Zihafamu nia za Mwaka wa Imani : Padre Flavian Kasalla
maadhimisho ya mwaka wa imani unaotarajiwa kuanza hapa mwezi oktoba mwaka huu. Sina
shaka moja ya matarajio makubwa ni kuelewa sababu za kuuita mwaka huu mwaka wa imani.
Maadhimisho ya mwaka wa imani ni sehemu ya safari ya Kanisa katika historia nzima
ya ukombozi. Kwa utamaduni wake Kanisa nimekuwa likiweka malengo mbalimbali yanayolisaidia
kama jamii ya Mungu kuingia katika ukweli wa mafumbo linayoyaadhimisha kila siku.
Vipindi hivi vya tafakari huchukua sura mbalimbali kulingani na matukio na ndani ya
Kanisa au historia ya Kanisa.
Natumaini tunakumbuka jinsi Kanisa lilivyoadhimisha
mwaka wa mapadre na jinsi lilivyotumia nafasi hiyo kuichambua Sakramenti ya upadre,
kukosoa mapungufu yanayoikabili huduma ya kipadre, kuwatia moyo mapadre na hatmaye
kuweka mikakati mipya ya kuilinda na kuidumisha Sakramenti hiyo kama ilivyotakiwa
na Kristo mwenywe. Pia Kanisa katika miaka ya karibuni limekwisha adhimisha mwaka
wa Ekaristi Takatifu, mwaka wa rozari Takatifu, nk. Kwa namna ya kipekee kabisa na
kwa upendo mkubwa baba Mtakatifu benedikto XVI amelitangazia Kanisa kipindi maalumu
cha tafakari kitakachojulikana kama mwaka wa imani.
Katika kuendelea na kuiishi
historia yake, Kanisa kwa namna ya pekee linakumbuka matukio makubwa mawili ambayo
yamehusianishwa na mwaka wa imani. Kwanza ni kuadhimisha miaka hamsini ya kufunguliwa
kwa Mtaguso wa Pili wa Vatikani (11 oktoba 1962). Pili Kanisa linaadhimisha miaka
ishirini tangu kuzinduliwa kwa katekismu ya Kanisa katoliki (11 oktoba 1992). Matukio
haya mawili yamechukuliwa na Kanisa kama nafasi ya neema inayoliwezesha kutafakari
hali ya imani ndani ya Kanisa.
Katika adhimisho la kwanza linaloliingiza
Kanisa katika mwaka wa imani, Kanisa ninatafakari Mtaguso wa Pili wa Vatikani ambao
ulitambulishwa na Baba Mtakatifu Yohani XXXIII kama “kipindi cha kusambaza mafundisho
sahihi na kamilifu, bila mkanganyiko wa tafsiri, ili kuyafikisha kwa uaminifu mafundisho
ya imani yasiyobadilika kwa mahitaji nyakati zetu.” Mtaguso unafundisha katika hati
yake ya Mwanga wa Mataifa (Lumen Gentium, 1) kwamba “Kristo ni mwanga wa mataifa.
Kwa hali hiyo, Mtaguso uliokutanishwa na Roho Mtakatifu unahitaji kupeleka mwanga
wa Kristo kwa watu wote, mwanga unaoonekana wazi katika Kanisa lake.” Katika kupeleka
Mwanga huo wa Kristo Mtaguso ulichambua mazingira manne na kuyatolea hati maalumu
kama mwongozo wa kuifikisha imani katika yakati zetu. Hati ya Kwanza ni ile inayoonesha
kwamba mwanga wa Kristo unaonekana katika kila adhimisho la Liturjia Takatifu (hati
ya Liturjia, Sacrosanctum Concilium). Hati ya pili inahusika na Neno la Mungu kama
pia njia ambamo mwanadamu wa nyakati mbalimbali anakutana na mwanga wa Mungu yaani
Kristo mwenyewe, (Hati ya Maandiko Matakatifu, Dei Verbum). Mtaguso unachambua pia
kwa kina asili ya Ki-Mungu ya Kanisa katika hati yake juu ya Kanisa, (Hati juu ya
Kanisa, Lumen Gentium). Na hati nyingine ni ile inayoonesha uhusiano kati ya Kanisa
na ulimwengu kwa nyakati husika (Hati ya Kichungaji, Gaudium et spes). Ni katika hati
hazi nne kwa kweli ambamo mafundisho mbalimbali ya Mtaguso wa Pili wa Vatikani yamejengeka.
