2012-10-04 09:06:38

Tuheshimu alama Takatifu za kidini - Patriaki Bartholew I


Viongozi wa kidini wanaendelea kutoa wito kwa wanasiasa na wanaharakati wa mapinduzi , kuheshimu tofauti za kidini na kusitisha ghasia na fujo.
Hivi karibuni, Patriaki wa Kiekumene wa Constatinople, Bartolomeo 1, akizungumza na shirika la habari la Sir, alijiunga na viongozi wengine wa kidini kukemea ghasia na fujo za umwagaji wa damu na uharibifu wa mali. Katika maelezo yake alionyesha hofu na wasiwasi wa kina , juu ya matokeo ya ghasia hizi kwamba hakuna faida wala jingine, isipokuwa kudhoofisha maisha na maendeleo ya watu, na hasa watu wanyonge na maskini.
Aliendelea kuchambua kwamba, kipindi hiki, kimekuwa ni kipindi cha fujo, vurugu na ghasia zinazofanywa kwa kisingizio cha kuimarisha imani . Lakini katika ukweli wake, ni kukosa kuheshimu dini na tofauti za kidini. Ni utendaji unaoonyesha utomvu wa nidhamu na ustaraabu, ni utendaji uliogubikwa katika ghadhabu, zinazofanyika kwa kisingizio cha kutunza sheria za dini au kulinda imani. Na kumbe ni kuhatarisha maisha na imani, mtendaji akijijengea mazingira ya kisasi, hasira, chuki na kukosa matumaini , mambo yanayoharibu tunu za mshikamano wa ubinadamu, asili aliyoumbwa nayo binadamu tangu mwanzo wa kuumbwa kwa dunia.
Patriaki Bartolomeo, kwa muono huo, ametoa ombi kwa watu wote, na hasa wanaohusika na ghasia na fujo kwa visingizio vya kisiasa na dini, wafanye kila linalowezekana, kwa yale yanayowakera kupata muafaka kwa njia za utuliVu , amani na kuvumiliana. Wakumbuke kwamba kila binadamu anayezaliwa, anao uhuru kamili wa kuishi duniani kwa amani na utulivu. Kila mmoja anapaswa kufuata dhamiri na dini kwa uhuru kamili , na bila ya kubugudhi wala kumshurutisha mwingine afUate imani yake.
Patriaki Bartolomew 1, pia ametoa wito wa kuheshimu alama za Imani na dini. Amesema, alama hizo ni lugha nyingine ya kueleza na kufikiri. Alama za kidini, huwakilisha ishara za nje ambazo huwaunganisha watu kimawazo na maadili ya ndani .
Hivyo pale alama hizi zinapoangamizwa kwa makusudi, wanao ziamini huumizwa nyoyo zao. Amehimiza watu kufanya mabadiliko makubwa kifikira, kitabia na mazoea. Mabadiliko ya kukataa uovu, kudharau wengine na kujiona wao ni bora zaidi. Ameasa dini ya kweli hukemea tabia za mtu kujitukuza na kudharau mwingine, kwa kuwa , mbele ya macho ya Mungu, hakuna aliye bora zaidi ya mwingine. Kwa maana hiyo tunapaswa kuishi kwa kuvumiliana na kuheshimu tofauti zetu. Na kwamba masuala ya imani ni uchaguzi huru wa mtu , maana ni mambo ya kiroho na si mambo ya dunia hii







All the contents on this site are copyrighted ©.