Huu ni muda muafaka wa kujikita katika Uinjilishaji wa kina!
Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, baada ya kuwa pamoja katika tafakari ya Hati
ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI, Africae Munus, nakukaribisha tena katika
mfululizo wa vipindi vyetu vya uinjilishaji wa kina. Katika juma hili, tukizingatia
kuanza kwa Sinodi ya Maaskofu juu ya uinjilishaji mpya hivi karibuni, basi tuangalie
japo kwa ufupi nini Mama Kanisa anawaongoza Maaskofu kujadili ili kuboresha na kuimarisha
utume wa Kanisa kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wa Yesu.
Katikati ya
mwezi wa Tisa mwaka huu, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alitoa hati (linieamenta) ambayo
ni kama chombo cha kufanyia kazi na Maaskofu wa Sinodi juu ya uinjilishaji mpya. Katika
hati hii Baba Mtakatifu anaanza kwa kufanunua dhana nzima juu ya uinjilishaji mpya
hususan nini maana ya uinjilishaji mpya na uhitaji wake leo katika Kanisa. Dhana ya
uinjilishaji mpya ilianza na Mwenye heri Yohane Paulo wa Pili, alipotembelea Poland
na baadaye dhana hii ilipata mvuto zaidi alipotembelea Amerika ya Kusini.
Mwenye
Heri Yohane Paulo wa Pili, akiwa Amerika ya Kusini, aliitumia dhana ya Uinjilishaji
mpya akitaka kuamusha tena miongoni mwa wanafamilia ya Mungu Amerika ya Kusini ile
nguvu, ari na kasi mpya ya uinjilishaji barani Amerika ya kusini baada ya uinjilishaji
wa awali kufanyika. Kumbe uinjilishaji mpya unabeba pamoja na mambo mengine ari, kasi
na nguvu mpya ya uinjilishaji kwa kutumia mbinu mpya na njia mpya za uinjilishaji
katika mazingira ya mapya yenye muonekano, mahitaji, matatizo na mtazamo mpya kuhusu
maisha na jamii.
Tunapozungumzia uinjilishaji mpya haimaanishi kuwabatiza watu
upya au kubadilisha Injili, bali kumpeleka Kristu ndani kabisa katika maisha ya mtu
ya kila siku mahali pale alipo. Uinjilishaji mpya hauishii kutangaza tu Imani ya Kristu
bali kuwafanya waumini kumwelewa zaidi Kristu na ujumbe wake ndani kabisa ya maisha
yao ya kila siku.
Uinjilishaji Mpya unalenga kumuwezesha muumini kuiishi imani
yake kwa kujiamini zaidi kwani kwayo anaona njia ya kufuata, anapata ukweli kuhusu
maswali mengi ya maisha na hatimaye uzima utokanao na ushuhuda wa maisha ya Imani
aliyoipokea na kuiamini tangu alipobatizwa. Katika ujumla wake uinjilishaji mpya unalenga
kutangaza ufalme wa Mungu katika mazingira mapya katika maana kwamba Binadamu ameongezeka
kimo na akili katika kuutawala ulimwengu wake.
Maendeleo ya sayansi na teknologia
ambayo yamepelekea kuongezeka kwa ustawi wa jamii, utandawazi ambao umepelekea dunia
kuwa ndogo kama kijiji, kuongezeka kwa ushirikiano miongoni mwa mataifa kwa upande
mmoja; na ongezeko la watu, kupungua kwa kasi kwa rasilmali za dunia, migogoro ya
kisiasa nyuma ya tofauti za kiimani, ugumu wa maisha kwa watu wengi, kuyumba kwa uchumi
wa kimataifa, na kuongeza kwa biashara haramu ya dawa za kulevya na watoto ni miongoni
mwa mambo ambayo yaipa sura mpya dunia ya leo ambamo Kanisa linaishi na kuendeleza
utume wake.
Katika mazingira hayo Kanisa linawajibika bado kuendeleza utume
wake wa awali kumpeleka Kristo kule ambako bado hajafika lakini zaidi kuwaimarisha
wale walikwishakumpokea Kristo tayari. Ili kufanya vizuri katika utume wake Kanisa
halina budi kuwaimarisha watoto wake nyumbani ili waweze kuwavuta watoto wenzao huko
barabarani na kuwaleta nyumbani. Changamoto za maisha ya dunia ya leo hazijaliacha
Kanisa salama. Wanafamilia ya Mungu wanapambana na changamoto hizi kumbe wanahitaji
majibu sahihi kukidhi changamoto hizi.
Leo hii ambapo Makanisa mengi mahali
pengi yamegeuzwa kuwa kumbi za starehe, kupungua kwa miito ya Upadre na Utawa, kusambaratika
kwa thamani ya ndoa na familia miongoni mwa vijana ni mambo ambayo Kanisa lazima litulie
na kubuni mbinu mkakati za kuweza kurudisha tena Imani ya Kanisa miongoni mwa watu.
Mpendwa
msikilizaji kwa kifupi huo ndio uinjilishaji mpya. Naomba nikutakia Baraka tele toka
kwa Mwenyezi Mungu na kukushukuru sana kwa kuwa nami kwa muda wote huu. Tuonane tena
juma lijalo wakati na wasaa kama huu. Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi mtayarishaji
na msimulizi wako Padre George wa Bodyo.