2012-10-09 12:15:11

Zaidi ya watu millioni 870 wanakabiliwa na utapiamlo duniani


Taarifa ya Umoja wa Mataifa inaonesha kwamba, kwa sasa kuna zaidi ya watu millioni mia nane na sabini, wanaokabiliwa na tatizo la utapiamlo kutoka sehemu mbali mbali za dunia, lakini, bado kuna uwezekano wa kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millenia. Hayo yamo kwenye taarifa za Mashirika ya Chakula, Usalama wa Chakula Duniani na Mpango wa Chakula Duniani.

Waathirika wakuu wa baa la njaa ni wale wanaoishi katika Nchi changa zaidi duniani, wanaokadiriwa kufkia zaidi ya watu millioni mia nane na hamsini na mbili. Hawa ni jumla ya asilimia kumi na tano ya idadi ya watu wote wanaokabiliwa na baa la njaa duniani. Watu wengine millioni kumi na sita, wanaishi katika nchi zilizoendelea zaidi ulimwenguni.

Inasikitisha kuona kwamba, hata katika ulimwengu unaotaliwa na kwa kiasi kikubwa kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia bado kuna watoto zaidi ya millioni mia moja wenye umri chini ya miaka mitano, wanasumbuliwa na utapiamlo wa kutisha. Hali hii kwa kiasi kikubwa anasema Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO kwamba, inachangia kudumaza maendeleo ya watoto hawa: kijamii, kiuchumi na kiutu! Utapiamlo bado unaendelea kusababisha vifo kwa zaidi ya watoto millioni mbili nukta tano kila mwaka.

Haya yote ni matokeo ya myumbo wa uchumi kimataifa, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia juhudi za kukwamua uchumi katika Nchi zinazoendelea duniani, kwa kuzijengea uwezo wa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kwa ajili ya watu wake.

Licha ya changamoto zote hizi, Umoja wa Mataifa una imani kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kufikia Malengo ya Millenia, ifikapo mwaka 2015 kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa duniani. Kuna idadi kubwa ya watu wanaoishi Barani Asia wanateseka kwa baa la njaa, lakini hali hii inazidi kuongezeka kwa kasi Barani Afrika. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo, sanjari na kuwawezesha wakulima kuboresha kilimo ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula.

Licha ya baa la njaa kuendelea kutesa watu wengi zaidi duniani, lakini pia kuna watu zaidi ya billioni moja nukta nne wanasumbuka kutokana na kuwa na uzito wa kupindukia, kiasi cha kuhatarisha maisha yao. Juhudi za makusudi hazina budi kufanywa na Jumuiya ya Kimataifa ili kuokoa maisha ya watoto wanaosumbuliwa na utapimlo wa kutisha, kwa kuwekeza katika kilimo na elimu sanjari na kukuza uwezo wa uzalishaji kiuchumi, ili kupunguza baa la njaa na hatimaye kufuta kabisa tatizo la utapiamlo.







All the contents on this site are copyrighted ©.