2012-09-24 08:18:02

Mwili wa Kardinali Laurean Rugambwa kuzikwa upya Bukoba


Mwili wa Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa , utazikwa rasmi katika Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Bukoba octoba 6 mwaka huu, wakati huo kesho yake th 7oktoba kufanyika sherehe za kutabaruku kanisa katoliki baada ya kumalizika ukarabati mkubwa uliochukua takribani miaka 17.
Aidha sherehe za kutabaruku kanisa katoliki la Jimbo la Bukoba linaenda sambamba na sherehe za kuadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwa kiongozi huyo aliyekuwa Kardinali wa kwanza nchini Tanzania na afrika kwa ujumla. Hili kuelewa zaidi juu ya Mwadhama Kardinali Rugambwa , ufasaha wa maisha yake, moyo wake, kazi zake za kitume, upendo wake na mambo mengi turudi nyuma katika makala iliyoandikwa na aliyekuwa wakati ule Padre Method Kilaini kwa magazeti mbalimbali mara baada ya kifo cha mwadhama Desemba 1997. Padre Kilaini wakati huo alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Katika makala hii itatupatia kina cha kujua historia nzima ya huo mwadhama. Padre Methodius Kilaini sasa ni Askofu msaidizi wa Jimbo katoliki la Bukoba ambaye alitumwa Roma na Mwadhama mwaka 1968 kusomea Upadre. Na hata baadaye alikuwa karibu sana naye kiasi kwamba ndiye aliyemwachia kuwa msimamizi wa mirathi yake.
Naye Baba Kilaini aliandika makala hiyo kwamba; mwaka 1968 wakiwa Roma Kardinali Rugambwa alikuja kikazi Roma, ikawa bahati ya kumsindikiza mjini Roma na Vatikani. Kwa mara ya kwanza alielewa ukubwa wa kardinali na alipolinganisha na jinsi alivyotendewa pale ndipo alitambua unyenyekevu wake. Huko nyumbani kwao Bukoba na Tanzania kwa ujumla watu hawakujua wamwiteje ndipo wakatengeneza maneno ya 'Nyakutununta' kwa kihaya, na Mwadhama kwa kiswahili.
Kardinali katika Kanisa Katoliki lenye waumini zaidi ya bilioni moja, alikuwa ni mmoja wa watu bawaba au wa msingi 130 katika kanisa hilo. Kikanisa yeye alikuwa yuko juu ya maaskofu, maaskofu wakuu, balozi wa Baba mtakatifu na wengine. Kidiplomatia hupokelewa kama Mwana Mfalme. Yeye alikuwa anashiriki katika uchaguzi wa Baba Mtakatifu,hivyo (Rugambwa alishiriki kuwachagua Baba Watakatifu watatu).
Aliendelea kueleza kuwa anakumbuka mwaka 1992, Baba Mtakatifu Yohana Paulo II akiwapokea maaskofu wa Tanzania alimwita mwana wa kwanza wa kanisa la Afrika. Aliwaambia maaskofu kwamba anamheshimu sana kwa sababu alimtangulia kama Kardinali. Rugambwa alikuwa mjumbe katika kamati na tume mbali mbali huko Vatikani ikiwemo ile ya Liturujia na ile ya Uenezaji Injili.
Kama Kardinali alipewa kanisa lake la kudumu Roma, kanisa la zamani sana la Mtakatifu Fransisco wa Ripa. Mwaka 1992 akisherehekea miaka 40 ya Uaskofu aliweza kuwaalika maaskofu wa Tanzania katika kanisa ambako walipokelewa vizuri na waumini wake. Waumini hao walimpenda na kujivunia kuwa na kardinali wa kwanza wa Afrika kama kardinali wao wa pekee.
RUGAMBWA ALIKUWA HESHIMA YA WATU WEUSI
Baada ya kuteuliwa kuwa kardinali alipotembelea nchi za Ulaya na Marekani alipokelewa vizuri sana na heshima zote za kiserikali. Ikumbukwe kwamba wakati huu ulikuwa bado wakati wa ukoloni katika nchi karibu zote za Afrika. Kupitia kwake mtu mweusi aliheshimiwa na kukubalika kwa wote. Ulaya hasa Italia, Ujerumani, Uholanzi, Ubelgiji na Austria alipokelewa na viongozi wa juu wa serikali. Ujerumani alionana na Raisi, Waziri Mkuu na kuiongelea Bundestag ambalo ndilo bunge la Ujerumani. Hii ilikuwa heshima kubwa sana ambayo walikuwa hawapewi hata wakuu wa serikali.
