Angalieni jinsi ambavyo nguvu ya upendo wa Mungu inavyotenda muujiza katika maisha
ya binadamu!
Mwaka wa Imani unaotarajiwa kufunguliwa rasmi na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, hapo tarehe 11 Oktoba, 2012 ni changamoto ya kumwilisha imani katika uhalisia
wa maisha. Kifuatacho ni kisa kinachosimuliwa na mwamini mmoja aliyeonja upendo wa
Mungu katika maisha yake, akajitahidi kuumwilisha, ili kuonesha jinsi ambavyo nguvu
ya upendo wa Mungu inavyoweza kutenda muujiza hata leo hii: Soma kwa umakini mkubwa!
Ni
siku nyingi kidogo, mwaka 1979, lakini ni tukio ambalo liliniuma sana. Ilikuwa vigumu
sana kulisahau na lilinifanya nijiulize, inakuwaje Mungu anakuwa mkatili kiasi kile.
Lakini bila shaka ilikuwa ni wakati ule wa ufahamu mdogo. Hivi sasa ninafahamu mengi
na hasa baada ya kujifunza maarifa haya ya utambuzi.
Ilikuwa ni mwaka 1979
nikiwa nasafiri kutokea Dar es salaam kwenda Arusha. Sijui ilikuwaje, lakini ilitokea.
Tuliondoka Dar es salaam saa 12.30 jioni. Wakati ule mabasi yalikuwa yakisafiri jioni
na usiku, sio kama siku hizi.
Nilikuwa ninakwenda Arusha kwenye usaili
kwa ajili ya ajira, nikiwa ndio kwanza nimemaliza kidato cha nne. Niliajiriwa moja
kwa moja serikalini, kwani siku zile ajira zilikuwa ni za kumwaga. Hata hivyo sikuridhishwa
na kazi niliyokuwa nafanya, hivyo niliomba kazi kwenye kampuni moja kule Arusha na
niliitwa kwa usaili.
Tulifika mji unaoitwa Korogwe ambao wakati ule ulikuwa
ndio mji maarufu kwa hoteli zake katika barabara yote ya Segera hadi Moshi na Arusha.
Tulipofika Korogwe basi letu lilisimama kwa ajili ya abiria kupata chakula. Niliingia
kwenye hoteli moja ambayo nakumbuka hadi leo kwamba ilikuwa ikiitwa Bamboo. Niliagiza
chakula na kula haraka kutokana na muda mfupi wa kula uliotolewa na wenye basi la
TTBS ambalo ndilo nililosafiri nalo.
Wakati wa kulipa ndipo niliposhangaa
na kuogopa. Niliingiza mkono mifukoni na kukuta kwamba sikuwa na hela. Nilianza kubabaika
na mwenye hoteli alisema hawezi kukubali ujinga huo, "Abiria wengine wahuni bwana,
anakula na kujifanya kaibiwa, ukikubaliana nao kila siku hasara tu" Mwenye hoteli
alisema kwa kudhamiria hasa.
Kulizuka zogo kubwa, huku mwenye hoteli akisema
ni lazima anipeleke polisi. Ni kweli alimtuma mmoja wa watumishi wake kwenda kituo
cha polisi ili nishughulikiwe…… Hapo Hotelini kulikuwa na bwana mmoja aliyekuwa amekaa
pembeni na mkewe na watoto wao wakila. Yule bwana alipoona vile alimtuma mhudumu mmoja
aniite. Niliondoka pale kaunta nilipokuwa nabembeleza na kuja kwa yule bwana.
Alikuwa
ni kijana mtu mzima kidogo, mwenye miaka kama 50 hivi. Nilimsalimia na aliitikia,
nilimsalimia mkewe pia. Yule bwana aliniuliza kisa cha vurugu ile na nilimsimulia.
Aliniuliza sasa huko Arusha ningeishi vipi wakati wa usaili wakati nimeibiwa fedha
zote na ningerudi vipi Dar. Nilimwambia nilikuwa napanga namna ya kurudi Dar, kama
huko polisi ningeaminika.
