2012-10-17 08:32:19

Ujumbe wa Mababa wa Sinodi ya Uinjilishaji Mpya kwenda Syria ili kuonesha mshikamano wa Kanisa kwa wananchi wa Syria katika kipindi hiki kigumu!


Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican akichangia mada kwenye maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji Mpya anasema, Kanisa haliwezi kuendelea kukaa kimya wakati ambapo kuna maafa makubwa yanayoendelea kujitokeza nchini Syria. Tayari idadi kubwa ya Mababa wa Sinodi wamekwisha lizungumzia tatizo hili.

Kardinali Bertone anasema kwamba, suluhu ya mgogoro wa kisiasa na kijamii unaoendelea nchini Syria, hauwezi kupatikana tu kwa njia za kisiasa peke yake, ikizingatiwa idadi kubwa ya wananchi wanaoendelea kuteseka na vita hii, wale wanaokimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao, sanjari na kuangalia kwa umakini mkubwa mustakabali wa Syria kwa siku za usoni.

Kutokana na changamoto hizi zote, kwa ridhaa ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameamua kwamba, ujumbe kutoka Mababa wa Sinodi ya Uinjilishaji Mpya kwa siku za karibuni kwenda nchini Syria, ili kujionea wenyewe hali halisi na kama njia ya kuwaonjesha mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita na Kanisa zima, katika kipindi hiki kigumu cha mahangaiko yao kutokana na mgogoro wa kisiasa na kijamii nchini Syria.

Ujumbe wa Vatican unalenga kuunga mkono juhudi za kitaifa, kimataifa na kwa wadau mbali mbali wanaoendelea kujibidisha ili muafaka, haki, amani na utulivu viweze kutawala tena nchini Syria.







All the contents on this site are copyrighted ©.