Huko Marekani alihutubia katika vyuo vikuu vingi vilivyomtunuku shahada za juu za udaktari wa heshima. Alikutana na vingozi wa marekani weusi ambao walijionea sifa sana kwake. Katika yeye walijivuna kuwa weusi na kukumbuka kwamba wao ni watoto wa Afrika. Kwa mara ya kwanza wamarekani weusi walimwona mwafrika aliyepata cheo kikubwa kama hicho, hata na wazungu wa marekani ingawa waliwadharau watu weusi walimheshimu sana. Makardinali weupe wa Marekeni kama Kardinali Cushing, walimkaribisha majimboni kwao kwa heshima kubwa. Hivyo wote walimwona kama ishara ya uwezo wa mtu mweusi katika harakati zao za kupigania usawa huko marekani. Walianza kujihusisha na kanisa la Afrika.
RUGAMBWA ALIKUWA KIUNGO CHA UPATANISHI KWA WOTE.
Rugambwa alikuwa askofu wa tatu mwafrika na kardinali wa kwanza wa bara la Afrika. Maaskofu wa Afrika walimtambua na kumkubali kama kiongozi wao. Wakati wa Mtaguso Mkuu wa Vatikano II (1962-65) uliohudhuliwa na maaskofu zaidi ya 3,000 yeye alikuwa askofu mwafrika pekee aliyepewa fursa ya kuhutubia maaskofu wote kwa pamoja katika ukumbi mkuu katika miaka yote mitatu ya mkutano huo. Hata wazungu ni wachache sana waliopewa fursa hiyo.
Wakati wa mtaguso huo aliwaita pamoja maaskofu wote kutoka Afrika (wengi wao wakiwa wamisionari wazungu) na yeye akiwa mwenyekiti wao zilianza harakati za kuundwa umoja wa maaskofu wa Afrika, (SECAM). Vivyo hivyo Rugambwa alikuwa kiuongo cha kusaidia kuunda umoja wa maaskofu wa Afrika ya Mashariki, zikiwemo nchi za Eritrea, Ethiopia, Somalia, Sudan, Kenya, Uganda, Tanzania, Malawi na Zambia, (AMECEA). Mpaka alipofariki alikuwa bado baba mlezi wa umoja huo. Kwa sababu hiyo alikuwa mjumbe wa kudumu wa kamati tendaji, pamoja na kuwa vile vile baba mlezi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika ya Mashariki ambacho kiko nchini Kenya.
RUGAMBWA NA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA
Rugambwa alikuwa ni mmoja wa waasisi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na Askofu Mkuu Marantha akiwa askofu mwafrika pekee katika baraza hilo mwaka 1956. Yeye ndiye aliyewakaribisha maaskofu wengine waafrika katika baraza hilo na kuwaelekeza. Baada ya kuwa kardinali mwaka 1960 wengi wao aliwapa uaskofu au aliwasimika katika viti vyao vya uaskofu. Alijiona kama kiungo chao. Hakutaka hata mara moja kukosa vikao vya baraza hili ikijulikana kwamba kwa heshima alikuwa mwanachama wa kudumu katika kamati tendaji mpaka alipostaafu.
“ Askofu Mathias Joseph Isuja akitoa rambi rambi zake alisema 'Rugambwa alikuwa nguzo yetu na kiungo chetu. Kule kuwako kwake kulimfanya mtu kushika adabu. Kama mtu hakushika adabu alimwita na kumwambia neno moja tu na lilitosha.”
Kilaini anaendelea; Vile vile kama alivyoeleza askofu huyo hakuzungumza sana katika vikao vya baraza lakini ilipofika wakati, akaona kwamba maaskofu kidogo hawakubaliani alisema maneno machache na ndio ulikuwa mwisho wamabishano. Alipenda sana umoja wa maaskofu na alitaka wawe kitu kimoja. Mwaka 1967 alikuwa msitari wa mbele katika kuunganisha seminari kuu za Tanzania ili kuleta umoja. Yeye aliitoa Seminari yake ya Ntungamo iwe kwa ajili ya Baraza zima.
Maaskofu walimpenda na kumheshimu sana. Yeye vile vile aliwapenda sana. Mfano mmoja ni mwaka 1996 alipoona Askofu Castor Sekwa wa Shinyanga ameugua sana na ukawa muda mrefu bila kumwona, alifunga safari mpaka Shinyanga kumtia nguvu na kumpa moyo licha ya barabara mbaya ingawa yeye tayari alikuwa ameanza kuwa mnyonge kiafya. Alibaki naye zaidi ya wiki moja wakati wa pasaka.