Kama mzaha vile yule bwana aliniambia kuwa angenipa
fedha za kutumia huko Arusha na nikirudi Dar nimrudishie fedha zake. Nakumbuka alinipa
shilingi 90 kwa ahadi kwamba nikirudi Dar nimpelekee fedha zake ofisini kwake. Alinielekeza
ofisini kwake, mtaa wa Nkuruma na kuniambia kuwa ameamua kunisaidia kwa sababu kila
binadamu anahitaji msaada wa mwingine na maisha haya ni mzunguko.
Nilimshukuru
na kuondoka kukimbilia basini. Basi lilikuwa linanisubiri mimi tu. Nilipanda ndani
ya basi na abiria wengine walinipa pole. Tuliondoka Korogwe, lakini haikuchukua muda
basi letu lilipata tatizo la pancha ya gurudumu moja la mbele. Ilibidi tuegeshe pembeni
ili litengenezwe. Baada ya matengenezo, tuliondoka kuendelea na safari yetu.
Karibu
na mji wa Same kwenye saa saba usiku, basi letu lilisimama ghafla. Abiria walisimama
ndani ya basi na kulizuka aina ya kusukumana. Huko nje kulikuwa na ajali. Abiria tulishuka
haraka na wengine huko chini walishaanza kupiga mayowe, hasa wanawake. Niliposhuka
niliona gari ndogo nyeusi ikiwa imebondeka sana na hapo kando kulikuwa na maiti wawili.
Nilijua
ni maiti kwa sababu walikuwa wamefunikwa gubigubi. Halafu kulikuwa na katoto kalikokuwa
kanalia sana kakiwa kamefungwa kanga kichwani. Tumwahishe huyu mtoto hapo Same hospitali
ameumia, ingawa sio sana. Nilikatazama kale katoto ka kiume kenye umri wa miaka kama
mitatu. alikuwa ameumia kwenye paji la uso, lakini kalikuwa hai. Bila shaka wale walikuwa
ni wazazi wake, kalikuwa yatima tayari. Machozi yalinitoka.
Baada ya kupata
msaada na askari wa usalama barabarani kuchukua maiti wale tulipanda basini kuendelea
na safari yetu. Kale katoto kalichukuliwa na jamaa fulani waliokuwa na Land Rover
ya serikali kukimbizwa hospitalini. Ndani ya Basi mazungumzo yalikuwa ni kuhusu ajali
ile tu, hadi tunafika Arusha. Tulichelewa sana kufika Arusha kwani tulifika kwenye
saa tano asubuhi, badala ya saa mbili.
Nililala kwenye hoteli rahisi na kufanya
usaili kesho yake. Ni hiyo kesho, baada ya usaili niliponunua gazeti ambapo nilipata
mshtuko mkubwa ajabu. Kumbe wale watu wawili waliokufa kwenye ajali ile ya Same walikuwa
ni yule bwana aliyenisaidia hela na mkewe. Yule mtoto wao ndiye aliyeokoka. Niligundua
hilo baada ya kusoma jina lake na jina la kampuni aliponiambia nimpelekee fedha zake
nikirudi Dar, pamoja na picha yake, mke na mtoto. Nililia sana, kama mtoto.
Nillishindwa
kujua ni kwa nini afe. Nilijiuliza ni nani sasa angemlea mtoto yule? Yalikuwa ni maswali
yasiyo na majibu na pengine maswali ya kijinga pia. Nilijua kwamba nilikuwa na
deni, deni la shilingi tisini. Kwa wakati ule shilingi tisini zilikuwa ni sawa na
shilingi laki moja za sasa. Kwa mara ya kwanza sasa nilijiuliza ni kwa nini marehemu
yule aliniamini nakuamua kunipa fedha zile. Sikupata jibu.
