2012-10-15 10:25:53

Matukio mbali mbali ya Kanisa yakoleze ari na moyo wa maadhimisho ya Mwaka wa Imani


Askofu mkuu Protas Rugambwa, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa, Jumapili iliyopita, tarehe 14 Oktoba 2012, wakati wa maadhimisho ya Kumbu kumbu ya miaka kumi na tatu tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, muasisi wa Tanzania alipofariki dunia, ametumia fursa hii kuwaalika Wakristo kuhakikisha kwamba, wanatumia kikamilifu matukio mbali mbali yanayoendelea ndani ya Kanisa kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, hivi karibuni.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji mpya kama nyenzo makini ya utangazaji wa Injili, Maadhimisho ya Jubilee ya miaka hamsini tangu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulipozinduliwa, Kumbu kumbu kumbu ya miaka ishirini tangu kuchapishwa kwa mara ya kwanza kwa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki pamoja na Maadhimisho ya Siku ya Kimissionari Kimataifa; yawe ni chachu ya maadhimisho ya kina ya Mwaka wa Imani.

Katika Ibada ya Misa iliyoandaliwa na Jumuiya ya Wanafunzi Wakatoliki Wanaosoma Roma pamoja na Watanzania kwa ujumla wao, ilihudhuriwa pia na Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Askofu mkuu Josephat L. Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara pamoja na idadi kubwa ya Mapadre, Watawa, Waamini na Marafiki wa Tanzania. Watanzania kwa ujumla wao, waliongozwa na Dr. James A. Msekela, Balozi wa Tanzania nchini Italia.

Yafuatayo ni Mahubiri ya Askofu mkuu Protas Rugambwa wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka kumi na tatu tangu alipofariki dunia Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius K. Nyerere, aliyoyatoa kwenye Kanisa la Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Petro, mjini Roma. RealAudioMP3







All the contents on this site are copyrighted ©.