2012-10-13 10:56:46

Yaliyojiri katika maadhimisho ya Sinodi ya Uinjilishaji mpya inayoendelea hapa mjini Vatican


Viongozi wawakilishi kutoka katika Mashirikisho ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, sehemu mbali mbali za dunia, wamepata fursa ya kuweza kutoa mchango wao kuhusu hali ya maisha na utume wa Kanisa kutoka katika maeneo yao.

Kardinali Peter Erdò, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, amekazia umuhimu wa Bara la Ulaya, kutambua na kuenzi utambulisho wao unaopata chimbuko lake katika Ukristo. Hii ndiyo changamoto endelevu iliyojitokeza mara tu baada ya maadhimisho ya Jubilee kuu ya Ukristo, iliyofanyika kunako mwaka 2000. Licha ya matukio mbali mbali ya kiimani ambayo yameendelea kuadhimishwa na Mama Kanisa, lakini Bara la Ulaya linaendelea kuonesha ukakasi katika maisha ya kiimani ya Kikristo.

Hii ni propanda inayoendeshwa na vyombo vya mawasiliano ya kijamii. Mafundisho ya dini shuleni hayana mkazo wa pekee. Huu ni utafiti uliofanywa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya kwa kusema kwamba, hizi ni dalili za kuporomoka kwa misingi ya imani, miongoni mwa wananchi wa Ulaya.

Nchi nyingi zinaendelea kukazia umuhimu wa haki msingi za binadamu, lakini zenye mwono tenge kuhusu maisha ya mwanadamu na utu wake. Kumeibuka ndoto ya kudhani kwamba, kwa nguvu ya mawasiliano ya jamii na kiuchumi, hata wakati mwingine kwa kubeza maadili; watu wanaweza kuitawala dunia kama wanavyopenda. Lakini, ukweli wa mambo ni kwamba, kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa Barani Ulaya pamoja na uwepo wa idadi kubwa ya wazee wanaohitaji hifadhi za kijamii ni kati ya viashilia vikubwa kwa kuyumba kwa uchumi Barani Ulaya.

Kardinali Erdò anasema, matatizo na changamoto zote hizi zinaibua kwa namna ya pekee, kiu na njaa ya tumaini jipya, kama inavyojionesha katika maadhimisho ya Siku za Vijana Kimataifa na katika hija za kichungaji za Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa miaka ya hivi karibuni. Matukio haya yamekuwa ni chemchemi ya miito na matumaini mapya kwa waamini Barani Ulaya.

Parokia nyingi zimeanza kutambua na kuthamini utume na dhamana yao ya kushiriki katika azma ya Uinjilishaji mpya kwa kuzishirikisha pia Familia za Kikristo na Vyama vya Kitume. Uwepo wa Waamini na Wamissionari kutoka Mabara mengine umechangia kukoleza moto wa matumaini! Matendo ya huruma kwa watu wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ni utume unaoendelea kumwilisha utamaduni wa upendo. Licha ya kinzani, migogoro na vita ambavyo vimejitokeza katika maeneo kadha wa kadha Barani Ulaya. Zote hizi zimekuwa ni fursa za kujenga na kukuza moyo wa upatanisho wa kitaifa sanjari na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga Jamii inayoheshimu na kudumisha misingi ya haki, amani na upendo.

Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, kwa upande wake amekazia umuhimu wa Kanisa Barani Afrika kuwa na sura ya Kiafrika na bado likaendelea kujitambulisha kuwa ni Katoliki. Uinjilishaji mpya Barani Afrika, kwa namna ya pekee kabisa, ulipata chimbuko lake kutoka kwa Papa Paulo wa Sita, aliyewahamasisha Waafrika kuwa ni Wamissionari Barani Afrika. Changamoto kubwa kwa SECAM iliyoanzishwa kunako mwaka 1969 ni kunenga na kuendelea kuimarisha: umoja, mshikamano na ushirikiano wa dhati miongoni mwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika la Madagascar.