Nilikata kipande
kile cha gazeti la kingereza kilichokuwa na habari ile. Nilichukuwa kipande hicho
na kukiweka kwenye Diary yangu. Deni, Ningelipa vipi deni la watu? Nilijikuta nikipiga
magoti na kuomba mungu anipe uwezo wa kuja kulilipa deni la mtu yule mwema kwa njia
yoyote. 'Mungu naomba uje uniwezeshe kulilipa deni la marehemu kwa sura na namna ujuavyo
wewe. Nataka kulilipa deni hili ili nami niwe nimemfanyia jambo marehemu,' niliomba.
Nilirejea Dar siku hiyo hiyo.
Kwa sababu ya mambo mengi na hasa baada ya matokeo
ya usaili ule kuwa mbaya kwangu, nilijikuta nikiwa na mambo mengi na kusahau haraka
sana kuhusu mtu yule aliyenisaidia mbaye ni marehemu. Nilifanikiwa hata hivyo kupata
nafasi ya kusoma Chuo cha Saruji na baadae chuo cha ufundi na hatimaye nilibahatika
kwenda nchini Uingereza. Mwaka 1991 nilianza shughuli zangu.
Ilikuwa ni mwaka
1995 nikiwa ofisini kwangu pale lilipokuwa jengo Nasaco ambalo liliungua mwaka 1996,
ambapo lilijengwa upya na kubadilishwa jina na kuitwa Water Front. Nikiwa nafanya
kazi zangu niliambiwa na sekratari wangu kwamba kulikuwa na kijana aliyekuwa anataka
kuniona. Nilimuuliza ni kijana gani, akasema hamjui. Nilimwambia amruhusu aingie.
Kijana huyo aliingia ofisini. Alikuwa ni kijana mdogo wa umri miaka kama 17 au 18
hivi, mweupe mrefu kidogo. Alikuwa amevaa bora liende, yaani hovyohovyo huku afya
yake ikiwa hairidhishi sana.
Nilimkaribisha ilimradi basi tu, kwani niliona
atanipotezea bure muda wangu. Ni lazima niwe mkweli kwamba sikuwa mtu mwenye huruma
sana na nilikuwa naamini sana katika watu wenye pesa au majina. Nilimuuliza, “nikusaidie
nini kijana na ukifanya haraka nitashukuru maana nina kikao baada ya muda mfupi”.
Nilisema na sikuwa na kikao chochote , lakini nilitaka tu aondoke haraka.
“Samahani
mzee, nilikuwa na shida…..nimefukuzwa shule na sina tena mtu wakunisaidia kwa sababu
…..nime….niko ….kidato cha pili na hivyo tu natafuta tu kama atatokea mtu...Nilimkatisha.
“Sikiliza kijana. Kama huna jambo lingine la kusema, ni bora ukaniacha nifanye kazi.
Hivi unafikiri kama nikiamua kumsaidia kila mtu aliyefukuzwa shule si nitarudi kwetu
kwa miguu! Nenda Wizara ya Elimu waambie……Kwanza wazazi wako wanafanya kitu gani,
kwa nini washindwe …..Kwa nini walikupeleka shule ya kulipia kama hawana uwezo, wanataka
sifa?”
“Hapana wazazi wangu walikufa na ninasoma shule ya serikali. Nimekosa
mahitaji ya msingi na nauli ya kwendea shule. Nasoma shule ya Kwiro, Morogoro. Shangazi
ndiye anayenisomesha, naye ana kansa na hivi sasa hata kazi hafanyi….,” Alianza kulia.
Huruma fulani ilinijia na nilijiambia, kama ni nauli tu na matumizi, kwa nini nisiwe
mwema, angalau kwa mara moja tu. “Baba na mama walifariki lini?” Niliuliza nikijua
kwamba, watakuwa wamekufa kwa ukimwi, maana kipindi kile ndipo fasheni ya ukimwi ilipoanza,
ambapo kila anayekufa huhesabiwa kwamba kafa kwa ukimwi.
