Waamini walei wanalo jukumu la kuyatakatifuza malimwengu kwa moyo na tunu msingi za
Kiinjili
Askofu Beatus Kinyaiya mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika maadhimisho
ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji mpya, amekazia juu ya dhamana ya waamini
walei katika azma ya Uinjilishaji. Mama Kanisa ana rasilimali kubwa ya watu ambayo
ni waamini walei, inayoweza kutumika katika mchakato wa Uinjilishaji. Waamini hawa
kwa njia ya nguvu na imani yao wanaweza kutoa msukumo mpya katika maisha ya Kikanisa.
Askofu
Kinyaiya anasema, Barani Afrika kuna kampeni ya chini chini inayopania kuhakikisha
kwamba, Kanisa na Viongozi wake hawajishughulishi kabisa na maisha ya Kijamii, kwa
maneno mengine, viongozi wa Kanisa wanapaswa kuhubiri Makanisani na kamwe wasijishughulishe
na masuala ya kijamii.
Kuna mikakati na sera zinazotolewa na baadhi ya Nchi
Barani Afrika, zinazotaka kulinyima Kanisa fursa za kushiriki na kuchangia kikamilifu
katika sekta ya elimu, afya, huduma za kijamii, vyombo vya mawasiliano ya jamii pamoja
na kutaka kuzima sauti ya kinabii inayokazia umuhimu wa maadili na utu wema mintarafu
tunu msingi za Kiinjili.
Katika mazingira kama haya anasema Askofu Beatus
Kinyaiya wa Jimbo Katoliki la Mbulu, Tanzania kwamba, wito na dhamana ya waamini walei
ni kuyatakatifuza malimwengu kwa kujikita zaidi na zaidi katika wito na dhamana waliyojitwalia
wakati walipopokea Ubatizo. Ni jukumu lao kuhakikisha kwamba, maadili, mafao ya wengi,
haki na amani vinadumishwa katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kitamaduni, kisayansi,
kisanaa na katika vyombo vya mawasiliano ya jamii.
Waamini walei wanadhamana
ya Kuinjilisha: upendo wa kibinadamu, maisha ya kifamilia, kwa kujikita katika malezi
na majiundo ya watoto na vijana; kwa kushirikisha taaluma na ujuzi wao kwa ajili ya
mafao ya wengi sanjari na kuwahudumia wagonjwa na wote wanaoteseka; yote haya yafanyike
kwa lengo la kujenga na kudumisha Ufalme wa Mungu hapa duniani.
Viongozi wa
Kanisa kwa upande wao, wanayo dhamana na jukumu la kuhakikisha kwamba, waamini walei
wananolewa barabara, kwa kujenga na kuimarisha vituo na taasisi za majiundo ya walei
bila kusahau kutumia pia taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa.
Ni changamoto kwa Mabaraza ya Maaskofu na Majimbo mbali mbali kuanzisha mchakato
wa kuadhimisha Sinodi katika maeneo yao, ili kuwashirikisha waamini katika hatua mbali
mbali za maisha na utume wa Kanisa. Waamini walei wanapaswa kusaidiwa katika maisha
yao ya kiroho kwa njia ya mafungo na semina mbali mbali bila kusahau kuwajengea moyo
na ari ya kimissionari ndani mwao.
Askofu Beatus Kinyaiya anakamilisha mchango
wake katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji mpya kwa kusema
kwamba, Yesu Kristo ndiye Mkulima wa kweli, anayewaita wanadamu kushiriki katika kazi
ndani ya shamba lake, ili liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Ni wajibu wa waamini
walei kuyatakatifuza malimwengu, changamoto inayoweza kujionesha kwa namna ya pekee
katika: mila, sheria na miundo ya jamii wanamoishi. Ni jukumu la waamini walei kuyatakatifuza
malimwengu kwa moyo na tunu msingi za Kiinjili.