Wito: Imarisheni juhudi za kuwahudumia wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi duniani
Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za
Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, akichangia hoja kwenye mkutano wa sitini na
tatu wa kamati tendaji ya Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, ameitaka kwa namna
ya pekee, Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kuimarisha mshikamano sanjari na kuwalinda
wakimbizi. Kinzani na migogoro inayoendelea kufuka sehemu mbali mbali za dunia,
imekuwa ni chanzo cha kuibuka kwa wimbi kubwa la wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi
maalum. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, hata baadhi ya vyombo vya habari
vinaendelea kufumbia macho tatizo hili kwa kuandika na kutangaza maeneo ambayo yanagusa
masilahi yao binafsi, kiasi cha kuwaacha wakimbizi na wahamiaji kutangatanga, hali
inayohatarisha usalama na maisha ya watu hawa. Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano
huu umetoa shukrani za dhati kwa Mataifa na Jumuiya za Kimataifa zinazoendelea kutoa
hifadhi na msaada kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji, wanaokimbia nchi zao kwa kuhofia
usalama wa maisha na mali zao. Wanatoa mwaliko wa pekee, kwa Jumuiya ya Kimataifa
kuzisaidia nchi kama hizi ili kubeba walay gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji
wanaoendelea kuongezeka maradufu kila siku ya maisha. Wajumbe hao wamelitaka Shirika
la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, kuhakikisha kwamba, linatoa ulinzi na
usalama kwa wakimbizi kwa kuzingatia sheria na kanuni za Umoja wa Mataifa. Ni jukumu
la Shirika hili kuongeza juhudi kwa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa kushirikiana
kwa karibu zaidi na Mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, alisema, Askofu mkuu Silvano
Maria Tomasi.