2012-10-16 08:25:52

Jitajirishe na mchango wa Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji mpya kama njia ya kurithisha imani ya Kikristo!


Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji mpya wanaendelea kuadhimisha Sinodi hii inayoongozwa na kauli mbiu Uinjilishaji mpya ni kutangaza imani ya Kikristo. Kwa namna ya pekee, Mababa wa Sinodi wameguswa na ushuhuda wa imani iliyooneshwa na wafiadini ndani ya Kanisa kwa nyakati mbali mbali. Hawa ni watu walioguswa kwa namna ya pekee na upendo wa Yesu na Mafundisho yake, hata wakawa tayari kuyamimina maisha yao.

Hata leo hii, kuna Wakristo bado wanaendelea kudhulumiwa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Mababa wa Sinodi wanasema, waamini hawa wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kutokana na ushuhuda wa imani yao, kwani kimsingi imani ni jambo la hadhara na wala si kitu cha kuficha, bali inapaswa kutolewa ushuhuda wenye kuleta mvuto na mguso katika maisha ya watu.

Wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum ni kundi linaloteseka na kuonja hadha ya maisha. Ni watu wanaotafuta maana ya maisha yao hapa ulimwenguni. Mababa wa Sinodi wanasema, hili ni kundi ambalo ni chemchemi mpya ya Uinjilishaji unaopaswa kufanywa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Wahamiaji na wakimbizi hawa, wakishainjilishwa nao pia wanageuka na kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji kwa wale wanaowazunguka. Ili kufanikisha azma hii, haki zao msingi hazina budi kuheshimiwa na kuthaminiwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Kanisa linapaswa kutambua kwamba, Injili ya Upendo ni ushuhuda makini kabisa wa Uinjilishaji. Waamini wajikite zaidi na zaidi katika kumwilisha Injili ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili wao pia waonje huruma na upendo wa Kristo unaojionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya Kanisa. Uinjilishaji mpya uwe ni mwendelezo unaopania kuonesha uwepo wa Kristo kati ya wafuasi wake.

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, linalopaswa kuwa kweli ni shule ya utakatifu, haki na amani; hii ni chemchemi ya Uinjilishaji mpya. Pale ambapo mikakati ya kichungaji imeshindwa kutekelezwa ni kwa vile Kanisa limeshindwa kujitambua kuwa ni Familia ya Mungu inayowajibika na badala yake dhana ya Kanisa kama Taasisi imekuzwa na kupewa kipaumbele cha kwanza, kiasi hata cha kusahau changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Mababa wa Sinodi wanasema, Kanisa kamwe halitaweza kukaa kimya na kufumbia macho mmong'onyoko wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, unaofanywa kwa makusudi mazima na baadhi ya wanasiasa, ambao sera na mikakati yao inalenga kubomoa misingi bora ya kifamilia. Hii ni changamoto kubwa kwa Mama Kanisa hasa katika nchi za Ulaya zinazokabiliwa na ukanimungu wa kutisha. Kanisa linaposimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za kifamilia mintarafu Mafundisho ya Kristo na utu wema, wanandoa wanajikuta wakiwa na dhamana ya kukuza na kudumisha uaminifu wao kama kielelezo makini cha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Mababa wa Sinodi wanasema, Parokia zinapaswa kutekeleza wajibu wake katika maisha na utume wa Kanisa kwa kukuza na kuendeleza Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, shule ya majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali. Majadiliano haya yanapaswa kuwa ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya, changamoto iliyotolewa kwa mara ya kwanza na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, takribani miaka hamsini iliyopita.

Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na utamaduni wa kusikilizana, kuheshimiana, kuthaminiana na kushirikishana mang'amuzi na tunu msingi za maisha ya kidini, daima mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza. Mababa wa Sinodi wanakiri kabisa kwamba, vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kiimani na tabia ya baadhi ya watu kutozingatia na kuheshimu sheria ni mambo yanayokwamisha jitihada za Mama Kanisa katika mchakato mzima wa majadiliano ya kidini sehemu mbali mbali za dunia. Lakini matukio yote haya yasiwakatishe moyo waamini kujikita katika majadiliano ya kidini.

Tema nyingine iliyojitokeza ni umuhimu wa utamadunisho kama njia ya Uinjilishaji mpya, ili Injili iweze kuota mizizi na kushika hatamu katika maisha na vipaumbele vya waamini, wakiwa tayari kuitolea ushuhuda imani yao kwa Kristo na wakiendelea kubaki na utambulisho wao wa mahali wanapotoka.

