Taalimungu inayofundishwa na kumwilishwa, iwe ni sayansi ya imani inayomsaidia mwanadamu
kufahamu kweli za Kiimani
Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya ni kati ya Mababa wa
Sinodi waliochangia mada wakati wa maadhimisho ya kikao cha kumi na moja cha Sinodi
juu ya Uinjilishaji mpya inayoendelea hapa mjini Vatican. Anabainisha kwamba, kuna
ukakasi miongoni mwa watu kutaka kufahamu masuala ya dini na hasa "dini ya kweli",
kwani inaonekana kwamba, watu wanatafuta kwa namna ya pekee, kufahamu mang'amuzi ya
kidini na mifumo mbali mbali ya maisha ya kidini inayoridhisha njia zao za ufahamu.
Kardinali
Njue anasikitika kusema kwamba, inashangaza kuona kwamba, kuna umati mkubwa hata miongoni
mwa waamini wasiomfahamu Mwenyezi Mungu na hiki ndicho kielelezo cha myumbo wa imani
unaojionesha sehemu mbali mbali za dunia. Umefika wakati kwa Mama Kanisa kufungua
malango yake ili kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu,
kwa njia ya ushuhuda makini wa wafuasi wake, unaojionesha katika nia na majitoleo
ya imani. Wakristo wanayo dhamana ya kuihabarisha Jamii kwa njia ya Mafundisho ya
Kristo na Kweli za Kiinjili.
Taalimungu inayofundishwa na kumwilishwa na Mama
Kanisa, iwe ni sayansi ya imani inayosaidia akili ya mwanadamu kufahamu kweli za kiimani.
Akili na Imani ni chanda na pete, vinaopaswa kusaidiana ili kumsaidia mwamini katika
maisha yake ya kiroho. Wanataalimungu wanaoishi katika Mapambazuko ya Millenia ya
Tatu ya Ukristo wanapaswa kuonesha utakatifu wa maisha na wala si tu kama majaalimu
waliobobea katika taaluma ya kufundisha ukweli. Wawe ni watu waliomwongokea Kristo
na watakaowasaidia waamini kumwilisha imani yao kwa njia ya upendo.
Kardinali
John Njue ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi anasema kwamba, Kanuni
ya imani inapaswa kuwa ni "chakula cha kila siku" kwa ajili ya waamini; kwani huu
ni muhtsari wa imani ya Kanisa inayopaswa kufahamika na kumwilishwa. Waamini wanapaswa
kukabiliana na changamoto za kiimani kwa njia ya ukweli na ujasiri pasi ya kukata
tamaa, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kuhakikisha kwamba, imani hii inashughulikiwa
kikamilifu.
Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaitolea ushuhuda
makini imani yao, kwa njia ya neema iliyomiminwa ndani mwao, inayowawezesha kumwongokea
Kristo kutoka katika undani wa mioyo yao. Hii ni hija ndefu inayopaswa kuendelezwa
na wafuasi wa Kristo katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Waamini wanapaswa
kukua na kukomaa katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.