2012-10-11 14:29:47

Papa azindua Mwaka wa Imani na maadhimisho ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa Ibada ya Misa Takatifu!


Tangu mapema Alhamisi hii, 11 Oktoba 2012, maelfu ya waamini, walifurika katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Mjini Vatican, kushuhudia kuzinduliwa kwa mwaka wa Imani na maadhimisho ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican, pia kutimia wka miaka 20 tangu kuchapishwa kwa Kateksimompya ya Kanisa Katoliki.
Baba Mtakatifu Benedikto XV1, aliingia katika uwanja huo majira ya saa nne za asubuhi kwa Maandamano ya Makadinali na Maaskofu kama ifuatavyo kwamba, Jumla ya waadhimishaji wakiwa 400 yaani Makardinali 80, Mapatriaki wa Kanisa la Mashariki 8, Maaskofu Wakuu na Maaskofu Sinodi 191, na Marais wa Mabaraza ya Maaskofu kutoka pande zote za dunia 104 na mapadre kadhaa wanaohudhuria Sinodi inayoendelea hapa Vatican , juu ya uinjilishaji mpya.
Papa katika homilia yake , kwa taadhimia na shukurani za dhati, aliwashukuru wote waliohudhuria Ibada hii, wakiwepo pia wakuu wa Makanisa mengine, Patriaki Bartholomew 1 wa Upatriaki wa Constantinople, Pia Mkuu wa Jumuiya ya Waanglikan, Askofu Mkuu Dr. Rowan Williams wa Canterbury. Pia Papa alionyesha kufurahia maandamano yaliyofungua Ibada akisema, yalirudisha kumbukumbu kwa Baraza la Mtaguso wa 11 wakati Mababa wa Baraza hilo, walipoingia katika Kanisa hili, wakiwa na Nakala ya kitabu cha Injili kilichotumika na kitabu cha Katekisimu ya Kanisa Katoliki.
Papa ameeleza ishara hizi, zinasaidia si tu kukumbuka ya yaliyotendeka siku za nyuma, lakini pia kuona uwezekano wa kusonga mbele, zaidi ya kukumbuka.”Ni wito unaotutaka kuzamisha zaidi harakati za kusonga mbele kiroho, kama Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican unavyohimiza, kuufanya upya utu wetu na maisha kuendelea kwa kadiri ya maana yake halisi”. Na maana yake ya halisi, inabaki kuw ileile, kuwa na imani kwa Kristo, imani ya kitume, inayohamasishwa na hamu ya ndani ya kukutana na Kristo kama mtu binafsi na watu wote, katika Hija ya Kanisa, sambamba na mapito ya historia.
Papa aligeukia Mwaka wa Imani, na maelezo kwamba, Mwaka huu unaozinduliwa leo, una muungano na mapito ya kanisa katika kipindi kizima cha miaka hamsini iliyopita: yaani tangu wakati wa Baraza Kuu la Pili , kupitia mafundisho ya Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI, ambaye alitangaza Mwaka wa Imani hapo 1967, hadi Jubilei Kuu ya mwaka 2000, ambamo Mwenye Heri Yohane Paulo II, alirudia kutaja ubinadamu wote wa Yesu Kristo, kuwa Mkombozi pekee mmoja , jana, leo na milele.
Papa Benedikto XV1 , aliendelea kusema kwamba, kati ya Mapapa hawa wawili , Paulo VI na Yohane Paulo II, maelezo yao yana muungano wa kina na bayana, juu ya Kristu, kwamba , ndiye kiini cha historia, kama inavyoonyeshwa na hamu yao ya kitume, ya kutaka kumtangaza Kristu, ulimwenguni kote. “ Yesu ni mtima wa imani ya Kikristo. Mkristo anaamini katika Mungu ambaye sura yake ilidhihirishwa na Yesu Kristo. Yesu ni utimilifu wa Maandiko Matakatifu na Mkalimani pekee wa ukweli. Yesu Kristo si chambo cha imani lakini, kama ilivyoandikwa katika Barua kwa Waebrania, Ndiye aliyeianzisha imani yetu na ndiye atakayeikamilisha (12:02)”.
Papa amesema, uwepo wa mwaka wa Imani na uinjilishaji mpya, maadhimisho haya si tu kwa heshima ya kumbukumbu ya miaka 50, lakini kwa sababu kuna haja ya kufanya hivyo, hata zaidi ya ilivyokuwa miaka hamsini iliyopita! Na jibu linalohitajika kutolewa katika haja hii, na ni moja ya hamu za Mapapa na Baraza la Maaskofu na yaliyomo katika nyaraka zake. Hata juhudi za kuunda Baraza la Kipapa kwa ajili ya ukuzaji wa uinjilishaji mpya, zinapaswa kueleweka katika muktadha huo.
Na aliangalisha katika hali halisi za maisha ya jamii katika miongo ya hivi karibuni, akisema, kuna “kiu na jangwa la kiroho”. Amekilinganisha kipindi cha miaka ya 1960 wakati wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na sasa na kutoa maelezo kwamba,w akati ule kulikuwa na uwezekano mdogo wa kuona vitisho vya utendaji usiojali uwepo wa Mungu, lakini sasa imekuwa ni utendaji wa kila siku unaoshuhudiwa” Utupu umeenea”.
Hata hivyo, Papa ameonyesha matumaini yake kwamba, katika uzoefu huu wa utupu na jangwa, panakuwa ni mahali pa kuanzia, kuigundua tena furaha ya kuamini na umuhimu wake kwetu sote , wake kwa waume. Katika jangwa, tunapata kuona tena kitu kilicho cha thamani zaidi katika maisha yetu. Kitu cha thamani katika dunia ya leo yenye kuwa ishara nyingi , zinazo jionyesha waziwazi kuwa na kiu kwa Mungu, na katika kujua hatima ya maisha. Katika jangwa hili la Imani, watu wa imani wanahitajika, kuyaonyesha maisha yasiyokaukiwa na tumaini, kwa mfano wa maisha yao wenyewe, wanaionyesha njia inayoelekea katika nchi ya ahadi na kuliishi tumaini hai.
Wanaoishi kwa imani, huufungua moyo katika neema ya Mungu, inayotuweka huru dhidi ya kukosa matumaini. Leo hii kuliko ilivyokuwa hata siku za nyuma, uinjilishaji una maana ya kushuhudia maisha mapya, kubadilishwa na Mungu, na hivyo kuonyesha njia yenye tumaini .
Na mwishowe, Papa ameukabidhi Mwaka wa Imani katika dhamana ya Mama Bikira Maria Mtakatifu sana, Mama wa Mungu,akimwomba daima aangaze kama nyota, katika njia ya uinjilishaji mpya. Na asaidie kuweka katika vitendo, mafundisho ya Mtume Paulo yanenayo” Ujumbe wa Kristo na ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Na kila mfanyalo, kwa neno au tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kupitia kwake " (Kol 3:16-17). Amina.








All the contents on this site are copyrighted ©.