Mwezi wa saba akiwa kitandani baada ya kutembelewa na maaskofu alimwambia Kilaini kuwa: 'Mwanangu najisikia vizuri nikiwaona maaskofu'. Kwa kawaida Mwadhama alikuwa hataniani sana lakini alipokuwa na maaskofu hasa kama Askofu Isuja wa Dodoma, Marehemu Askofu Sekwa wa Shinyanga, Amedeus aliyekuwa wa Moshi na wakati huu ni askofu wa Mwanza, hata na maaskofu kama Askofu Paul Ruzoka aliyekuwa wa kigoma na sasa Tabora na Marehemu Askofu Justin Samba aliyekuwa wa Musoma na wengine alitaniana nao sana hata kusahau kama ni yeye ambaye kikawaida alikuwa ni mtu mtulivu mwenye maneno machache. Alitafuta namna ya kuwafanya wacheke na kujisikia vizuri naye.

Miaka 100 ya kuzaliwa Hayati Kardinali RUGAMBWA
Makala ya Askofu Methodi Kilaini aliyoiandika baadaya ya kifo cha Kardinali Rugambwa Desemba 1997 inaendelea.
Hayati Rugambwa hakupenda ukabila. Askofu Mkuu Pengo akitoa buriani kwa aliyemwita, Baba yetu Rugambwa, aliongelea juu ya uwezo wake wa kuwa juu ya makabila na vikundi. Akiongelea juu ya kazi yake Dar es Salaam alisema aliweza kuwafanya waumini wa jiji wajisikie wenye kanisa la Dar es Salaam bila kujali walitoka wapi.
Aliwapata mapadre wa Dar es Salaam, masista wa Dar es Salaam na waumini wa Dar es Salaam. Kardinali kwao ni Bukoba na Bukoba aliipenda lakini hakupenda ukabila hata kidogo. Akiwa askofu wa Bukoba baada ya kumaliza nyumba yake ya kiaskofu, aliwaalika masista wa Kilimanjaro waje kumtunza na kuhudumia katika nyumba yake. Hivyo watawa waliokuwa karibu naye kumhudumia kwa miaka 34 ya uongozi wake wengi walikuwa ni wachagga.
Ni hao vile vile aliowaleta katika seminari kuu ya Ntungamo na siyo shirika lake la Bukoba. Alifanya juu chini kutuma wasichana katika shirika hilo la Kilimanjaro ili wapate upeo wa kitaifa. Kwa moyo huo alipokuja Dar es Salaam alikaribisha mashirika mbali mbali ya watawa kutoka sehemu zote za Tanzania na kuwaweka katika parokia mbali mbali ili kuwafanya watanzania wote wajisike nyumbani jijini.
RUGAMBWA NA UMOJA WA WAKRISTO NA UELEWANO NA WAISLAMU
Askofu mstaafu kwa sasa Elinaza Sendoro wa kanisa la Kiluteli Tanzania akitoa rambi rambi zake naye alimtaja Kardinari Rugambwa kama baba wa umoja wa makanisa Dar es Salaam. Pamoja na Askofu Sambano wa kanisa la Kianglikana walimkumbuka kama mwanzilishi wa umoja huo na mwenyekiti wake kwa miaka 8. Alihimiza ujenzi wa makanisa ya pamoja kama lile la hospitali ya Muhimbili. Wakati wa kuifungua aliomba waibariki kwa pamoja. Huu ni moyo alioukuza katika uongozi wake wote.
Kamachumu alikozaliwa Mwadhama Laureani Kardinali Rugambwa palikuwepo madhehebu matatu yaliyoshindana. Wakatoliki wakiwa na makao yao katika kilima cha Rutabo, Waluteli wakiwa Ndolage na Waislamu wakiwa wafanyabiashara tajiri Kamachumu mjini. Kwanza alijitahidi kuelewana na kutoa ugomvi kati ya wakristo na Waislamu.
Aliwaonyesha upendo wake kwa kuwafanya watambue kwamba analeta maendeleo, elimu na huduma kwa wote bila ubaguzi. Kwa hilo alifanikiwa kiasi kwamba Waislamu wenye siasa kali walimwita Sheik Mkuu wa Bukoba mkristo asiyebatizwa lakini yeye hakujali kwasababu ya uwezeo wake wa kuleta upendo na uelewano.
