2012-10-19 14:47:59

HIJA JIMBO KUU LA MWANZA MWAMKO MPYA WA IMANI NA MAHUSIANO KINA!


Waamini wa Kanisa mahalia, Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, wameaswa kutokuwa na ubaguzi au kudharau na kubeza utu au imani ya mtu awaye yote. Hata wale ambao hawajalipokea Neno la Bwana, wana thamani mbele za Mungu, nao wana kiu na shauku ya kumwambata Mwenyezi Mungu.
Dunia na watu wa sasa hawatofautiani sana na mfalme Naamani kutoka Siria, ambaye alifunga safari kwenda Israeli kumtafuta nabii Eliya ili amponye na ukoma. Naye nabii Eliya hakumbeza bali alimpokea na kumshauri afanye hija kwenda mto Yordani ili ajitakase na ukoma naye akapona. Binadamu leo anao ukoma wa mwili, ukoma wa roho, ukoma wa imani, ukoma wa mahusiano kwa kuruhusu dhambi kumsakama na kusababisha mmong'onyoko wa maadili.
Mafundisho hayo yametolewa na Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi, wa Jimbo kuu la Mwanza katika kilele cha hija ya Jimbo kilichoadhimishwa mnamo 16 Oktoba 2012 katika viwanja vya kilima cha Kawekamo ambapo kuna madhabahu ya Bikira Maria Malkia wa Kawekamo.
Nia ya hija hiyo kwa mwaka huu 2012 ilikuwa: kufungua rasmi mwaka wa imani kijimbo wakiungana na Baba Mtakatifu aliyetangaza rasmi mwaka wa imani tarehe 11 Oktoba 2012, na kufungua sinodi ya maaskofu juu ya uinjilishaji mpya; kumuenzi mwenye heri Yohane Paulo wa pili ambaye alifika katika kilima hicho tarehe 4 Septemba, 1990 na kuadhimisha Misa Takatifu, kutoa Sakramenti ya ubatizo, komunyo ya kwanza, kubariki ndoa na kuombea wagonjwa; na nia ya tatu ilikuwa kubariki ufunguzi rasmi wa ujenzi wa Kanisa kuu jipya la jimbo ambalo msimamizi wake atakuwa mwenye heri Yohane Paulo wa pili.
Hija hiyo ilianza saa 3 asubuhi ya tarehe 15 Oktoba 2012 kutokea Parokia ya Mt. Yosefu Mkasa, Nyakato kuelekea kilima cha Kawekamo ambako mahujaji wote wa jimbo walipokelewa na Askofu mkuu Ruwa’ichi na mapadri majira ya saa nane mchana. Kisha wakatafakari njia ya msalaba, Misa Takatifu kwa heshima ya Bikira Maria, kukawa na mada, Tafakari ya Rosari Takatifu, muhtasari wa Injili, Sakramenti ya Upatanisho, Misa Takatatifu ya mkesha, kuabudu Ekaristi Takatifu mpaka asubuhi ambapo hija hiyo ilihitimishwa kwa Misa Takatifu ya Shukrani.
Watoa mada, Mheshimiwa Pd Richard Makungu, makamu wa askofu mkuu aliongelea juu ya nafasi ya Bikira Maria katika Kanisa Katoliki; mheshimiwa Pd Bonaventura Kamuli alifundisha juu ya maana ya hija na umuhimu wa kuabudu Ekaristi Takatifu; Pd Celestine Nyanda alichambua mchakato wa utangazaji wenye heri na watakatifu kisha mahusiano ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili na madhabahu ya Bikira Maria Malkia wa Kawekamo; na Bwana Josephat Nkigwa alipembua nafasi ya vyama vya kitume katika ujenzi wa Kanisa mahalia.
Askofu mkuu Ruwa’ichi akifafanua nia za hija hiyo alimuelezea Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, Papa, kama mtu wa Mungu, mtu wa imani, upendo, kujitoa na mwenye bidii ya kazi. Mfano wa maisha yake ulipelekea vijana na watoto wengi waliokusanyika katika viwanja vya Mtakatifu Petro mjini Vatican, kuomba kwa sauti moja atangazwe mtakatifu “santo subito”. Askofu Ruwa’ichi akatolea mfano wa maisha ya Mwenyeheri Yohane Paulo aliyejitoa kikamilifu “totus tuus” na amewaalika waamini wote kutokuwa na woga kuuchuchumilia utakatifu, kuienzi na kuifundisha imani yao na kuwa tayari kumjengea Mungu Kanisa. Bali waifungue milango ya mioyo yao kwa Kristo.
