Imarisheni huduma za afya kuzuia ugonjwa wa upofu duniani!
Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba, inaadhimisha Siku ya Vipofu
Duniani. Taarifa za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wagonjwa
wenye tatizo la macho wapatao millioni mia mbili na themanini na tano duniani na kati
yao kuna watu millioni thelathini na tisa ni vipofu kabisa. Tatizo la upofu linaendelea
kukua na kuongezeka kwa kasi Barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini na katika baadhi
ya nchi za Ulaya. Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kwamba, kuna jumla
ya watoto millioni sita ambao wanakabiliwa na upofu, kati yao kuna watoto millioni
nne ambao ikiwa kama wangepata huduma bora ya afya na tiba wangeweza kusalimisha uwezo
wao wa kuona, lakini kwa vile wanaishi vijijini ambako mara nyingi huduma za afya
bado ni duni, wamejikuta wanakabiliwa na upofu. Kutokana na changamoto hii, kuna
haja kwa Jumuiya ya Kimataifa, Serikali na watu binafsi kuongeza jitihada za kuboresha
tiba kwa kukazia kwa namna ya pekee, kinga dhidi ya magonjwa yote yanayoweza kupelekea
upofu kwa watu. Jitihada hizi hazina budi kutekelezwa tangu watoto wakiwa wachanga.
Ni changamoto pia kwa Jamii kujenga utamaduni wa kuwaheshimu, kuwathamini na kuwasaidia
vipofu katika shida na mahangaiko yao, ili waweze kujisikia kuwa hata wao ni sehemu
ya Jamii inayowazunguka licha ya matatizo wanayokabiliana nayo. Utu na heshima
yao kama binadamu vinapaswa kuzingatiwa na pale inapowezekana, basi wajengewe uwezo
wa kujitegemea wao wenyewe. Inasikitisha kuona kwamba, vipofu wamekuwa ni kero katika
mitaa ya miji mingi duniani, watu ambao wanatangatanga barabarani ili kupata riziki
yao, huku wakisaidiwa na watoto wadogo ambao kimsingi walipaswa kuwa shuleni wakisoma,
matokeo yake, hata watoto hawa wanajikuta wakitumbukia katika mzunguko wa umaskini
kwa kukosa elimu ambayo ni msingi na mkombozi mkuu wa mwanadamu.