Familia, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo na Vyama vya Kitume ni nyenzo msingi katika
Uinjilishaji mpya na ule wa kina Barani Afrika!
Bwana Joakim Kipyego Koech ni mwamini mlei kutoka Chama cha Kitume cha Comunal and
liberation, kinachotekeleza utume wake nchini Kenya. Ni kati ya Mababa wanaoishi katika
Sinodi ya Uinjilishaji Mpya inayoendelea hapa mjini Vatican.
Akihojiwa
na Radio Vatican anabainisha kwamba, ameguswa kwa namna ya pekee, kwa jinsi ambavyo
Mababa wa Sinodi wanavyojadili kwa kina na mapana kuhusu mustakabali wa Kanisa kwa
sasa na kwa siku za usoni kwa kuonesha matumaini makubwa licha ya matatizo, changamoto
na fursa mbali mbali zinazojitokeza.
Anasema, mkazo wa Mababa wa Sinodi kuhusu
Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, Vyama vya Kitume pamoja na Familia unaonesha dhamana
kubwa ambayo waamini wanatakiwa kuitekeleza katika maisha na utume wa Kanisa, wakati
wa mchakato mzima wa Uinjilishaji mpya na ule wa kina kwa Familia ya Mungu Barani
Afrika.
Waamini walei kwa kushirikiana na viongozi wa Kanisa na Jamii kwa
ujumla wake, wajibidishe kukuza, kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia,
ili hata watoto na vijana ndani ya Familia zao waonje kweli uwepo wa Mungu ambaye
ni upendo. Ni mwaliko na changamoto ya kukazia malezi ya awali na endelevu kwa waamini
walei, ili watambue dhamana na utume wao ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.