Kama baba wa Mtaguso Mkuu wa Vatikano II aliamini katika umoja wa wakristo. Alilelewa katika moyo wa Papa Yohana XXIII aliyesema kila wakati 'tafuteni kile kinachowaunganisha na si kile kinachowatenga' Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia Tanzania, Mchungaji Albert Mongi akituma rambi rambi za chama alikumbuka maneno ya Kardinali Rugambwa ' Jambo hili (maana yake ya kueneza pamoja Biblia kati ya wakatoliki na waprotestanti) halihitaji ushawishi. Ikiwa tutashindwa kushirikiana katika huduma ya kuwapa watu Biblia, basi tutakuwa hatuna la kutuunganisha'.
Rugambwa alitumia uwezo wake wote kuleta ushirikiano. Akiwa Bukoba alishirikiana kwa karibu na Askofu wa Kiluteli, Marehemu Josias Kibira. Kibira alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiluteli ulimwenguni, Kardinali alifanya mpango wakaenda pamoja kumsalimu Papa Paulo VI huko Roma.
Picha ya Kardinali Rugambwa na Askofu huyu wa Kiluteli, Kibira, ilipochapishwa katika gazeti na kalenda ya gazeti la jimbo la Rumuli, mmoja akiwa mkono wa kulia na mwingine wa kushoto wa Baba Mtakatifu Paulo VI, iliamsha uelewano na ushirikiano mkubwa kati ya madhehebu haya makubwa ya kikristo Bukoba.
Moyo wake wa ushirikiano uliendelea vizuri hivyo hata wakati wa sinodi ya Afrika, iliyofanyika Roma 1994, aliyekuwa mrithi wa marehemu Askofu Kibira, Askofu Mushemba sasa msaatafu alialikwa na Baba Mtakatifu Yohana Paulo II kuwakilisha kanisa la Kiluteli Afrika katika sinodi hiyo.
Hata baada ya kustaafu kama wakristu walikuwa na kitu chenye utata au walitaka kumwona Raisi wa Tanzania kwa pamoja kutatua tatizo fulani walimwomba awe kiongozi wao. Yeye alikuwa juu ya tofauti za kidhehebu au kikabila.
RUGAMBWA NI MTU MWENYE UPEO MKUU KATIKA KUELIMISHA WATU (USHUHUDA WA ASKOFU MSTAAFU NKALANGA)
Kilaini aliendelea katika mala yake ; Jioni baada ya mapokezi makubwa ya Mwili wa marehemu Rugambwa Mwanza, alipata fursa ya kuongea kwa faragha na Mhashamu Askofu Gervase Nkalanga, Askofu mstaafu wa Bukoba ambaye sasa yuko katika monastri ya wa benediktini wa Hanga. Nkalanga alikuwa parokia moja na Rugambwa alipotangazwa kuwa askofu, baada ya hapo alitumikia chini yake miaka 11, miaka sita kama katibu wa jimbo wa elimu na miaka mitano kama Askofu Msaidizi.
Kilaini alimuuliza swali moja kuwa Alimwonaje Mwadhama' alimwona uso wa Askofu Nkalanga ukingara kwa tabasamu na alisema: 'Mwadhama alikuwa na upeo mkubwa ajabu, hakukata tamaa katika shida'. Muda wote hasa baada ya kupewa jimbo jipya la Rutabo, likiwa fukara, mwadhama alimwambia kwamba kuna ufunguo mmoja tu kwa shida hizi zote, yaani kuwapa watu elimu na matatizo mengine wangeweza kuyatatua wao wenyewe.
Askofu Nkalanga aliendelea ; katika miaka kumi na moja aliyotumikia chini ya Mwadhama, ingawa jimbo lilikuwa fukara hakuna hata siku moja alimwendea kumwomba fedha kwa ajili ya elimu akamnyima. Nkalanga alisema kwamba hata mapadre wengine walipata hata kumchukia wakiuliza kwa nini alipata fedha kwa ajili ya shule na wengine hawakupata kwa ajili ya shughuli nyingine muhimu.
Upeo wake wa elimu Kwa Kardinali Rugambwa ulikuwa ni wa kumwelimisha mtu mzima, kijamii, kifamilia, na kitaifa. Kutimiza hilo alianza umoja wa 'St. Augustine Social Guild' katika umoja huu aliwaweka pamoja vijana na watu wazima wenye uwezo na kuwaendeleza kwa pamoja. Wale waliokuwa na akili zaidi aliwatuma sehemu mbali mbali kwa masomo ya juu hata Ulaya na Marekani. Wengi waliporudi walichukuliwa na serikali lakini aliendelea kuelimisha tu.