“Walikufa kwa ajali
nilipokuwa mdogo sana, nilipokuwa na miaka mitatu. Ndio shangazi yangu akanichukua
na kunilea hadi sasa anakufa kwa kansa.” Yule kijana alilia zaidi. Naomba nikwambie
wewe msomaji unayesoma hapa kwamba, kuna nguvu fulani na sasa naamini kwamba ziko
nyingi ambazo huwa zinaongoza maisha yetu bila sisi kujua.
Kitu fulani kilinipiga
akilini paaa! Nilijikuta namuuliza yuel kijana. “Kwa nini umeamua kuja kwangu, ni
nani alikuelekeza hapa na wazazi wako walikufa mwaka gani na wapi? Yule kijana alisema,
“Nimeona nijaribu tu kwa mtu yeyote ambaye anaweza kunisaidia, na ndio nimejikuta
nikiingia hapa, sijui... Sikutumwa na mtu. Wazazi wangu walikufa mwaka 1979 huko Same
na mimi wanasema nilikuwa kwenye ajali, nikaokoka. Niliumia tu hapa.” Alishika kwenye
kovu juu ya paji lake la uso.
Nilihisi kitu fulani kikipanda tumboni na kuja
kifuani halafi niliona kama vile nimebanwa na kushindwa kupumua. “Baba yako alikuwa
anaitwa nani?” “Alikuwa anaitwa Siame….Cosmas Siame….” Niliinuka ghafla hadi yule
kijana alishtuka . Nilikwenda kwenye kabati langu mle ofisini na kuchakura kwenye
droo moja na kutoka na diary. Mikono ikinitetemeka, nilitoa kipande cha gazeti ndani
ya diary hiyo, nilichokuwa nimekihifadhi.
“Ndio alikuwa anaitwa Cosmas Siame.
Huyu ni mtoto wake, ni yule mtoto aliyenusurika.” Nilinong’ona. Nilijikuta nikipiga
magoti na kusali. “Mungu, wewe ni mweza na hakuna kinachokushinda. Nimeamini baba
kwamba kila jema tunalofanya ni akiba yetu ya kesho na kesho hiyo huanzia hapa duniani.”
Halafu nillinyamaza na kulia sana. Nililia kwa furaha na ugunduzi wa nguvu zinazomgusa
binadamu kwa kila analofanya.
Nilisimama nikiwa nimesawajika kabisa. Nilihisi
kuwa mtu mwingine kabisa. Nilimfuata yule kijana na kumkumbatia huku nikiwa bado ninalia.
“Mimi ni baba yako mdogo, ndiye nitakyekulea sasa. Ni zamu yangu sasa kukulea hadi
mwisho” Naye alilia bila kujua sababu na alikuwa amechanganyikiwa kabisa. Nilirudi
kwenye kiti na kumsimulia kilichotokea miaka 17 iliyopita.
Tuliondoka hapo
na kwenda kumwona shangazi yake Ubungo, eneo la maziwa ambako alikuwa amepanga chumba.
Kutokana na hali yake nilimhamishia kwangu, baada ya kumsimulia kilichotokea. Huyo
dada yake Cosmas alifurahi sana hadi akashindwa kuzungumza kwa saa nzima. Alifariki
hata hivyo mwaka mmoja baadaye, lakini akiwa ameridhika sana.
Kijana Siame
alisoma na kumaliza Chuo Kikuu na hivi sasa yuko nchini Australia anakofanya kazi.
Ukweli ni kwamba ni mwanangu kabisa sasa. Naamini huko waliko Mbinguni wazazi wake
wanafurahia kile walichokipanda miaka mingi sana nyuma. Lakini nami najiuliza bado.
Ilikuwaje Cosmas akanipa msaada ule? Halafu najiuliza ni kitu gani kilimvuta mwanae
Siame hadi ofisini kwangu akizipita ofisi nyingine zote? Nataka nikuambie, usiwe mbishi
sana bila sababu, kuna nguvu za ziada zinazoongoza matokeo maishani mwetu... NGUVU
HIZO NI UPENDO WA MUNGU!