Kashfa ya utengano kati wafuasi wa Kristo ni mada ambayo pengine haijapewa msukumo wa pekee, lakini Mama Kanisa anachangamo kuhakikisha kwamba, anawajengea waamini wake moyo na ari ya kutaka kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene miongoni mwa wafuasi wa Kristo, ili siku moja kadiri ya mapenzi ya Mungu, umoja huu uweze kuonekana kama kielelezo makini cha imani ya Kanisa.

Juhudi hizi ziyahusishe Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo, ili wote wawe ni wamoja kama Kristo anavyotaka Kanisa lake liwe. Lengo ni Wakristo katika umoja wao, kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Umoja na mshikamano wa Kikristo unapaswa pia kujionesha kwa namna ya pekee, wanaposhiriki katika "kuumega mkate", wanaposoma na kulitafakari kwa pamoja Neno la Mungu, tayari kulitolea ushuhuda katika uhalisia wa maisha yao.

Uinjilishaji mpya unajikita wanasema Mababa wa Sinodi katika utangazaji wa Neno la Mungu kwa umakini na umahiri mkubwa, ili hatimaye, Neno hili liwe ni kichocheo cha tafakari ya kina inayolenga kuzima kiu ya uwepo wa Mungu miongoni mwa binadamu. Uinjilishaji mpya ni mchakato wa ndani ya mtu unaolenga kwa namna ya pekee kumletea wongofu wa ndani, utakatifu na hatimaye, maisha ya uzima wa milele. Imani kwa Kristo na Kanisa lake inadai utii na upendo mkamilifu.

Mababa wa Sinodi wanaona umuhimu wa kuwainjilisha vijana wanaoendelea kukumbana na changamoto mbali mbali katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ili waweze kumfahamu, kumpenda na htimaye, kujitoa bila ya kujibakiza kumtumikia Kristo katika maisha ya Kipadre na Kitawa. Uinjilishaji mpya kwa vijana unapaswa kwenda sanjari na jitihada za Mama Kanisa katika maboresho ya sekta ya elimu na umakini katika majiundo ya vijana, ili waweze kutambua wajibu na dhamana yao ndani ya Kanisa, tayari kuitolea ushuhuda imani hii katika mazingira na changamoto za maisha yao ya ujana.

Utume wa Kanisa miongoni mwa vijana ni jambo linalopaswa kupewa msukumo wa pekee kwa kuhakikisha kwamba, wahudumu wakuu wanaandaliwa kwa umakini mkubwa, ili kuwamegea vijana hawa tunu msingi za maisha ya Kikristo na kweli za Kiinjili, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na mafundisho yao.

Uinjilishaji mpya ujenge mahusiano mema na ya dhati miongoni mwa watu wa Mataifa. Uhusiano huu kwanza kabisa ujioneshe katika maisha ya Kifamilia, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, Vyama vya Kitume na Jamii katika ujumla wake. Kila mtu aguswe kwa namna ya pekee na uwepo wa jirani yake. Mshikamano huu wa upendo ujioneshe hasa kwa wagonjwa, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Watu washikamane kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto za hali ngumu ya maisha na mmong'onyoko wa maadili na utu wema. Hakuna muujiza unaoweza kufanywa wa kupata mali au kumaliza matatizo bila ya kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa.

Waamini watambue kwamba, Mwenyezi Mungu anaendelea kutenda miujiza ya uponyaji kwa kushirikiana na madaktari na kamwe wasipuuze huduma za afya wakitarajia miujiza katika maisha yao, matokeo yake, watajikuta wakitangatanga katika madhehebu na dini mbali mbali, kielelezo cha myumbo wa imani.

Mababa wa Sinodi wanatambua na kuheshimu mchango wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Wanaalikwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa utakatifu wao binafsi, maadili na utu wema, bila kusahau mchango na ushiriki wao katika Jumuiya ndogo ndogo za kikristo. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yatoe changamoto ya pekee kwa wanaume na vijana kushiriki kikamilifu katika utume wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo kama chemchemi ya Uinjilishaji mpya. Ile ni shule ya Neno la Mungu na umwilishaji wa Injili ya upendo.







All the contents on this site are copyrighted ©.