Kwa watu wa kawaida kijijini aliona kwamba hawawezi kuendelea kama hawajifunzi kuweka pesa zao na kupanga maendeleo yao. Akitumia Marehemu Padre Robert Rweyemamu ambaye baadaaye alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu, na Padre Peter Mutashobya, aliyewahi kuwa mhasibu wa jimbo la Bukoba, alianzisha chama cha kukopa, (Credit union) Kilipofanikiwa katika parokia moja ya Mwemage waliieneza katika jimbo zima na baadaye wakajaribu kulieneza kitaifa. Watu wengi waliinuka kwa huduma hii.
Alipenda kuwaelimisha viongozi akianzia na mapadre, watawa na walei. Ni kweli ni wengi katika makundi hayo matatu aliowaelimisha wanaosaidia taifa katika nyadhifa mbali mbali Askofu Nkalanga alisema kwamba mara nyingi ilikuwa vigumu kuelewa malengo yake kwa sababu yalionekana magumu na ya juu mno yasiyoweza kutekelezwa. Lakini mwadhama alisema kila mara kwamba itawezekana tu, na kama kwa mwujiza iliwezekana. Mwishoni wale aliofanyakazi nao walipata imani kubwa kwake na walitimiza kama Yesu alipowaambia wafuasi wake wawagawie umati wa watu elfu tano vipande vitano vya mikate na wakafanya.
Uhusiano wake na serikali ulikuwa mzuri kwa sababu yeye alichotaka kwao ni kwamba wampe fursa ya kufanya mema, kujenga hospitali, mashule na kupewa fursa za kutoa huduma kwa watu. Askofu Nkalanga aliendelea kwamba; serikali ilipoanza kuzungumzia juu ya kutaifisha shule za kanisa alimwuliza Kardinali kama angeendelea kujenga au kuacha , na kardinali alimjibu, 'endelee kujenga ili wapate cha kutaifisha, si shule zitaendelea kuelimisha watu' Kutaifisha haikuwa shida ya Kardinali mradi bado zinaendelea kulea watoto na vijana. Hii ndiyo sababu hata baada ya kutaifisha mashule bado aliendelea kuwa karibu a shule zilizotaifishwa.
RUGAMBWA NA UJENZI WA SEMINARI
Mwadhama kardinaliRugambwa aliamini kwamba uchungaji hauwezi kufanikiwa kama hakuna wachungaji wenye akili, ucha Mungu na elimu ya kutosha. Hivyo nguvu zake za kwanza zilikuwa kuwapata mapadre waliotayarishwa vizuri.
Seminari ndogo ya Rutabo:
Alipoteuliwa kuliongoza jimbo changa la Kagera ya chini ambalo baadaye lilitwa Rutabo alikuwa na mapadre 17 tu wote wa jimbo. Wakat huo kulikuwepo seminari ndogo ya Bunena na seminari ya sekondari ya Rubya kwa ajili ya jimbo la Bukoba. Mara alipewa idadi ya watoto ambao angeliweza kupeleka katika seminari hizo. Mara moja aliona umuhimu wa kufungua seminari yake walau ile ndogo. Mwaka 1958 alifungua seminari ndogo ya Rutabo iliyowapokea vijana kwa ajili ya darasa la tano. Seminari hiyo ipo hadi leo na imekwisha elimisha vijana wengi na kutoa mapadre wengi sana.
Seminari Kuu ya Ntungamo
Baada ya kuwa askofu wa Bukoba aliona umuhimu wa kuwa na Seminari Kuu badala ya kuwatuma mafrateli Uganda. Aliomba msaada na kujenga seminari Kuu ya Mtakatifu Antoni wa Padua pale Ntungamo nje kidogo ya Bukoba mjini. Seminari hii ilipokea mafrateli wa kwanza wa jimbo la Bukoba na Rulenge mwaka 1964. Mwaka 1967 maaskofu wa tanzania walipomuomba iwe sehemu ya seminari ya taifa alikubali na hadi leo ni Seminari Kuu ya Falsafa.
