2012-10-08 15:49:41

Padre Theodorus Johaness Slaat wa Jimbo Katoliki Mbeya afariki dunia!


Simanzi na majonzi makubwa yamemkumba Askofu Evarist Chengula(IMC) wa Jimbo Katoliki la Mbeya, mapadre,watawa wa kike na kiume pamoja na waamini wote baada ya kumpoteza aliyekuwa Katibu wa Askofu na mshauri wa Jimbo aliyefariki tarehe 4 Oktoba 2012 majira ya saa saba kasorobo nyumbani kwake uaskofuni.

Wingu la vilio na simanzi limetanda wakati mwili wa Paroko wa Kanisa la Roho Mtakatifu,Parokia ya Ruanda, Padre Theodorus Johannes Slaats kupokelewa tarehe 8 Oktoba, 2012 na mapadre,watawa na waumini wa Jimbo la Mbeya waliokuwepo kanisa la Ruanda kuupokea mwili wake kutoka katika chumba cha kuhifadhia miili ya marehemu katika Hospitali ya Meta Rufaa,Mbeya majira ya saa 9.00 mchana kwa ajili ya misa na mkesha hadi tarehe 9 Oktoba, 2012 anapokwenda kuhifadhiwa katika nyumba yake ya milele.

Akizungumzia wasifu wake,Paroko msaidizi wa Parokia ya Roho Mtakatifu,Padre Deus Tarimo alisema marehemu padre Slaats aliyefariki akiwa na umri wa miaka 82 alizaliwa huko Eindhoven,Uholanzi Novemba, 3 mwaka 1930 akiwa ni mtoto wa saba katika familia ya watoto 12 na kubatizwa siku hiyo hiyo katika Kanisa la Mt.Theresia Trudo huko Uholanzi.

Padre Tarimo alisema marehemu alipata sakramenti ya kipaimara mei,17,1939, elimu ya msingi katika shule ya Msingi ya Mt.Theresia mwaka 1937 hadi 1940 na baadaye alihamia katika shule ya msingi Jan Smitslaan mwaka 1940 hadi mwaka 1943 huko Eindhoven na baadaye kujiunga na seminari ndogo ya shirika la Roho Mtakatifu, Weert mwaka 1943 hadi 1950.

Alisema baadaye aliendelea na malezi ya Novisiati katika Shirika hilo huko Gennep Uholanzi mwaka 1950 na kuweka nadhiri zake za kwanza Sept,7,1951 hadi mwaka 1952 alifanya masomo ya falsafa katika seminari kuu ya Shirika hilo huko Gemert,Uholanzi, masomo ya Taalilimungu katika chuo kikuu cha Gregoriana, Roma, Italia (1953-1957), nadhiri za daima(1954) huko Gemert, Uholanzi, daraja takatifu la ushemasi katika kanisa la Mt. Marcelli, Roma, Italia (1956).

Padre Tarimo alisema padre Slaats alipata daraja takatifu la upadre mwaka 1956 ambapo mwaka 1957 alitumwa kufanyakazi za umisionari nchini Tanzania na utume wake ulianzia Parokia ya Kisanga,jimbo Katoliki la Morogoro, mwaka 1958 alihudumu Parokia ya Matombo Morogoro na mwaka 1962 hadi 1964 alikuwa mratibu Taaluma na mwalimu katika seminari kuu ya Mt.Thomas, Morogoro huku akifundisha dini katika chuo cha ualimu kigurunyembe,Sekondari ya Mzumbe na Chuo cha Marian kwa sasa ni Sekondari ya Kilakala.

Alisema marehemu Padre Slaats alihudumu kama Mkurugenzi wa Idara ya Katekesi na afya Jimbo Katoliki la Morogoro,mwaka 1971 aliombwa na Mhashamu Askofu James Sangu wa Jimbo Katoliki la Mbeya kufanyakazi ya Ukatibu na Paroko wa Parokia ya Mwanjelwa hadi mwaka 1983.

Enzi za uhai wake Padre Slaats amewahi kuwa Mkuu wa chuo cha ufundi cha Ruanda (1985-1996), mwaka 1997 baada ya kusimikwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Mbeya, Askofu Evarist Chengula, aliteuliwa kuendelea na kazi ya Ukatibu na chancela wa Jimbo na baadaye aliomba kuanzisha Parokia mpya ya Ruanda ambapo Askofu Chengula alimsimika kuwa Paroko mwaka 2003.

Alisema Padre Slaats aligundulika kuwa na ugonjwa wa Saratani kunako mwaka 2004 na kwa nyakati tofauti alikuwa akipata matibabu katika Hospitali mbalimbali ndani na nje ya Nchi na lakini aliendelea kujitoa na kuchapa kazi katika nafasi zote hadi alipokwenda nchini Uholanzi kwa matibabu mwezi januari,mwaka huu na kurudi mwezi juni na afya yake iliendelea kudhoofika huku akihudumiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.









All the contents on this site are copyrighted ©.