Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika barua yake ya kichungaji “Porta Fidei”
ametangaza maadhimisho ya Mwaka wa Imani utakaofunguliwa rasmi hapo tarehe 11 Oktoba
2012, kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka hamsini tangu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican
ulipofunguliwa. Mwaka wa imani utahitimishwa rasmi katika maadhimisho ya Siku kuu
ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu hapo tarehe 24 Novemba, 2013. tarehe 11 Oktoba 2012
ni kumbu kumbu ya miaka ishirini tangu Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki ilipochapishwa
kwa mara ya kwanza, chini ya uongozi wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, akipania
kuwaonesha waamini nguvu na uzuri wa imani.
Baba Mtakatifu
anasema, mlango wa imani daima uko wazi na unaendelea kutoa mwaliko kwa waamini kujenga
uhusiano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa. Inawezekana kabisa kujenga uhusiano
huu ikiwa kama Neno la Mungu linahubiriwa na mioyo ya waamini inaruhusu Neno hili
kuleta mabadiliko ya ndani katika maisha kwa njia ya neema.
Tangu mwanzo Baba
Mtakatifu anasema, amekuwa anawahimiza waamini kugundua hija ya imani itakayowawezesha
kuona mwanga wa furaha ari mpya ya kukutana na Yesu Kristo. Miaka iliyopita ilikuwa
ni rahisi kwa jambo hili kutokana na mwelekeo wa kitamaduni uliokuwepo na kukubalika
mintarafu miongoz ya imani na tunu msingi za maisha ya kiroho. Lakini, kwa sasa hali
imebadilika sana kutokana na mmong’onyoko wa tunu msingi za maisha ya kiimani, kiutu
na kimaadili ambao umewakumba watu wengi duniani.
Itakumbukwa kwamba, Mwezi
Oktoba, 2012, kutakuwepo na Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji
Mpya, inayoongozwa na kauli mbiu “Uinjilishaji mpya kama njia ya kurithisha imani
ya Kikristo”. Hiki kitakuwa ni kipindi muafaka kwa Mama Kanisa kufanya tafakari ya
kina pamoja na kuendelea kutambua umuhimu wa imani, kama sehemu ya mwendelezo wa Mwaka
wa Imani uliotangazwa na Papa Paulo wa sita, kunako Mwaka 1967; mwaka ambao ulihitimishwa
kwa kuchapisha “Kanuni ya imani ya Watu wa Mungu”, ili kuonesha maudhui ya imani ambayo
yamekuwa ni urithi wa Mama Kanisa kwa miaka mingi; imani ambayo haina budi kudumishwa,
kufahamika na kufanyiwa tafakari ya kina kila wakati, ili hatimaye, waamini waweze
kuitolea ushuhuda mintarafu mazingira ya kihistoria, pengine tofauti kabisa na hali
ilivyokuwa kwa miaka iliyopita.
Baba Mtakatifu anasema, Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani yamekuja wakati muafaka kabisa, Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilee ya Miaka
Hamsini tangu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulipofunguliwa, mwaliko kwa waamini
kutafakari kwa makini urithi mkubwa unaofumbatwa katika hati mbali mbali zilizotolewa
na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, nguvu na ari mpya katika maisha na utume
wa Kanisa.
Mama Kanisa anaendelea kushuhudia mabadiliko kutokana na ushuhuda
unaotolewa kwa njia ya maisha ya watoto wake; uwepo wao duniani na kwamba, Wakristo
wanaalikwa kuonesha nuru ya mwanga wa ukweli, walioachiwa na Yesu Kristo mwenyewe.
Mama Kanisa anatambua kwamba, miongoni mwa watoto wake kuna wadhambi, lakini ni Takatifu
na daima linahitaji kujitakasa.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema,
Mwaka wa Imani unalenga kuleta mwamko mpya katika wongofu wa ndani kwa Yesu Kristo
Mkombozi wa Ulimwengu. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka amedhihirisha Pendo linalookoa
na hivyo, huu ni mwaliko wa kuongoka kwa njia msamaha wa dhambi, ili kuweza kukumbatia
maisha mapya yanayojikita katika imani, inayomletea mwamini mabadiliko ya ndani na
ukweli mpya kwa njia ya Ufufuko. Hii ni imani inayotenda kwa njia ya upendo, kigezo
kipya cha uelewa na matendo yanayoleta mabadiliko katika maisha ya mwanadamu.