Seminari Kuu ya Segerea
Mwadhama Laureani Kardinali Rugambwa alipohamishiwa jimbo Kuu la dar es Salaam mwaka 1969, jambo la kwanza aliliotambua ni kuona changamoto za jiji ambazo zilihitaji mapadre ambao wamezoea kusuguana nazo. Aliona vile vile kwamba kuwa na seminari Kuu jijini kutaongeza chachu siyo tu kwa ajili ya jimbo Kuu la Dar es salaam bali kama kitovu cha nchi kutachangia katika kutatua changamoto za kitaifa. Aliomba pesa na kujenga seminari Kuu ya Segerea ambayo ni sehemu ya mfumo wa taifa ikiwa kwa ajili ya Tauhidi (Teologia). Sasa inaendelea kutoa matunda yake.
Seminari ya Visiga
Juhudi za mwisho katika kuanzisha seminari zilikuwa Dar es Salaam. Kwa miaka mingi alituma waseminari katika seminari ya Mtakatifu Petro, Morogoro lakini alivyosema hakupata mapadre wengi. Hapo aliazimia kuanza seminari ndogo ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam ambapo angewafundisha vijana katika mazingira watakayofanyia kazi.
Alijenga seminari hiyo Visiga, nje ya mji wa Dar es Salaam mkoa wa Pwani. Ilifunguliwa mwaka 1990 na alipostaafu mwaka 1992 vijana walikuwa katika kidato cha pili. Kilichomfurahisha sana ni pale Umoja wa Wanawake Wakatoliki wa Dar es Salaam ulipoipokea na kuikumbatia shule hiyo. Kabla hajafariki alipata habari kwamba imekuwa shule ya nne kitaifa katika mitihani ya kidato cha nne, hii ilikuwa ni faraja kubwa.
Katika majimbo yote matatu aliyoyaongoza, alitayarisha walimu wa seminari kwa kuwatuma mapadre kujifunza katika vyuo vikuu mbali mbali ndani na nje ya nchi.

MWADHAMA RUGAMBWA NA MAENDELEO YA ELIMU YA WANAWAKE
Makala ya baba kilaini inaendelea; Askofu Nkalanga alisema kwamba akiwa katibu wa jimbo wa elimu mwadhama alimwambia kwamba asielimishe wavulana tu bali hasa wasichana. Kwani wanawake ndio walimu wa binadamu. Alipopokea jimbo la Rutabo, wamisionari wote wa Afrika waume kwa wake waliondoka akabaki na mapadre na watawa wafrika.
Mpaka wakati huo watawa waafrika wa Mtakatifu Tereza wa Mtoto Yesu walikuwa hawajapata elimu ya kutosha kuendeleza elimu ya wanawake. Hapo ndipo alikwenda kuwatafuta masista wa Kanosa mwaka 1956 waje kusadia. Walipofika Mugana aliwapa jukumu moja nalo ni kuendeleza wanawake katika njia yote.
Chini ya mama yao aliyekuwa Riveta waligawana kazi. Sr. Josephina aliona watoto wana nguo zimechanika akaanza shule ya akina mama 300 akiwafundisha kushona kwa kutumia sindano, kitu kidogo lakini kilileta tofauti sana katika maisha ya watu, na baadaaye akaanza mambo mengine ya maendeleo ya akina mama, na mwishowe shule ya maarifa ya nyumbani ya kwanza Bukoba, na baadaye wakaanza vile vile shule ya kati ya wasichana,.Sr. Carolina akaanza na Sr. Victoria kliniki za akina mama ambayo sasa imekua na kuwa hospitali kubwa ya Mugana, shule ya wakunga wasaidizi na fani nyingine.
Alivyofanya hapo Mugana ndivyo alivyoendelea kutafuta watawa wenye moyo na ujuzi hasa kuwasaidia akina mama katika elimu, afya na maendeleo hadi alipostaaafu Dar es Salaam. Aliwatafuta masista wa Breda Uholanzi kufungua hospitali ya Rubya, sasa ni hospitali teule ya wilaya, Masista wa Familia takatifu kutoka Uholanzi kuanza shule ya msingi ya pekee Rumuli na shule ya kati Mwemage, Masista wa Mtakatifu Paulo kushika duka la vitabu la Mtakatifu Joseph Dar, wakamelitane - Changombe, Waivrea - Kawe, nk.
Kilaini aliendelea kuwa; anakumbuka alimsindikiza kwa masista wa Kamelitane na Waivrea alipokuwa anaomba, kila mara aliweza kujieleza vizuri sana na kuonyesha ulazima wa wao kuja kusaidia wanawake.
Katika kupigania elimu ya wanawake labda ya kukumbukwa kuliko zote ni ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Rugambwa. Wakati huo hata kiulimwengu haja ya kuwasaidia wanawake ilikuwa bado haijapata msisitizo. Kwa hilo Askofu Nkalanga alisema alipomwambia kwamba wajenge shule ya wasichana hadi kidato ch sita kidogo baada ya kuteuliwa kuwa kardinali, hakuamini masikio yake kuwa sababu hatukuwa na chochote.