Mapadri, watawa na waamini wote wajipange kuzama kwa kina katika katekesi ya imani katoliki katika mwaka huu wa imani. Takribani miaka 50 tangu kufunguliwa rasmi kwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Askofu mkuu Ruwa’ichi amewaalika mapadri, watawa, makatekista, waamini na hasa katika Jumuiya ndogondogo wawe na nakala za hati za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ili kuyazingatia upya mafundisho ya mababa hao. Na ikiwa miaka 20 tangu Kanisa kuzawadiwa muhtasari wa imani katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki, nakala hizo na mafundisho hayo yatiliwe maanani katika Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo.
Ikumbukwe kuwa ni takribani miaka 150 sasa tangu kundi la pili la Wamisionari liingie Tanzania na kufanikisha Uinjilishaji tangu 1863. Askofu Mkuu Ruwa’ichi amewaalika waamini wote kuifurahia, kuiadhimisha, kuizamia na kuihangaikia imani yao. Ikumbukwe tena ya kwamba ni takribani miaka kumi sasa tangu jimbo kuu la Mwanza liadhimishe Sinodi ya kwanza kijimbo. Na kwa kadiri ya maazimio nambari 137 & 138 ya Sinodi hiyo, kunapaswa kuwa na tathmini ya sinodi hiyo baada ya miaka kumi, tathmini inayoendelea kwa sasa jimboni humo. Askofu Ruwa’ichi amesisitiza kuitilia maanani tathmini hiyo kwa ufundi na umakini huku wakijikita zaidi katika uinjilishaji wa kina.
Uzinduzi wa kazi ngumu ya ujenzi wa kanisa kuu la jimbo ambalo ni ishara ya Kanisa mahalia, ambapo ndipo panapokuwa na kiti cha askofu jimbo. Kanisa hilo ni Nyumba ya Mwenyezi Mungu na hivyo inafaa kujitoa kwa moyo, imani na mapendo huku wakijikabidhi kwa Kristu mwenyewe aliye kichwa cha kanisa. Nia ya ujenzi wa kanisa hilo kuu ulianza tangu enzi za Askofu Joseph Blomjous miaka ya 1950. Nia iliyorithiwa na askofu Renatus Butibubage askofu wa kwanza mzalendo. Mchakato na nia ya ujenzi wa Kanisa hilo ulipamba moto wakati wa utume wa askofu mkuu Antony Petro Mayala, ambaye tarehe 19 Agosti 2009 siku mbili kabla ya kutia saini na msanifu majengo na mkandalasi ili kuanza ujenzi huo alifariki dunia.
Askofu mkuu Ruwa’ichi amewahimiza wamini kujifunza kutoka nabii Hagai anayewaonya wana waisraeli kuwa si jambo jema kuishi katika nyumba zilizopambwa na kupendeza huku Nyumba ya Bwana haipo imara na katika hali inayosthili (Rej. Hagai 1.4).
Wana Jimbo Kuu la Mwanza wanapoendelea kumuomba Mwenyezi Mungu afanikishe nia zao za hija mwaka huu ikiwa ni pamoja na changamoto za ujenzi wa Kanisa hilo, wanawaalika wote wenye mapenzi mema kuchangia ujenzi wa Kanisa hilo kwa sala, maombi na michango mbalimbali. Waweza kuchangia mchango wako kupitia (MKOMBOZI COMERCIAL BANK PLC, KAWEKAMO CATHEDRAL, A/C No 00311401126401). Na kwa mawasiliano zaidi bonyeza nambari ya simu au ‘fax’ +255 28 250 1029, email .

Na Pd. Celestin Nyanda
Mwanza, Oktoba 16, 2012.








All the contents on this site are copyrighted ©.