Ndugu msikiliza wa Radio Vatican, baada ya kusema kwa kirefu kuhusu uzazi kwa njia
ya asili nakualika leo tugeukie upande mwingine tuwatazame wanandoa wasiojaliwa zawadi
ya watoto. Tamaa au hamu ya kuwa na mtoto au watoto kwa wanandoa ni matokeo ya upendo
kati yao. Ni matokeo ya ahadi na matumaini wanayokuwa nayo wanandoa ya kujenga
familia ambayo hutajirishwa na ujio wa mtoto au watoto. Katika vipindi vichache vijavyo
tutazitazama jitihada za wanandoa kutafuta mtoto/watoto hasa pale ugumba unapodhihirika
kuwa bayana. Hamu ya kuwa na mtoto sio tu kwa ajili ya tamaa binafsi bali ni nafasi
ya kupokea mtu mwingine, atakayeshiriki baadaye ya maisha pamoja na wazazi wake. Zawadi
ya mtoto/watoto ni baraka toka kwa Mungu (Mwanzo 4:1) kwa wazazi. Naomba ndugu msiklizaji
naomba turejee tena katika fikra za mwafrika kuhusu mzao. Lengo kuu la ndoa ni kuzaa
mtoto au watoto hivyo kwa mwafrika maana ya ndoa hutoweka endapo hakuna mzao. John
Mbiti mwandishi mashuhuri kutoka Afrika anasema “Anayekufa bila mzao amezima moto
wa maisha kwani hana wa kumkumbuka au kumtolea ubani.” Kukosa uzao barani Afrika kuliongeza
uke wenza na mahusiano mengi ya kimapenzi nje ya ndoa. Matokeo yake ni ongezeko
la magonjwa na vifo kutokana na baadhi ya wanandoa kukosa uaminifu kwa wenzi wao wa
ndoa kwa lengo la kutafuta mtoto kwa udi na uvumba. Hapa inabidi pia kukumbuka athari
za nyumba ndogo katika mshikamano na mapenzi ya dhati ndani ya familia, kwani Yesu
anasema huwezi kuwatumikia Mabwana wawili! Leo hii maendeleo ya sayansi na teknolojia
yamekuwa msaada mkubwa katika hili kwani wana-ndoa huweza kusaidiwa kupata mzao. Kwani
matatizo mengine ya uzazi yanahitaji tiba ya kawaida ambayo haitenganishi tendo la
ndoa na uzazi. Kwa kawaida wanandoa wanapokamilisha ndoa yao hutegemea mzao na
mara mtoto asipokuja mahangaiko huwajia. Jitihada zao huwasukuma kwenda kumwona daktari
ambaye naye hufanya vipimo na kuona jinsi ya kuwasaidia. Wakati mwingine jitihada
za wazazi huleta matunda mazuri wanaposaidia kupata uzao katika njia ya kawaida. Wakati
mwingi hufikia mahali pa kuhuzunisha wanapoambiwa kwa uhakika kuwa sio rahisi kupata
mtoto kwa njia ya kawaida na huku wakiendelea kudumisha uaminifu wa muungano wa kindoa
kati yao. Hiki ni kipindi kigumu sana kwa wanandoa kwani matumaini waliokuwa nayo
ya kujenga mji wenye furaha pamoja na zawadi ya watoto wao hutoweka. Kweli hapa isipotumika
busara ya kichungaji hata ndoa iliyo na tabia ya umoja usiogawanyika huingia hatarini.
Na wakati mwingine huingia katika tamaa ya kutafuta mtoto hata kwa njia ya kumtengeneza
katika maabara kwa ushirikiano na daktari ambalo tutalisema katika kipindi kijacho,
jambo ambalo lina hatari kubwa. Wakati mwingine, wanandoa kama hawa wanaweza kujikuta
wamejiingiza katika vitendo vya kishirikina. Wanandoa wasipokuwa makini kwa jambo
hili wanaweza kufilisika na hatimaye ndoa yao kubomoka kwa kuendekeza ushauri wa waganga
wa kienyeji. Ni vyema ikiwa kama wanandoa watapata ushauri wa kina kutoka kwa wataalam
wa masuala haya. Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Raphel Mwanga, wa
Jimbo Katoliki la Same, Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa Laterano-
Roma.