijana waliokuwa wanatoka kwenye Familia Maskini zaidi. Alisaidia harakati za kuwanoa waandisi wa Kikristo katika sekta ya Kilimo, iliyopata mafanikio makubwa huko Brescia. Alianzisha Mashirika ya Kitawa kwa Wanaume na Wanawake; akajenga kiwanda cha uchapaji, kiasi cha kuchangia kwa kiasi kikubwa, kuibuka kwa Viwanda vya uchapaji vilivyokuwa vinamilikiwa na kuendeshwa na Parokia nchini Italia na Ulaya kwa ujumla wake.

Padre Giovanni Battista Piamarta aliongozwa na kauli mbiu "Yote kwa ajili ya binadamu wote", akaishi maisha ya kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya mafao ya jirani zake, akidumu katika sala na akafariki dunia hapo tarehe 25 Aprili 1913.

4. Maria Carmen Salles Barangueras, Mwanzilishi wa Shirika la Masista Waamissionari wa Mafundisho ya Kanisa wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, aliishi kati ya Mwaka 1848 hadi mwaka 1911. Alibahatika kuzaliwa katika Familia ya Kikristo iliyokuwa na Ibada kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Ni mtu aliyependa kuomba ushauri kutoka kwa wakuu wake kabla ya kufanya maamuzi makubwa.

Kunako mwaka 1869 alijiunga na Shirika la Masista Waabuduo Ekaristi Takatifu. Akiwa Shirikano humo, aligundua elimu kama njia ya kupata mwanga wa Fumbo la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Kunako mwaka 1870 alijiunga na Shirika la Masista wa Kupashwa Habari la Wadomenikani, alikoishi kwa miaka ishirini na miwili. Tarehe 15 Oktoba 1982 Sr. Carmen na Kikundi chake waliwasili Jimboni Burgos na tarehe 7 Desemba 1982 wakaanzisha Shirika na kupewa dhamana ya kufungua shule. Katika maisha yake, alifungua nyumba kumi na tatu. Ni Shirika ambalo limeendelea kutoa huduma nchini Brazil na Italia.

Daima alipenda kuwainjilishaji vijana pamoja na kurithisha tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu kwa wanafunzi waliobahatika kupata elimu katika shule alizozianzisha. Alifariki dunia tarehe 25 Julai 1911 na kutangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 15 Marchi 1998. Leo hii Shirika hili limeenea katika nchi kumi na sita duniani.

5. Marianne Cope, Mtawa wa Shirika la Masista wa Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Francisco wa Syracuse, alizaliwa huko Ujerumani, lakini baadaye Familia yake ilihamia Ujerumani. Aliishi kati ya mwaka 1838 hadi mwaka 1918. Alijiunga na Shirika la Masista wa Mtakatifu Francis wa Syracuse kunako mwaka 1862. Alikuwa ni mwalimu na alibahatika kuanzisha Hospitali mbili, hasa kwa ajili ya wagonjwa wa Ukoma, uliokuwa unatisha wakati huo.

Alijitoa kimasomaso kuwahudumia wakoma kwa takribani miaka thelathini, akwamegea upendo na huduma ya Injili. Akafariki dunia kunako tarehe 9 Agosti 1918, huku akipewa heshima kuwa ni "Mama wa wanyonge na wasiopendwa".Alitangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 14 Mei 2005.

6. Kateri Tekakwitha, Mlei, aliyeishi kati ya Mwaka 1656 hadi mwaka 1680, huko New York, Marekani. Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kunako mwaka 1676 alibatizwa na tangu wakati huo akaboresha uhusiano wake na Kristo Msulubiwa, kiasi kwamba, akakataa kuolewa na Kijana aliyekuwa amechaguliwa na kabila lake, ili kuimarisha uhusiano ambao alikuwa ameujenga na Kristo kwa njia ya Ubatizo. Uamuzi huu ulimgharimu sana kiasi cha kutishia usalama wa maisha yake, hali ambayo ilipelekea Kateri kuhamia Kijiji kingine.

Mwaka 1677 alipokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza na kwa kipindi cha miaka mitatau aliishi kijijini hapo akijitahidi kumwilisha Injili ya Upendo kwa wagonjwa na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii. Tarehe 24 Marchi 1679 baada ya kupata ushauri wa kina kutoka kwa Padre wake wa kiroho, akaamua kujiweka wakfu kwa kukumbatia usafi kamili na akatambuliwa na Mama Kanisa kuwa ni kielelezo na mfano wa kuigwa kwa Wahindi Wekundu, Amerika ya Kaskazini. Tarehe 17 Aprili 1680 alifariki dunia akionesha upendo wa hali ya juu kwa Yesu

7. Anna Schaffer, Mlei aliyeishi kunako mwaka 1882 hadi mwaka 1925, ni mtu aliyeonja mateso makali na umaskini wa kutisha, lakini alikuwa na upendo mkubwa kwa Mungu na jirani, akatambua kwamba, alikuwa na wito wa kushuhudia mateso yanayokoa. Aliimarishwa katika hija ya maisha yake hapa duniani kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Akaeneza Ibada kwa Ekaristi Takatifu kwa njia ya sala na machapisho mbali mbali. Alifariki dunia tarehe 5 Oktoba 1925. Kwa hakika alijitahidi kuliishi kwa ukamilifu Fumbo la Msalaba, alilolipenda na kulipokea kwa moyo wa shukrani, akawa ni kielelezo cha wote wanaoteseka kiroho na kimwili.







All the contents on this site are copyrighted ©.