Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, karibu tena katika mfululizo wa vipindi vyetu
vya uinjilishaji wa kina. Juma lililopita tulizungumzia dhana ya uinjilishaji mpya
katika ulimwengu wa leo mintarafu maana yake na umuhimu wake. Leo tuendelee mbele
kuungana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI, anapobainisha maeneo muhimu yanayoguswa
moja kwa moja na Uinjilishaji Mpya.
Unijilishaji mpya anasema Baba Mtakatifu
ni ile hali ya kuwa na ari na moyo mpya wa kiutendaji ambapo Kanisa hutafsiri alama
za nyakati na kubainisha mazingira mapya anayoishi Mwanadamu na hivyo kubuni mbinu
mkakati za kumpeleka Kristo kuangaza mazingira haya ambayo kimsingi yanagusa Nyanja
zote za maisha ya Mwanadamu: kisiasa, kiutamaduni, kiuchumi na kidini.
Utamaduni
ni eneo la kwanza kabisa kuguswa na uinjilishaji mpya. Utamaduni wa leo umekumbwa
zaidi na mtazamo wa kidunia zaidi kuliko wa kiroho miongoni mwa wanajamii. Uchaji
na hofu ya Mungu vimetoweka kabisa na watu wala hawatoi tena kipaumbele kwa mambo
ya dini au mambo ya Mungu. Katika nchi za magharibi hali hii imeongezeka sana kiasi
kwamba Mungu taratibu anatoweka katika fikra za watu na badala yake watu wamezama
katika kuhangaika na mambo ya kiulimwengu tu mintarafu mali, nguvu na umaarufu. Badala
ya kuhangaikia wokovu war oho watu wanahangaika na kutafuta pesa zaidi, kutafuta kukuza
jina kwa karama fulani na kuonekana zaidi kuliko wengine.
Utamaduni huu wa
kidunia umejikita zaidi katika maisha ya mtu binafsi na uhuru wake hivi kwamba haukatai
moja kwa moja uwepo wa Mungu bali unakuza na kuweka mbele mambo ya dunia hivi kwamba
mtu hana muda wa kufikiria tena mambo ya Mungu. Aidha mtazamo huu wa kidunia hukuza
zaidi hisia tepetevu katika mambo muhimu ya maisha ya mtu na kurahisisha kila kitu
kuonekana cha kawaida. Katika mazingira haya watu wengi wameathirika kifikra na kimtazamo
na kuona kila kitu sawa na haki, hivyo kukuza hisia za kipenda roho hula nyama mbichi
au uzuri uko kwa jicho la mtazamaji. Kila kitu huwa halali ili mradi mtu havunji sheria
ya nchi. Hali hii imepelekea malumbano makali ndani ya wanafamilia, kuongezeka kwa
biashara ya ukahaba, dawa za kulevya na ndoa za jinsia moja.
Sekta ya jamii
ni eneo jingine muhimu linahitaji uinjilishaji mpya. Mchangamano wa watu unaotokana
na kuibuka kwa wimbi kubwa la uhamiaji katika kigezo cha utandawazi umechangia sana
katika kuporomoka kwa mila na desturi nyingi zilizokuwa zinajenga jamii fulani. Leo
hii kutokana na kukua kwa mawasiliano na ugumu wa maisha watu wengi wanahamia maeneo
ya miji, nchi fulani au bara fulani kwa kigezo cha kutafuta maisha bora. Hali hii
imegeuza kabisa sura za miji mingi na hata nchi fulani. Hali hii hupelekea kuporomoka
kwa utambulisho wa jamii fulani, kuzuka kwa mila na desturi za wastani ambazo basi
kila mtu anaishi kadiri ananvyoweza.
Njia za mawasiliano ni eneo jingine
nyeti linalohitaji uinjilishaji mpya. Njia bora za mawasiliano zimewesha upatikanaji
haraka wa habari, elimu na kukuza biashara. Njia za mawasiliano pia zimewezesha kuunganisha
watu kutoka pembe zote za dunia na kushirikiana iwe katika mawazo, maafa na mambo
mengine. Lakini lazima pia kuona hatari inayotokana na urahisi huo wa mawasiliano
kati ya watu. Mtandao kwa mfano unatoa changamoto kubwa sana kwa watu wa marika yote
pale unapotumika kudhalilisha ubinadamu, kuunganisha magendo, kupanga njama za kigaidi,
kusambaratisha ndoa n.k. Hivyo ni lazima kwa wanafamilia ya Mungu kuelimishwa namna
bora ya matumizi ya mtandao.
Mpendwa msikilizaji, wakati ukuta. Kufikia hapa
tumefikia mwisho wa kipindi chetu kwa siku ya leo. Mungu akubariki katika yote, akuzidishie
imani, matumaini na mapendo. Nikikuaga kutoka studio za Radio Vatican ni mimi mtayarishaji
na msimulizi wako Padre George wa Bodyo.