2012-10-08 15:00:53

Tatizo la vidhibiti na vizuia mimba kwa wanandoa!


Ndugu msilizaji wa Radio Vatican katika vipindi vyetu viwili vilivyopita tumejenga mazingira mazuri yanayotushuhudia kuwa muungano wa kimwili na zawadi ya watoto huenda pamoja nayo hukumbatia nafasi ya ubaba na umama kati ya wanandoa. Leo nakualika tugeukie vidhibiti mimba ambavyo vilishika kasi miaka mingi iliyopita na mpaka leo vinaendelea licha ya Waraka wa Kichungaji uliotolewa na Papa Paulo wa sita; humane Vitae ya 1968 kuhusu maisha ya Mwanadamu. Msimamo huu ukaimarishwa zaidi na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili, katika Waraka wake wa Kichungaji Evangelium Vitae: Injili ya Uhai
Kama muungano wa kindoa hautenganishwi na uzazi, na uzazi hautenganishi na malezi ya watoto. Iweje kwa sababu za msingi wana-ndoa wanapotamani kupumzika uzazi na wakati huo huo kuendelea kutunza upendo kati yao kwa njia ya muungano wa kindoa? Je, si sahihi kutafuta njia yoyote kupanga uzazi? Kanisa linakubali kwamba kweli kuna wakati ambao busara ya kawaida hairuhusu kuendelea kuleta watoto ulimwenguni. Hata hivyo, lengo hili zuri la kupumzika uzazi kwa wakati fulani ni lazima lizingatie mpango wa asili uliowekwa katika maumbile ya mwanadamu kwa namna ya pekee mwanamke.
Namba 14 ya barua hii ya Papa Paulo VI, inasema “tendo lolote, kabla, wakati na hata baada ya kukutana kimwili lenye lengo la kuzuia mimba kwa makusudi kama njia na lengo la mwisho sio sahihi” Japo wana-ndoa wanaungana kimwili lakini muungano wao ni kimwili tu bila lengo la kuwa wazazi kwani wameshakataa uzazi.
Mafundisho haya ya Kanisa yanaendelea kuwa magumu hasa nyakati zetu kwani wote tunajua kila mtoto anayezaliwa ulimwenguni anahitaji matunzo ikiwemo elimu na mahitaji msingi katika maisha yao. Sio kweli kwamba, kila mtoto anayekuja ulimwenguni anakuja na bahati yake, kama jamii zetu za kiafrika zilivyofundisha miaka kadhaa iliyopita! Hili laweza kuwa kweli, lakini bahati nayo lazima ijengewa mazingira ya kukua. Kanisa linakubaliana na ukweli kuwa wazazi wawe na watoto wanaoweza kuwatunza hata hivyo nia hii njema iheshimu mpango wa asili uliowekwa katika maumbile.
Tunatambua jitihada nyingi zinazofanywa na serikali zetu kuwahamasisha wana-familia watambue umuhimu wa kuzaa watoto kulingana na uwezo wao wa kuwahudumia hasa katika nyakati zetu zinazokabiliwa na myumbo wa kiuchumi. Hata hivyo jitihada hizi hazipaswi kuwachangulia wazazi idadi ya watoto. Pia sio sahihi kuwalazimisha kutumia njia za kisayansi kupanga uzazi zinazopingana na imani zao.
Licha ya Kanisa kukataa mpango wa uzazi kwa njia ya kisayansi lakini ukweli ni kuwa takwimu inaonyesha ongezeko kubwa sana la vidonge, sindano na njia nyingine za kupanga uzazi kwa njia ya kisayansi katika ulimwengu mzima. Na zaidi sana nyumbani kwetu Afrika, ambapo wakati mwingine tunalazimishwa kukubali njia hizo kwa kisingizio cha kupatiwa misaada. Misaada tunaihitaji, lakini, iheshimu utu wetu na isitufanye kutenda dhambi na kwenda kinyume cha maadili na maumbile ya binadamu.
Lakini pia liko kundi dogo la watu wanaojikuta wamechangua kupanga uzazi kwa njia za kisayansi kwani hawajui kutumia duara la asili, yaani mpango wa uzazi kwa njia ya asili. Kanisa linalazimika kuwafundisha hawa. Ni vizuri katika vituo vya mafundisho ya ndoa kuwa na wataalamu wakuwaandaa wanandoa wetu tusiishie kwenye mafundisho ya kitaalimungu, tukasahau mpango wa uzazi kwa njia ya asili na mambo mengine ambayo ni muhimu sana katika kutunza na kukoleza utakatifu wa maisha ya wanandoa.
Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Raphel Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi ya Ndoa na Familia, chuo kikuu cha kipapa Laterano- Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.