Katika tafakari ya mwaka wa imani inayotarajiwa kuanza hapo tarehe 11
oktoba 2012, kinachofanyika kwa kweli ni kusherehekea zawadi ya imani ambayo ni Mungu
pekee anaweza kumkirimia mwanadamu. Kipindi hicho cha shukurani na tafakari ya kina
juu ya imani, kinasindikizwa na programu mbalimbali ambazo zitahitimishwa hapo tarehe
24 novemba 2013 kwa adhimisho la sikukuu ya Yesu Kristo mfalme wa ulimwengu. Ni kipindi
kinachotarajiwa kumwingiza muamini katika undani wa kuitabua imani yake iliyojengeka
juu ya mkutano wake na Kristo Mfufuka. Mwaka wa imani ni mwendelezo wa kuyaweka
katika matendo mafundisho yote ya Mtaguso wa Pili wa Vatikani. Ni kipindi cha tathmini
juu ya mafanikio yaliyokwisha patikana kutokana na zawadi iliyotolewa na Mtaguso
wa Pili wa Vatikani. Maadhimisho haya ya mwaka wa imani hayatakuwa ya kwanza ya kutambua
nafasi ya Mtaguso wa Pili wa Vatikani katika historia ya Kanisa. Mara tu baada ya
Mtaguso wenyewe, mapapa wamekuwa wakiitisha sinodi mbalimbali ili kuangalia na kuongoza
utekelezaji wa vipengele mbalimbali vya Mtaguso huo. Na hata katika adhimisho la
mwaka huu wa imani bado baba Mtakatifu benedikto XVI ameitisha sinodi nyingine ya
maaskofu wa dunia nzima ili kujadili juu ya uinjilishaji mpya sanjari na maadhimisho
ya mwaka wa imani.
Mwaka wa imani ni kipindi pia cha shukrani kwa zawadi
ya katekismu ya Kanisa katoliki. Katekismu hii ambayo inatimiza miaka 20 imekuwa ni
msaada mkubwa wa kuikuza imani kulingana na mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatikani.
Baba Mtakatifu benedikto XVI anaiita katekismu hii kuwa ni tunda halali za Mtaguso
wa Pili wa Vatikani na chombo sahihi cha kupokelea Mtaguso huo. Katikesmu ya Kanisa
katoliki ni mkusanyiko wa mambo ya kale na mapya ambayo yote yako kwa ajili ya huduma
ya imani ambayo haibadiliki huku ikimsaidia mwanadamu kupata mwanga mpya maishani.
Katika katekismu ya Kanisa katoliki, imani inachambuliwa katika mazingira
matatu. Kwanza ni imani kama inavyoungamwa na kila muumini katika kanuni ya imani.
Pili imani inaangaliwa katika maadhimisho ya kiliturjia Takatifu, na hasa maisha ndani
ya Sakramenti mbalimbali. Tatu imani inajionesha katika maisha ya kikristo kama yanavyoongozwa
na amri za Mungu. Na mwisho, ni imani katika maisha ya sala ya kikristo. Mafundisho
haya ya kikatekesi ingawa yamekuwa yakifundishwa kwa karne nyingi tu, katekismu ya
Kanisa katoliki inayachambua katika mtazamo wa mazingira na hali mpya ya wakati wetu.
Hali hii ndiyo inayoifanya katekismu ya Kanisa katoliki kuwa chombo sahihi cha muungano
wa kikanisa na njia sahihi ya kufundishia imani.
Kwa hali hiyo, mwaka
wa imani unategemewa kuelekeza katika wongofu mpya na katika uvumbuzi mpya wa imani
kwa Kristo ili kuwawezesha waamini wote kuwa mashahidi aminifu na wenye furaha wa
Kristo mfufuka katika dunia yetu ya Leo. Ni shuhuda unaohusisha pia juhudi za kuwaongoza
wengine wote kuelekea mlango wa imani ambaye ni Kristo mwenyewe. Katika kufikia imani
ndani ya Kristo, kila mwanadamu anagundua kiini cha maisha, furaha na upendo wa kweli.
Kipindi hiki cha neema kinacholielekeza Kanisa katika uinjilishaji mpya ndicho kinachojulikana
kama mwaka wa imani. Ni kipindi cha kuvumbua kwa mara nyingine furaha ya kuamini na
cha msukumo wa kuwashirikisha wengine imani.