2012-10-17 08:18:48

Kanisa Katoliki litaendelea kuenzi shughuli za vyama vya ushirika na kilimo kama kielelezo cha umoja na mshikamano katika maboresho ya maisha ya watu!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 16 Oktoba, amemtumia ujumbe Bwana Jose Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, akisisitizia kwamba, Kanisa Katoliki litaendelea kuunga mkono juhudi zinazopania kuimarisha ushirika katika sekta ya kilimo.

Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Chakula Duniani, wakati ambapo watu wengi wanaendelea kuonja makali ya myumbo wa uchumi kimataifa kiasi cha kutishia upatikanaji wa mahitaji msingi, ikiwepo haki ya mtu kuwa na uhakika wa kupata chakula na lishe bora. Hali inazidi kuwa mbaya zaidi hasa katika Nchi ambazo zinaendelea duniani.

Hali hii inafanana kabisa na mazingira yaliyopelekea kuanzishwa kwa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa pamoja ili kuondkana na baa la njaa duniani, kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo sanjari na maboresho ya Jamii zinazoishi vijijini.

Lishe duni duniani ni jambo linaloendelezwa kwa vile bado hakuna mikakati makini ya kuinua sekta ya kilimo pamoja na ushindani usiokuwa na tija; mambo ambayo yanaweza kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kusahau kwamba, kwa pamoja wanaweza kupata suluhu ya changamoto hizi kwa kukidhi mahitaji ya mtu mmoja mmoja na Jamii kwa ujumla wake.

Baba Mtakatifu anaunga mkono juhudi zinazoendelea kufanywa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na kwa namna ya pekee, kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2012, yaani Vyama vya Ushirika na Kilimo ni nyenzo msingi katika kuilisha dunia.

Hii ni changamoto ya kuendelea kuvisaidia vyama vya ushirika na kilimo katika maboresho ya sekta ya uchumi kimataifa. Uzoefu unaonesha kwamba, vyama hivi vinamchango mkubwa katika uzalishaji pamoja na kushiriki katika utoaji wa maamuzi, kielelezo makini katika kufikia maendeleo endelevu ya binadamu.

Kanisa Katoliki anasema Baba Mtakatifu lina thamini na kuenzi vyama vya ushirika kama njia inayoonesha umoja na mshikamano, hali inayoweza pia kusaidia kuchangia utatuzi wa migogoro ya kijamii. Ni kutokana na mantiki hii, Kanisa katika Mafundisho yake Jamii, limeendelea kuunga mkono juhudi za vyama vya ushirika kwa kutambua kwamba, hizi si juhudi tu za masuala ya kiuchumi, lakini pia zinachangia ukuaji wa mtu, jamii, tamaduni na maadili kwa wadau na wahusika wa vyama hivi.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, pale ambapo kuna migogoro na kinzani za kijamii au majanga asilia, kiasi cha kuathiri shughuli za kilimo, mkazo wa pekee hauna budi kuwekwa kwa wanawake ambao wamekuwa ni mhimili mkuu katika kuziwezesha familia zao sanjari na kuhifadhi urithi wa maarifa na teknolojia inayopatikana huko vijijini.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anahitimisha ujumbe wake kwa Mkurugenzi mkuu wa FAO, akisema kwamba, uongozi wa kitaifa na kimataifa hauna budi kutoa sheria, miongozo na fedha ili kuhakikisha kwamba, vyama vya ushirika vijijini vinakuwa ni nyenzo muhimu katika uzalishaji kwenye sekta ya kilimo, usalama wa chakula, mabadiliko ya kijamii na maboresho ya maisha ya watu wengi zaidi vijijini.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, vijana wanaweza kuanza tena kujenga matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi, kwa kuendelea kushiriki katika shughuli za kilimo pamoja na kuenzi tunu msingi za mapokeo huko vijijini.







All the contents on this site are copyrighted ©.