Kardinali Pengo anasema kwamba, Jumuiya ndogo ndogo za kikristo ni chemchemi ya Uinjilishaji wa kina Barani Afrika. Utandawazi na athari zake ni kati ya vikwazo vinavyodumaza mchakato wa Uinjilishaji wa kina Barani Afrika, madhara yanayojioneshahata katika imani ya Kikristo. Tunu msingi za maisha ya Kiafrika zinaendelea kuwekwa majaribuni, kiasi hata cha kuanza kubeza thamani ya uhai wa binadamu kwa kupenda kukumbatia utamaduni wa kifo. Kuna watu wenye misimamo mikali ya imani hali ambayo imesababisha kinzani na migogoro kati ya Waislam na Wakristo; hali ambayo kimsingi ni kikwazo cha Uinjilishaji wa kina Barani Afrika.

Kardinali Pengo anachambua historia ya Uinjilishaji Barani Afrika kwa kusema kwamba, uwepo wa Wamissionari kutoka nje ya Afrika, kulionekana kuwa ni chanzo cha kutaka kukidhi zaidi mahitaji ya malighafi kwa nchi zao asilia. Dhana kama hii pia inajitokeza kwa Wamissionari wanaotoka Afrika kwenda Kuinjilisha Ulaya, kujikuta kwamba, wanaelemewa zaidi na uchu wa kutafuta mali.

Ni ukweli usiopingika kwamba, Wamissionari waliopikwa na kuiva barabara katika nyanja mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa wamekuwa wakichukuliwa na kupelekwa kufanya kazi Ulaya na hivyo kuliacha Bara la Afrika likiendelea kuwa na uhaba wa wataalam na mabingwa katika nyanja mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Polycarp Pengo, ametumia fursa hii, kumshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa kuitisha Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika pamoja na ujumbe wake kuhusu Dhamana ya Afrika, Africae Munus. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji Mpya ni fursa nyingine kwa Mama Kanisa Barani Afrika kuamsha imani na hatimaye, kupata ufumbuzi wa matatizo, fursa na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza Barani Afrika.

Hati za Sinodi ya Maaskofu Barani Afrika, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Biblia Takatifu na Mafundisho Jamii ya Kanisa ni nyenzi muhimu katika Uinjilishaji wa kina Barani Afrika. Kardinali Polycarp Pengo ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, anabainisha kwamba, Familia ya Mungu Barani Afrika, ina matumaini makubwa katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji Mpya.

Askofu mkuu Carlos Aguiar, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Amerika ya Kusini, anasema kwamba, changamoto kubwa iliyoko mbele yao ni mpasuko wa kitamaduni na Mapokeo hai. Ili kufanikisha mchakato wa Uinjilishaji mpya, kuna haja ya Watoto wa Kanisa kujenga umoja na mshikamano wa dhati na kwamba, kuna matumaini makubwa katika mchakato mzima wa Uinjilishaji mpya unaoendelea huko Amerika ya Kusini.

Anasema, waamini walei ndio wadau wakuu wa Uinjilishaji mpya Amerika ya Kusini, kwani wanao wajibu mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Wanachangamotishwa kumwilisha ndani mwao, tunu na kweli za Kiinjili kama sehemu ya mchakato wa kuuatakatifuza malimwengu. Waamini walei wanahitaji majiundo makini mintarafu utambulisho wao wa Kikristo unaogusa maisha ya mtu binafsi, familia na kama Jumuiya ya waamini. Ni mwaliko wa kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya uhalisia wa maisha yao.

Askofu mkuu Carlos anasema, Uinjilishaji mpya unadai kwa namna ya pekee, umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, kiekukemene pamoja na ulimwengu. Jitihada hizi hazina budi kuimarishwa katika taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Mama Kanisa. Neno la Mungu, utu na heshima ya binadamu; familia, umuhimu wa zawadi ya maisha, elimu, maadili na utu wema; uchumi na maendeleo endelevu ya watu; wahamiaji, watu wasiokuwa na makazi pamoja na wakimbizi; utunzaji bora wa mazingira; haki na amani ni kati ya kweli zinazopaswa kufundishwa na Mama Kanisa kwa umakini mkubwa miongoni mwa watoto wake.

