2012-10-18 10:12:32

Mawazo makuu yaliyojitokeza kutoka kwa Mababa wa Sinodi ya Uinjilishaji Mpya yanayofanyiwa kazi kwa sasa!


Kardinali Donald Wuer, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Washington, mwezeshaji wa jumla katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya anabainisha kwamba, changamoto kubwa iliyotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa ufunguzi wa maadhimisho haya ni waamini kutambua wito na mwaliko wa kuchuchumilia utakatifu na waamini watambue kwamba, ni wadau wakuu katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya.

Huu ndiyo mfano ulioneshwa na Waalimu wa Kanisa waliotangazwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Kardinali Wuer anajaribu kuchambua kwa kina na mapana, mada msingi zilizojitokeza kutokana na mchango wa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya, tayari kwa maandalizi ya Hati mbali mbali mara baada ya maadhimisho ya Sinodi. Uinjilishaji Mpya una mwelekeo unaopania kulipatia Kanisa fursa ya kuangalia maisha na utume wake kwa siku za usoni, kama sehemu ya mchakato wa kuleta uamsho mpya wa imani miongoni mwa Wakristo, kwa kutangaza habari Njema ya Wokovu kama utume wa kwanza wa Kanisa.

Kanisa linaangalia mbinu na mikakati itakayoliwezesha kutangaza kwa umakini na ufanisi mkubwa Neno la Mungu katika ulimwengu mamboleo; katika mazingira ya utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; pamoja na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza siku kwa siku, hasa ukanimungu wa kukithiri miongoni mwa watu wa Ulaya. Mama Kanisa anaalikwa kuwa na ari mpya ya utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu inayojionesha katika uhalisia wa maisha.

Ili kufanikisha azma ya Uinjilishaji Mpya, kuna haja anasema Kardinali Wuer: Kudumisha majadialiano ya kiekukemene na kidini, hasa miongoni mwa waamini wa dini ya Kiislam ili kujenga misingi ya haki, amani na utulivu; dhidi ya vurugu na ukiukwaji wa uhuru wa kuabudu. Kanisa linapaswa kuviinjilisha vyombo vya mawasiliano ya kijamii, kwani vinahitaji kupata lugha na sanaa mpya ya mawasiliano kutoka ndani ya Kanisa: kuna haja ya kukazia kwa namna ya pekee, utamadunisho katika ngazi mbali mbali za maisha na vipaumbele vya waamini, sanjari na kuendeleza majadiliano na wasioamini.

Kanisa linapaswa kupaaza sauti yake ya kinabii kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za kijamii; kwa kutangaza Injili ya upendo hasa kwa maskini, wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Vyombo vinavyoweza kutumiwa na Mama Kanisa katika azma ya Uinjilishaji Mpya kwanza kabisa ni: Parokia, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu; maeneo ya hija; Makatekista ambao pengine umefika wakati kwa Kanisa kuwapatia utume maalum ndani ya Kanisa. Wanandoa na Familia ni kundi linalohitaji maandalizi makini ili kuweza kutekeleza wajibu na dhamana ya Uinjilishaji mpya na kama sehemu ya harakati za kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa imani thabiti.

Wanawake wanaangaliwa kwa jicho pa lekee sana na Mama Kanisa katika maisha ya Kanisa na dhamana ya kurithisha Imani, bila kusahau mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na Mapadre pamoja na Watawa. Wote hawa wanayo fursa nyeti ya kuchangia katika majiundo yatakayowawezesha watu kulifahamu Fumbo la Maisha ya Kristo, bila kulegeza kamba katika maisha ya usafi wa moyo na useja.

Mababa wa Sinodi anasema Kardinali Wuer kwamba, wanaendelea kukazia umuhimu wa waamini walei kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kuanzia katika ngazi mbali mbali, kwa kutambua kwamba, waamini walei wanayodhamana nyeti ya kutangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, kama jitihada za kuyatakatifuza malimwengu. Wahamiaji na wageni ni changamoto chanya inayoweza kutumiwa na Mama Kanisa katika Uinjilishaji Mpya. Ili kufanikisha wazo hili, Kanisa halina budi kujikita katika huduma kwa wahamiaji na wakimbizi sanjari na kuwashirikisha katika maisha ya Kanisa mahalia, kwani ndani ya Kanisa hakuna mgeni!

Kardinali Donald Wuer anawaachia Mababa wa Sinodi maswali kumi na nane wanayopaswa kuyatafakari kwa kina, ili hatimaye, waweze kutoa majibu muafaka: Wajibu wa kimissionari walioa nao waamini walei ndani ya Kanisa; umuhimu wa Parokia katika utoaji wa Katekesi ya kina na majiundo endelevu. Mababa wa Sinodi wanapaswa kubainisha mambo yanayoweza kuleta chachu mpya katika maisha na utume wa Kanisa. Je, Kanisa linapaswa kufanya kitu gani ili kuwawezesha vijana kufahamu undani wa Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake? Changamoto zipi zinazolikabili Kanisa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kardinali Wuer anawauliza Mababa wa Sinodi kwamba, ili kupata utajiri wa maisha ya kiroho, wongofu wa ndani na majiundo ya imani, Kanisa linapaswa kufanya nini? Haya ni baadhi ya maswali yanayogusa kwa namna ya pekee: umuhimu wa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki; Wainjilishaji na dhamana yao ndani ya Kanisa, ili mikakati na mipango ya Mama Kanisa katika Uinjilishaji Mpya iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Mchakato huu unahitaji muda muafaka, nia thabiti na utekelezaji wake unaojikita katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa, ili kutangaza kwa ari na nguvu mpya Habari Njema ya Wokovu, inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, kwa njia ya furaha.Bikira Maria, nyota ya Uinjilishaji Mpya awe ni mfano na kielelezo cha kuigwa na Wamissionari wote wanaojitosa kimasomaso katika utangazaji wa Injili, ili iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.