2012-10-15 11:20:45

Tumieni utajiri wenu kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano ili mjipatie utimilifu wa maisha na uzima wa milele!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican alitafakari kuhusu dhana ya utajiri mintarafu Ibada ya Neno la Mungu, Jumapili ya ishirini na nane ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa.

Anasema, ni vigumu kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu, lakini si jambo ambalo haliwezekani kabisa, ikiwa kama utajiri na mali hii itatumika kujenga na kuimarisha mshikamano na Injili ya upendo. Kwa njia hii, waamini na watu wenye mapenzi mema, watakuwa wanatembea katika njia ya maisha wakijitahidi kumfuasa Kristo ambaye licha ya kuwa tajiri, lakini alijinyenyekesha na kuwa maskini, ili kutokana na umaskini wake, wengi waweze kuwa ni matajiri.

Baba Mtakatifu anasema, Injili inamwonesha Kijana aliyekuwa na utajiri mkubwa, alikuwa ni Mchamungu na alijitahidi kumwilisha Amri za Mungu katika maisha yake, lakini kwa bahati mbaya alikuwa hajaonja maishani mwake furaha ya kweli, ndiyo maana anajitaabisha kumtafuta Yesu ili aweze kuzima kiu yake ya kupata furaha ya kweli na utimilifu wa maisha.

Yesu kwa jicho la Kimungu anamwangalia na kumpenda, lakini anatambua udhaifu wa kijana huyu kuwa ni kung'ang'ania mno mali, ndiyo maana anamchangamotisha kutoa mali yake yote kwa ajili ya maskini, kisha amfuate! Wazo hili hlikupokelewa kwa mikono miwili na badala yake, likajenga majonzi moyoni mwa kijana yule, kwani alishindwa kujinasua kutoka kwenye mali aliyokuwa anaimiliki, ambayo ilikuwa ni kikwazo kikubwa cha furaha na maisha ya uzima wa milele.

Ndiyo maana Yesu anawakumbusha Wafuasi wake, jinsi ambavyo ni vigumu kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu, maneno ambayo yaliwaaacha Mitume wakiwa wameshika tama! Anakazia kwamba, kile ambacho ni vigumu kwa binadamu, lakini kinawezekana mbele ya Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto kwa watu wenye utajiri kuhakikisha kwamba, wanatumia utajiri wao kwa ajili ya kujipata maisha ya uzima wa milele.

Ndani ya Kanisa kuna mifano mingi ya watu waliotumia utajiri wa mali yao mintarafu kweli za Kiinjili, kiasi hata cha kufikia utakatifu wa maisha. Hawa ndio akina Francisco wa Assis, Mtakatifu Elizabeth wa Hungaria na Mtakatifu Charles Borromoe, kwa kutaja wachache!

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Bikira Maria, Kikao cha Hekima aweze kuwasaidia kupokea mwaliko wa Kristo kwa moyo wa furaha, ili waweze kupata utimilifu wa maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.