Sinodi ya kawaida ya 13 ya Maaskofu kwa ajili ya Uinjilishaji Mpya yaanza Vatican
Mapema Jumatatu wajumbe wa Mkutano wa Sinodi ya Kawaida ya 13 ya Maaskofu, waliianza
ratiba ya sinodi hiyo, kama ilivyoandaliwa na Sekretariati kuu ya Sinodi. Askofu
Mkuu Nikola Eterovic, Katibu Mkuu wa Sinodi, ametaja idadi ya wajumbe katika sinodi
hiyo kwamba, Mababa wa Sinodi ni 262, waliotoka bara zote tano za dunia( Afrika 50,
Amerika 63, Asia 39, Ulaya 103 na saba kutoka Oceania). Pia kuna wawakilishi 13 kutoka
Makanisa ya Mashariki na wajumbe 114 kutoka Mabaraza ya Maaskofu na Shirikisho linalounganisha
wakuu wa Mashirika Katoliki, na wageni waalikwa kutoka makanisa na jumuiya zinazo
shirikiana kwa ukaribu na Kanisa Katoliki katika mada hii ya Uijilishaji duniani.
Pia kuna watalaam 45 na wahariri 49 wake kwa waume watakao kuwepo wakati wa maadhimisho
ya Sinodi hii. Na amerejea maneno ya Yesu" Nendeni basi mkawafanye watu wa mataifa
yote kuwa wanafunzi wangu , mkiwabatiza kwa jila la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu
. Wafundisheni kushika maagizo yote niliyowapeni . Nami nipo nanyi siku zote , mpaka
mwisho wa dahari Mt. 28:19-20, akisema, ni wito unaongoza Sinodi hii ya kawaida ya
XIII, katika kutafakari mada ya sinodi: Uinjilishaji mpya kwa ajili ya uenezaji wa
Imani ya Kikristo. Ni kuhusu utangazaji wa habari njema, iliyohubiriwa na mitume
na kudhaminishwa na Mama Kanisa, yaani: kumtangaza Kristo aliyekufa kwa ajili ya dhambi
za binadamu, kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu, kwamba alikufa na kuzikwa,
siku ya tatu akafufuka kwa utukufu na kujionyesha kwa Kefa na mitume wake kumi na
waili. Injili inayobaki kuwa ileile na haibadilishwi na utendaji wa binadamu wenye
kubadilika badilika katika maisha yake ya kidini, kitamaduni na mipangilio yake ya
kijamii, katika namna za kuliishi Neno hili la Wokovu linalohitajika kufikishwa kwa
kila binadamu. Na hivyo katika mkutano huu, Mababa wa Sinodi watachambua kwa
kina, haja ya kuwa na mbinu mpya za uinjilishaji kwa ajili ya kuifikisha habari hii
njema ya wokovu kwa kila binadamu. Na pia Mababa wa Sinodi watafanya takari hizo sambamba
na kutangazwa kwa mwaka wa Imani na maadhmisho ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili
wa Vatican na pia miaka 20 ya kuchapishwa kwa Kateksimu Katoliki. Askofu Mkuu
Nikola Eterovic,ameeleza na kuuweka mkutano huu katika neema za Roho Mtakatifu ili
kwamba, Mwaka wa Imani uweze kuwa na zawadi nyingi za kiroho kwa Kanisa la Mungu,
Mama wa Waamini. Na ametoa muhtasari wa Mkutano wa Sinodi hii kwamba kazi zake
zitafanyika chini ya vipengere vinne : 1. Uwasilishaji wa kazi zilizofanyika kati
ya mkutano ya Sinodi ya Kawaida ya XII na Mkutano wa XIII. Sinodi ya kawaida ya
XII, ilifanyika Oktoba 5-26 , 2008, juu ya: Neno la Mungu, katika Maisha na Utume
wa Kanisa. Mwisho wa Sinodi hiyo, Maaskofu waliunda sekretariat yenye wajumbe 15 kwa
ajili ya kutazama kwa makini yaliyojadiliwa katika sinodi hiyo . Kazi hiyo ilifanyika
na taarifa yake kutumwa kwa Maaskofu wote hapo tarehe 30 Mei 2009. 2. Kazi zilizofanyika
katika maandalizi ya Sinodi ya kawaida ya XIII, ambayo ni matokeo ya mtazamo mpana
wa mashauriano katika taratibu za utume wa kanisa duniani na katka kujali kazi za
kichungaji za Papa , Askofu wa Roma na Mchungaji mkuu wa Kanisa la Ulimwengu. Maandalizi
mwongozo kwa ajili ya Mkutano wa XIII wa Sinodi ya Kawaida, yalianza mara baada ya
Papa kutangaza mada ya majadiliano kabla ya kuchapishwa rasmi. 3. Kutazama shughuli
zilizofanywa na Sekretarit Kuu, tangu Octoba 2008 hadi leo, mabamo kwa ombi pa Papa
, Sekretariat iliandaa Mikutano ya sinodi mbili maalum , kwanza kwa ajili ya Afrika
tarehe 4-25 Oktoba 2009 , na pili kwa ajili ya Mashariki ya kati ya tarehe 10-24
Oktoba 2010. Na mwisho, Mababa wa Sinodi watajadili Yesu Kristo , Muinjilishaji
Mkuu wa kwanza , wakilenga Mada ya Sinodi XIII; Uinjilishaji Mpya kwa ajili ya Uenezaji
wa Imani ya Kikristu. Kama ilivyokuwa kwa mitume, katika chumba cha juu wakiwa na
Mama wa Yesu, mama wa Kanisa na nyota ya Uinjilshaji ,baada ya kushukiwa na Roho
Mtakatifu walitawanyika wote kwenda kuitangaza habari njema kwa watu wote.Hilo ndilo
lengo la sinodi hii. Na kazi zake zimedhaminishwa katika usimamizi wa Mtakatifu
Yohane wa Avila na Mtakatifu Hildegard wa Bingen , walimu wapya wa Kanisa, ili kazi
hii iwmeze kutoa matunda bora ya neno la Yesu Kristu , Mchungaji mwema" tena ninao
wanakondoo wengine ambao hawamo zizini humu. inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia
sauti yangu na kutakuwapo kundi moja na mchungaji mmoja (Yn.10:16).