Dhamana ya Wakristo katika mchakato mzima wa Uinjilishaji Mpya katika ulimwengu mamboleo!
Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji Mpya wanaendelea kuwahimiza Wakristo
kutoogopa kamwe kutokana na vitisho na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza
katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya kwani, Kanisa lina mtandao mpana unaojikita katika:
Majimbo, Parokia na Vigango. Fursa zote hizi zinaweza kutumiwa na Mama Kanisa ili
kufanikisha dhamana ya Uinjilishaji Mpya unaofanyiwa kazi kwa sasa.
Jambo
la msingi ni kuhakikisha kwamba, Wakristo wanahamasishwa kujitoa bila ya kujibakiza,
wakisukumwa na ari, moyo na ukarimu wa Kiinjili, kushiriki katika mikakati ya kichungaji
kwa ajili ya maisha na Utume wa Kanisa. Majukumu haya yanaweza kutekelezwa kwa njia
za kawaida, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, majiundo
makini ya wanafunzi shuleni na vyuoni, njia za mawasiliano ya jamii; uwanja wa sanaa,
utamaduni na michezo pamoja na kusimama kidete na wafanyakazi na wakulima, ili kukabiliana
na changamoto zao kwa moyo wa Kiinjili.
Vyama vya kitume vinapaswa kuwezeshwa,
ili kutekeleza wajibu wao, kwa kutambua kwamba, vinashiriki pia katika Unabii wa Kanisa.
Waamini wanapaswa kujitambulisha kwa njia ya utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu;
ushuhuda kwa njia ya Injili ya Upendo; ushiriki mkamilifu katika maadhimisho mbali
mbali ya liturjia ya Kanisa; ili matukio yote haya yawawezeshe waamini kuweza kukutana
na Yesu anayefanya hija katika maisha yao ya kiimani.
Mababa wa Sinodi wanasema,
ukanimungu, mawazo mepesi mepesi na uhuru usiokuwa na mipaka ni mambo yenye madhara
makubwa katika: imani, maisha adili, mahusiano katika familia na jamii katika ujumla
wake na matokeo yake ni watu kugubikwa na ubinafsi. Lakini ikumbukwe kuwa, wanadamu
wanategemeana na hakuna mtu anayeweza kujigamba kwamba, anajitosheleza, lakini zaidi,
mwanadamu anamtegemea na kumhitaji Mungu katika maisha yake.
Kumbe waamini
washirikishwe kwa ukamilifu katika kubuni, kupanga, kutekeleza na kutathimini mikakati
mbali mbali inayopania kukoleza ari na moyo wa Uinjilishaji Mpya miongoni mwa Jamii.
Lengo ni kuwajengea waamini uwezo wa kujisomea, kulitafakari na kuliishi Neno la Mungu
katika uhalisia wa maisha yao na kwamba, Wakristo wanapaswa kuona fahari ya kushirikishana
utajiri unaofumbatwa katika Neno la Mungu.
Mababa wa Sinodi kwa namna ya pekee,
wanawashukuru na kuwapongeza wanawake wanaojitoa bila ya kujibakiza katika maisha
na utume wa Makanisa mahalia, katika malezi na makuzi ya watoto na vijana; katika
huduma kwa wagonjwa, wazee na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni jukumu la
Kanisa kuwawezesha wanawake ili waweze kuchangia zaidi katika maisha, utume na ustawi
wa Kanisa katika ujumla wake.
Waamini wanapaswa kufundishwa namna ya kusali
ili waweze kusali vyema wakiwa na amani na utulivu wa ndani; daima wakitamani kuyafahamu
mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Watambue dhana na uwepo wa dhambi inayoharibu
uhusiano kati yao na Mungu pamoja na jirani zao. Wajitahidi kukimbilia huruma na upendo
wa Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, ili hatimaye, waweze kupata maisha mapya.
Waamini wawezeshwe kikamilifu, ili washiriki katika azma ya Uinjilishaji, kwani hawa
ni nguvu kazi ambayo ikitumiwa barabara inaweza kulisaidia Kanisa katika mchakato
wa kuyatakatifuza malimwengu.
Vijana ni kundi jingine linalopaswa kuwekewa
mikakati makini ya Uinjilishaji Mpya, ili katika harakati zao za kutafuta ukweli na
maana ya maisha, waweze kukutana na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Ni jukumu la Kanisa
kuwasaidia vijana hawa kutambua maana ya maisha kwa kujichotea utajiri unaofumbatwa
katika Kweli za Kiinjili.
Vijana watambue wazi kwamba, wanachangamotishwa
na Mama Kanisa kuwainjilisha vijana wenzao wanapokutana katika "vijiwe" vyao. Vyama
vya utume kwa vijana viendelee kupewa msukumo wa pekee, ili hatimaye, kwa pamoja waweze
kujenga Jumuiya ya Waamini wanaoshiriki kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Uinjilishaji
Mpya upanie kukoleza majadiliano na wasiomwamini Kristo, ili katika hija ya maisha
yao, waonje na kuguswa na uwepo wa Mungu aliyewaumba, anayewapenda na kuwathamini
na anataka kuwakomboa kwa njia ya Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo. Wasioamini waguswe
na mifano na ushuhuda wa mitume, watakatifu na waamini ambao wamekuwa mstari wa mbele
kumwilisha Injili ya Kristo katika uhalisia wa maisha yao.
Miaka hamsini imekwisha
gota, tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipoonesha dira na mwongozo
wa kufuata katika harakati za kukoleza ari na moyo wa majadiliano ya kiekumene miongoni
mwa Wakristo. Vikwazo vingi vimeweza kuvukwa hadi wakati huu, changamoto kwa Wakristo
wote katika umoja wao kushuhudia kweli za Kiiinjili kwa njia ya huduma ya upendo.
Kanisa linatambua kwamba, lipo kwa ajili ya Kuinjilisha.
Jukumu hili linapaswa
kupata pia chapa ya Kiekumene kwa kukazia utakatifu wa maisha, ili kwa pamoja waweze
kuungama Imani inayojikita katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Biblia Takatifu na Mapokeo.
Matunda ya Uinjilishaji Mpya ni neema ya Mungu inayojionesha miongoni mwa waamini
wenye dhamana ya Kuinjilisha. Ni lazima liwe ni Kanisa linalochota utajiri wake kutoka
katika Heri za Mlimani, ambazo kimsingi ni muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Yesu.
Waamini waundwe kikamilifu ili hatimaye, waweze kufikia ukomavu katika Ibada, maisha
ya kijumuiya na utume wao ulimwenguni.
Jumuiya za Kikristo zijibidishe kuhakikisha
kwamba, Injili ya Kristo inamgusa mwanadamu: kiroho na kimwili; na kwamba, utangazaji
wa Habari Njema, ufanyike kwa njia ya Liturjia ya Kanisa na Huduma ya Upendo. Maadhimisho
ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, yawe ni kiini na hitimisho la maisha na utume wa Kanisa.
Waamini wajichotee nguvu na neema kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Liturjia
ina umuhimu wa pekee, katika mchakato mzima wa Uinjilishaji Mpya.