Waamini wanaalikwa kumtangaza Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao; kwa kutumia tamaduni pamoja na njia mbali mbali za mawasiliano ya jamii. Watambue mikakati ya kitaalimungu na shughuli za kichungaji, ili kumwilisha kikamilifu ujumbe wa Neno la Mungu. Ili kuvuna matunda yanayokusudiwa na Mama Kanisa, kuna haja ya kuchuchumilia: toba na wongofu wa ndani; umuhimu wa ushiriki mkamilifu na kwa njia ya uchaji Ibada na Maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa, daima kwa kuonesha umoja na mshikamano na viongozi wa Kanisa mahalia na lile la Kiulimwengu. Familia na Vyama vya Kitume vijitahidi kushiriki vyema katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wao makini.

Askofu John A Dew, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Oceania, anasema kwamba, Uinjilishaji ni utume na dhamana ya Kanisa linalopaswa kutangaza ukweli mfunuliwa, ili watu waweze kusikia, kuelewa na kuamini katika huruma na upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa namna ya pekee kwa njia ya Yesu Kristo.

Kanisa la Oceania linazidi kukua na kupanuka; miito inazidi kuongezeka na waamini wanaendelea kuonesha hamu na kiu ya kutaka kumfahamu Yesu Kristo Mkombozi wa dunia kwa njia za asili pamoja na matumizi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya kisasa. Kanisa kwa upande wake, linaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu, kwa kuwawezesha waamini kujenga uwezo na kujiamini katika masuala ya uongozi na shughuli za kichungaji. Kanisa linaendelea kuhimiza umuhimu wa utamadunisho, ili mila na desturi njema za waamini wa Oceania ziweze kukumbatiwa na tunu msingi za Kiinjili; kwa kutambua na kuthamini mambo matakatifu, zawadi ya maisha bila kusahau ukarimu.

Kanisa Katoliki Oceania linapenda kuwekeza katika majiundo awali na endelevu miongoni mwa waamini ili waweze kuchangia kwa hali na mali katika ustawi wa maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, Kanisa halina budi kujifunga kibwebwe kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa ari na nguvu mpya zaidi.

Kardinali Oswald Gracias, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Asia, amekazia umuhimu wa kuendeleza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani; majadiliano na tamaduni pamoja na watu maskini wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; ili kutoa kipaumbele cha kwanza kabisa cha uwepo wa Mungu katika maisha yao pamoja na kudumisha mshikamano wa kifamilia. Vyama vya kitume kwa ajili ya familia ni kati ya mafanikio makubwa ya Kanisa Katoliki Barani Asia, hata kama bado kuna vikundi vinavyotaka kudhoofisha utume huu ndani ya Jamii.

Familia hazina budi kujengewa uwezo wa kuthamini utakatifu wa maisha, ili ziweze kusimama kidete kupinga utamaduni wa kifo na kwamba, Jumuiya ndogo ndogo za kikristo ni nyenzo muhimu sana katika azma ya Uinjilishaji mpya, kwani zinasaidia kujenga na kuimarisha Jumuiya za Waamini Barani Asia. Itakumbukwa kwamba, Kanisa Barani Asia linaendelea kukabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na watu wenye misimamo mikali ya kiimani. Kutokana na ukweli huu, Majadiliano ya kidini yanakuwa ni nguzo msingi katika harakati za ujenzi wa Jamii inayoheshimu misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano.

Kanisa Barani Asia linayaangalia Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa matumaini makubwa, kwani, waamini wanapania kumfahamu zaidi Kristo; kwa njia ya Neno la Mungu, Sala na Tafakari ya kina pamoja na kutambua kwamba, Liturjia ni chemchemi ya imani ya Kanisa inayomwilishwa na waamini katika hija ya maisha yao hapa duniani. Changamoto kubwa kwa Kanisa Barani Asia, ni kuendelea kuwajengea vijana uwezo wa kutumia njia za mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu.








All the contents on this site are copyrighted ©.