Aliendelea kuwa; alikuwa akimwona kama nabii kwa sababu aliposema kitafanyika kitu kilifanyika hivyo aliamini tu. Kwanza kupata ardhi ilikuwa shida lakini hapo Mwadhama hakuogopa mtu awe nani hata wakubwa wengine wa serikali walipoweka vipingamizi alipigana tu. Hapa alitumia hadhi yake kwa watu ambao walimwuunga mkono. Kwa ajili ya ujenzi alikwenda Ujerumani; akisaidiwa na Misereor, alionana na bunge zima la nchi hiyo akiwemo, Raisi na viongozi wengine ambao wote aliwahubiri juu ya ulazima wa kumwelimisha msichana mama na mwalimu wa kesho.
Kote huko hakuomba kitu kingine ila hicho tu. Walimwamini na kumpa fedha za kujenga shule nzuri sana yenye kupendeza. Ilipokuwa tayari serikali ilisema haina pesa za kuanza wakati huo kuiendesha, lakini akisaidiana na wananchi hasa wakulima wa kahawa wa Bukoba walikubali kukatwa hela kuendesha shule, aliifungua mwaka 1964.
Kusimamia na kufundisha katika shule hiyo aliwapata masista mashuhuri kwa kuendesha shule za wasichana, Masista wa Maryknol. Hawa tayari waliendesha shule za wasichana za Marian Morogoro na Rosary college Mwanza. Hapa siyo tu alijenga shule bali kwa kuwahusisha wananchi kuchangia uendeshaji wa shule hiyo, aliifanya shule ya watu wanaothamini elimu ya wasichana.
Katika maisha yake alipenda kuendeleza elimu hasa ya wasichana kama chaguo la kwanza. Hata mwishoni mwa utawala wake Dar es Salaam alitumainia bado kujenga shule ya sekondari ya wasichana ya bweni aliyotaka kuita 'Omushumba' maanake mchungaji. Kwa hilo alimaanisha kazi yake ya uchungaji ni hasa kuelimisha wasichana kama namna ya pekee ya kuelimisha jamii.
WATAWA:Shirika la Dada wadogo wa Mtakatifu Fransisko wa Asizi: Katika uzee wake kitu kimoja alichojivunia lilikuwa ni shirika hili la watawa wa Dar es Salaam. Alisumbuka sana kulianzisha hasa kuwapata walezi wazuri na kuwapa mwongozo.
Alisema kuwa walicheka kwa sababu kila walipokwenda kumtembelea aliwaonyesha picha hizo bila kutambua kwamba alisha waonyesha picha hizo mara nyingi. Alipokwenda Ulaya alikwenda na picha hizo za wajukuu wake kama walivyowaita kwa utani. Kila mara alitoa picha hizo mkobani na kueleza jinsi anavyotaka dada hao wadogo wawe watawa wa Jiji wenye kujiamini, elimu na mbinu mpya za uchungaji. Aliwashika kama mboni ya jicho lake.
Kadiri siku za kustaafu kwake zilivyokaribia ndivyo alivyozidi kupata homa juu ya wajukuu wake hao. Aliogopa kuwaacha yatima. Alipostaafu kwa wema wao hakuwaingilia ili wampokee askofu mkuu mpya na waweze kuendelea bila yeye. Hata hivyo kila mara aliulizia kwa mbali jinsi wanavyoendelea. Alifurahi kuona wanakua vizuri na kushika kasi nzuri chini ya uongozi wa Sr. Paulin Bommer na shirika la ‘Divine Providence’ la Balddeg Uswizi aliokuwa amewakabidhi.
Hospitali ya Ukonga:
Mradi mwingine wa misho ilikuwa hospitali ya ukonga. Aliweka nguvu nyingi sana katika mradi huu, kuipata ardhi ilikuwa na mlolongo mrefu sana lakini hakukata tamaa. Kwa sababu aliamini kwamba anataka kuwasaidia watu wa sehemu hiyo ambayo ilikuwa mbali ma huduma za afya alitulia nguvu zote za wadhifa wake kuletaufanisi. Kazi nyingine ilikuwa kuwapata wafadhili. Katika hayo yote alifanikiwa na kuanzisha kituo cha afya cha Ukonga kikiwa na lengo la kuwa hospitali kamili.
