2012-10-08 09:48:51

Jitokezeni kutoa maoni yenu kuhusu mchakato wa Katiba Mpya ya Tanzania


Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, linaendelea kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitokeza kwa wingi ili kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Wito huo umetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza. RealAudioMP3

Kati ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni kuangalia pia ukubwa wa Serikali, kwa kuangalia zaidi: tija, ufanisi na gharama za uendeshaji wa Serikali ikizingatiwa pia masuala ya uchumi. Ni jukumu la Katiba kuanisha mambo haya.

Kuna haja pia ya kuangalia nafasi za ubunge wa kuteuliwa na viti maalum na kwamba, wananchi wawe na dhamana kikatiba ya kuwawajibisha wabunge wao. Madaraka ya Rais kuhusu uteuzi wa viongozi wa juu yana wigo mpana mno unaoingilia mihimili mingine ya dola. Madaraka haya yanaweza kutumiwa vibaya na uwajibikaji wa viongozi hao walioteuliwa ukawa hafifu. Kuna haja kwa Katiba Mpya ya Tanzania kupunguza madaraka haya au kuweka udhibiti wake kisheria. Vigezo viwe wazi na uwamuzi ufikiwe kwa njia shirikishi.

Kuna haja ya kuwa na Tume huru ya uchaguzi na tume nyingine ili kuepusha hali ya wananchi kukosa imani na tume hizi na hivyo kuendelea kuibua malalamiko kwa Serikali. Uundwaji wa Tume ufanyike kwa uwazi na kwa kutumia njia shirikishi.

Serikali haina dini ndiyo nguzo ya umoja na amani ya nchi ya Tanzania. Uhuru wa kuabudu unapaswa kuheshimiwa na kulindwa. Kuna haja ya kuwa makini katika suala hili kwani mahali ambapo umetumika vibaya, umekuwa ni chanzo cha mtikisiko wa katika familia; chanzo cha kukashifu dini nyingine, uharibifu wa mali za watu pamoja na kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi.

Msukumo wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi ndani ya Mfumo wa mahakama za nchi siyo haki kwa hiyo isiwemo katika Katiba kwa kuwa ni mambo ya kidini na huenda ikawa ni njia ya kuipeleka Tanzania katika ukiukwaji wa dhana ya kuwa Serikali haina dini.

Kuhusu maoni ya Muungano: wananchi watoe maoni yao kwa kuangalia sababu zilizopelekea Waasisi wa Muungano kuuanzisha. Watu waangalie pia faida na hasara za Muungano. Wazo la Muungano wenye Serikali tatu ni hoja inayoweza kutolewa maoni, ukiangalia Katiba ya sasa ya Zanzibar.








All the contents on this site are copyrighted ©.