2012-10-08 15:16:19

Upadre ni changamoto kwa maisha ya vijana!


Katika asilimia kubwa ya jamii, kama sio jamii zote, ukasisi umekuwa ukichukua nafasi kubwa sana katika maisha ya kila siku ya jamii husika. Dini ni sehemu ya muhimu sana na ni kiini cha maisha ya mwanadamu, kwa sababu hiyo makasisi wamekuwa wakitoa huduma ya kutoa sadaka kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya jamii nzima, makasisi wamekuwa wakiunganisha mambo ya mhusuyo Mungu na wanadamu. Kujitakasa wao wenyewe, kuwatakasa wana jamii na kuitakasa jamii yenyewe.
Hata leo tunao makasisi katika Kanisa, makasisi ambao wanachota huduma ya ukasisi huo kutoka kwa Kristo mwenyewe. Katika huduma nyingi wanazotoa makasisi, pengine huwa unajiuliza mara kwa mara ni kwa nini au inakuwaje kasisi anahusika na hili au lile, au kwa nini asihusike na hili au lile.
Napenda kukukaribisha katika tafakari yetu leo, ili upate kuitambua huduma ya kasisi ni ipi katika Kanisa na jamii inayomzunguka. Hii itakusaidia kuwaelewa Makasisi wanaokuhudimia, na kama wewe ni kasisi itakusaidia kukukumbusha mambo mengi juu ya ukasisi wako na kama kijana bado hujachagua namna yako ya kuishi utakatifu, basi tafakari vema juu ya hili, pengine huo ndio wito wako.
Makasisi ni makuhani katika jamii, na wamewekwa kuwa makuhani ili kutolea sadaka kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya wengine na ulimwengu mzima. Sadaka wanayotolea leo makuhani hawa wa Kanisa ni kumbukumbu hai ya sadaka ya Kristo msalabani kwa ajili ya maondoleo ya dhambi na wokovu, kumbukumbu inayofanywa kuwepo wakati huo wa kuitolea sadaka. Makuhani katika sadaka hiyo huwatakasa wanadamu na ulimwengu mzima. Kwa sadaka hiyo huwaunganisha wanadamu, viumbe vyote na Mungu aliye Muumba wa vyote.
Makasisi ni walimu wa imani, walimu kuhusu mambo ya mhusuyo Mungu na mafumbo makuu ya ulimwengu huu. Makasisi ni walimu wa namna ya kuishi ubinadamu wako, ni walimu wa maadili mema ya kikristo.
Makasisi ni manabii katika jamii unamoishi. Ni manabii sababu wao ni watafsiri wa matukio ya maisha, matukio yaliyopita, matukio ya wakati wa sasa na matukio yatakayokuja. Katika kutafsiri matukio ya maisha ya kila siku, manabii hawa huonesha na kufundisha pia mahusiano yaliyopo kati ya matukio hayo.
Manabii hawa wanao wajibu wa kuonya na kutahadharisha kila mwana jamii juu ya matukio ya kila siku na namna ya kuishi vema kadiri ya mapenzi ya mwenyezi Mungu. Wewe uliye kasisi na nabii, hufafanui mambo yako binafsi wala kutafsiri matukio au mawazo yako, bali wewe ni mjumbe wa Mungu, na unatafsiri na kufafanua yale tu unayoagizwa na Mwenyezi Mungu.
Makasisi ni wafalme. Ufalme wenu makasisi upo sio katika ubabe, sio katika kampeni kupata kura, sio katika mapinduzi na vita vya kibinadamu kujipatia mamlaka, bali ninyi ni wafalme, mkishiriki ufalme wa Kristo mwenyewe ili kuliongoza Taifa la Mungu kuelekea Yerusalemu mpya. Ninyi ni viongozi katika jamii. Viongozi mnaosaidia wengine namna ya kuishi vema, viongozi mnaotoa ushauri bora, viongozi katika hija ya maisha ya Familia ya Mungu hapa duniani kimwili na kiroho. Ninyi ni wafalme mnaoilinda haki na amani ili dunia iwe kweli ni mahali bora pa kuishi. Ninyi ni wafalme kwa mifano bora ya maisha na utu wema.
Wito wa ukasisi, sio wito wa kujiamulia bali ni Kristo mwenyewe ndiye mwenye kuchagua wale awapendao ili washiriki naye kwa karibu kuiendeleza sadaka ya wokovu wa ulimwengu mpaka miisho ya dahari. Ni sauti ya Mungu anayekuita kwa upendo, nawe unaalikwa kuiitikia kwa upendo, kwa uhuru na kwa moyo mkunjufu. Ni sauti ya ndani ya moyo wako, sauti inayokuita kila siku, kwani ni wito sio wa siku moja, bali wito wa maisha. Isikilize kwa makini sauti hiyo ya Mungu na uifuate.
Katika kuwasaidia vijana kuitambua na kuiitikia sauti hiyo kama kijana Samueli, Jumuiya nzima ya wana wa Mungu mnahusika. Kila mmoja kwa nafasi yake: Maaskofu, Makasisi, mashemasi, wazazi, walezi na kila mwamini. Unalo jukumu hilo kubwa kuwasaidia vijana kuitambua sauti hiyo na kuwaongoza ili kuitikia vema na kusihi vema ukasisi wao.
Dunia itakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kubadilika na kuzaa matunda bora ya haki, amani na maisha bora, iwapo utaandaa makasisi bora. Kazi kwako, mi nakuacha na changamoto hiyo. Makala ya vijana Radio Vatican inakusubiri tena juma lijalo katika mida na nyakati kama hizi. Nikisanzuka kwa kunesanesa, ni sauti ya kinabii, Celestin Nyanda.








All the contents on this site are copyrighted ©.