Aliwaomba masista wa shirika la Mtakatifu Therezia wa Mtoto Yesu wa Bukoba wamsaidie kuiendesha. Misingi aliyoiweka ilifnikisha kituo hicho ambacho sasa ni hospili. Tunashukuru uongozi wa jimbo Kuu la dar es salaam ambao walitambua juhudi hizo na kuiita jina lake.
Pamoja na Ukonga aliyaalika mashirika mengine kufungua zahanati katika sehemu mbali mbali za jiji ikiwemo, Tegeta, Kawe na Kibiti.
SIRI YA UFANISI WA RUGAMBWA
Kilaini aliendela kuandika katika mala kuwa Baada ya ibada ya misa ya kumwombea marehemu Rugambwa alimwendea Padre Jovin Bakekera na kumwuliza amwambie siri ya mafanikio ya Kardinali Rugambwa. Padre Jovin alikuwa katibu wake katika miaka tisa ya mwisho. Alifanya kazi naye katika ofisi na aliishi naye nyumbani hadi alipokata roho. Baada ya kufikiri kidogo Bakekera alisema 'sitaki mimi nimwite mtakatifu; lakini katika uamuzi wa kibinadamu alikuwa mkamilifu, hii ilikuwa hoja kubwa na hivyo akamwomba maelezo yake ,naye alisema kufuatana na cheo chake, heshima yake ya kifalme na unyamavu wake watu wengi walimwogopa, lakini kusema ukweli alivyokaa naye miaka hiyo yote Rugambwa alikuwa na moyo mzuri ajabu,pamoja na misimamo thabiti lakini hakupenda kumwudhi au kumwonea mtu. Kama alifanya kitu na akaona emekuudhi hata ukiwa mdogo uliona alifanya juu chini mwenyewe kukuonyesha kwamba anasikitika na alikuwa wa kwanza kuja kwako.
Pia Kilaini aliuliza swali hilo kwa Askofu Nkalanga, na kumjibu kwa kiingreza 'He had a golden heart' alikuwa na moyo wa dhahabu. Alisema watu waliongelea sana juu ya unyenyekevu wake lakini alidhanizaidi ya unyenyekevu yeye alikuwa na upendo mkubwa kwa watu. Yeye alijinyima vitu vingi hata kukuta nguo zake nyingine zimechakaa lakini kila alichopata alitaka kiende kwa watu wenye shida.
Kilaini aliendelea; hata yeye vile vile alimjua kwa miaka 30; hasa katika miaka ya 80 alipoanza kuugua alikuja Roma kwa matibabu akiwa mwanafunzi, kitu kikubwa ambacho wote walijua ni kwamba hakutaka hata mara moja kusumbua watu hata kama aliumwa, alitaka watu wafanye mambo yao wamalize kabla ya kumhudumia.
Siri yake nyingine ni kwamba alijua kutumia vipaji vya watu. Alipokuwa na kazi alimpa mtu aliyeamini ataifanya vizuri lakini vile vile alifuatilia na alitaka ripoti kamili za mara kwa mara. Mwadhama alijali sana uwezo katika kutoa kazi au madaraka,mtu akifanya vibaya awe nani atamnyanganya kazi au madaraka. Alichukia kama kitu kilifanywa vibaya. Watu wengine walichukia kwa sababu alitaka ripoti. Lakini jambo hilo liliwafurahisha wafadhili kwa sababu alikuwa mkali sana katika matumizi ya fedha na kutoa ripoti. Kwa sababu hiyo wafadhili wengi walimsaidia wakijua kwamba fedha zitatumika vizuri kama zilivyokusudiwa.
PUMZIKA KWA AMANI RUGAMBWA
Apumzike kwa amani Rugambwa kwa kazi yake kubwa alioifanya. Alivyotaniwa kila wakati na Askofu Isuja wa Dodoma, yeye alikuwa namba one, katika upadre kijijini mwake, katika uaskofu Tanzania, Ukardinali Afrika, na Askofu Mkuu wa kwanza Mtanzania Dar es Salaam. Sasa yuko kwa Mungu kama Mwobezi wetu. Mungu amweke mahala pema mbinguni na sisi tufuate katika nyayo zake. AMINA
Ni makala ya Baba Askofu Kilaini msaidizi wa jimbo la Bukoba aliyoiandika desembe 1997 baada ya kifo cha Hayati Kardinali Laurean Rugambwa – Imeandaliwa na Angela Rwezaula.








All the contents on this site are copyrighted ©.