SEHEMU
YA PILI: MLANGO WA IMANI
Kwa njia ya upendo wake wa dhati, Yesu Kristo aliweza
kuwavuta watu wa nyakati zote; kwa njia ya Kanisa lake, anaendelea kuwaalika wengine
pamoja na kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, changamoto ambayo
daima ni endelevu. Kanisa linakabiliwa na changamoto ya Uinjilishaji ili kuwawezesha
waamini kutambua ile furaha ya kuamini na kushirikisha imani yao. Waamini wanapaswa
kugundua upendo wa Kristo kila siku ya maisha yao; kwa kujitoa kwa ajili ya kazi za
kimissionari, ili iweze kusonga mbele. Imani inakuwa pale tu inapomwilishwa kwa njia
ya mang’amuzi ya upendo unaopokelewa kwa dhati na kuwashirikisha wengine kama mang’amuzi
ya neema na furaha.
Kwa kuamini anasema Baba Mtakatifu, imani inakuwa na kuimarika
zaidi, kiasi kwamba, inakuwa ni vigumu kwa mwamini kuipatia kisogo, kwani hata upendo
kwa Mwenyezi Mungu utakuwa unaimarika zaidi, kwani Yeye ndiye chemchemi ya upendo
huo. Mama Kanisa anapenda kuadhimisha Mwaka wa Imani kwa ari kubwa zaidi, ili uweze
kuzaa matunda yanayokusudiwa. Tafakari kuhusu imani haina budi kuimarishwa zaidi,
ili kuwawezesha waamini kumfahamu Kristo zaidi na kujishikamanisha na Injili, hasa
wakati huu ambapo mwanadamu anashuhudia mabadiliko makubwa katika maisha yake.
Ni
kipindi cha kuungama imani kwa Kristo Mfufuka, ili kila mwamini aweze kuifahamu vyema,
ili hatimaye, kuirithisha kwa kizazi cha sasa. Jumuiya, Parokia na Vyama vya Kitume
vinachangamotishwa kutafuta njia ambayo itawawezesha kuungama imani yao hadharani
katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Mama Kanisa anapenda kuona watoto wake
wakiungama imani yao katika ukamilifu wake, kwa mwamko na ari mpya zaidi, kwa kujiamini
pamoja na kuwa na matumaini makubwa zaidi. Iwe ni fursa ya kuimarisha imani katika
Liturjia na kwa namna ya pekee katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini
na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni changamoto kwa waamini kutoa ushuhuda
unaoaminika. Waamini watambue maudhui yaliyomo kwenye Kanuni ya Imani wanayoungama,
wanayoadhimisha, ishi na kusali; mintarafu imani inayomwilishwa katika maisha ya kila
mwamini.
MLANGO WA IMANI SEHEMU YA TATU
Imani si jambo binafsi anasema
Baba Mtakatifu, bali inapaswa kushuhudiwa katika maisha ya hadhara. Hili ni tendo
huru linalohitaji uwajibikaji na utendaji wa maisha ya kijamii kwa mtu anaye amini.
Imani ni jambo binafsi linalofumbata pia maisha ya Kijumuiya. Imani ni urithi wa Kanisa,
ni urithi wa Jumuiya ya waamini na kwa kila Mbatizwa anayo alama isiyofutika inayomshirikisha
katika kundi la watu wanaoamini ili kupata uzima wa milele.
Maudhui ya Imani
ni jambo la msingi, ili kumwezesha mwamini kuikiri kwa akili na utashi wake, kile
ambacho Kanisa linafundisha. Ufahamu wa kiimani unamfungulia mwamini uelewa mpana
wa Fumbo la Ukombozi lililofunuliwa na Mwenyezi Mungu. Mwamini anapokubali kwa akili
na utashi wake inamaana kwamba, anakubali kimsingi Fumbo la Imani, kwani Mungu ndiye
anyemhakikishia ukweli wake na kumpatia fursa ya kuonja pendo lake.
Baba Mtakatifu
anasema, imani haina budi kuzingatia pia tunu msingi za maisha ya kitamaduni, kwani
hata kama kuna umati mkubwa wa watu ambao hawana imani, lakini, wako katika hija ya
kutafuta ukweli kuhusu maisha yao hapa duniani. Hija hii ya imani inawaongoza katika
kulifahamu Fumbo la Mungu. Daima akili inatafuta kile kilichochema na kinachodumu;
kwani haya ni mambo ambayo yamepigwa chapa katika moyo wa mwanadamu na yanapata utimilifu
wake katika Mungu mmoja. Imani inatoa mwanya kwa waamini kuuona utimilifu wake.
Katekisimu
Mpya ya Kanisa Katoliki ni nyenzo msingi katika kuifahamu imani ya Kanisa kwa muhtsari.
Haya ni matunda makuu ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto katika maadhimisho
ya Jubilee ya miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kugundua tena na tena
ile misingi ya imani, kama inavyopembuliwa kwa kina na mapana katika Katekesimu Mpya
ya Kanisa Katoliki na jinsi ambavyo waamini wanaweza kuimwilisha imani hii, baada
ya kushiriki katika tafakari ya kina iliyofanywa na Mama Kanisa. Ni nyenzo muhimu
katika majiundo endelevu kwa waamini mintarafu tamaduni za watu husika. Kanisa linaandaa
mwongozo maalum utakaowawezesha waamini kuadhimisha kikamilifu Mwaka wa Imani, mintarafu
azma ya Uinjilishaji.
Baba Mtakatifu anasema, kuliko ilivyokuwa miaka kadhaa
iliyopita, waamini leo hii wanakabiliana na maswali magumu katika hija ya maisha yao
kutokana na mabadiliko ya mwono; maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayokuja kwa
kasi katika Ulimwengu wa Utandwazi. Kanisa daima linapenda kuonesha kwamba, hakuna
kinzani kati ya Sayansi na Imani, kwani njia zote hizi zinapania kuufikia ukweli.
Mwaka
wa Imani, uwe ni muda wa kufanya hija ya historia ya imani ya Kanisa, inayofumbata
utakatifu wa maisha na uwepo wa dhambi. Kuna maelfu ya watoto wa Kanisa ambao wamejitoa
kimaso maso katika mchakato wa kumletea mwanadamu maendeleo endelevu kwa njia ya ushuhuda
wa maisha yao. Kwa wale ambao wanaogelea katika lindi la dhambi na mauti, ni mwaliko
wa kutubu na kuongoka, ili kuonja kwa mara nyingine tena huruma ya Mungu katika maisha
yao.
Baba Mtakatifu anasema, Mwaka wa Imani kiwe ni kipindi cha kutolea ushuhuda
matendo ya huruma, kwani imani inamwilishwa katika matendo. Watoto wa Kanisa wamekuwa
na utamaduni wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili huduma ya upendo kwa jirani zao;
hasa kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wapweke, wasiopendwa wala kuthaminiwa
na jamii inayowazunguka; Wote hawa kwa namna moja au nyingine wanaonesha ile sura
ya Kristo. Kwa njia ya imani, waamini wanaweza kuitambua Sura ya Kristo Mfufuka anayeomba
kuonjeshwa upendo wa dhati.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa na imani
thabiti katika hija ya maisha yao ya kiimani na kamwe wasikumbwe na uvivu. Imani inapaswa
kuandamana na waamini wenyewe katika maisha yao, daima wakijitahidi kuiuisha kwa ari
na nguvu zaidi, kama kielelezo cha matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu.
Ni mwaliko wa kusoma alama za nyakati na kwamba, imani inamchangamotisha mwamini kuwa
ni alama hai ya uwepo wa Kristo Mfufuka ulimwenguni.
Baba Mtakatifu anasema,
ulimwengu wa leo unahitaji kuona mashahidi amini wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa
ajili ya Mungu na jirani zao, ili kuweza kuzima kiu ya watu wanaomtafuta Mungu katika
maisha, ili hatimaye, waweze kupata maisha yenye uzima wa milele.