Parokia ya Bunena Bukoba yatimiza miaka mia, na Maziko mapya ya Kardinali Rugambwa.
Mamia ya waamini Jumapili walimiminika katika Ibada iliyoongozwa na Askofu Nestorius
Timanywa wa Jimbo la Bukoba kuadhimisha sherehe ya Jubilee ya miaka mia tangu parokia
ya Bunena , ilipoanzishwa na Wamisionari wa Afrika (White Fathers), mwaka 1912. Katika
homilia yake Askofu Timanywa aliwaasa waamini kwamba, Jubilee hii ya miaka mia, uwe
ni wakati wa kuwaweka karibu zaidi na Mungu, na katika mshikamano na umoja wa kufanikisha
maendeleo na ustawi wao kimaisha pia. Wafanye kazi kwa bidii na mshikamano zaidi,
huku wakitakatifusha matendo yao na kukataa maovu na vishawishi vya shetani, kama
tabia za ulevi, utoaji wa mimba, ufuska na kupambana kikamilifu na virus vya HIV/
UKIMWI. Pia Askofu Timanywa alitangaza uwepo wa tukio jingine muhimu la kihistoria
hivi karibuni ambamo Mtumishi wa Mungu , Marehemu Kardinali Laurian Rugambwa , atazikwa
upya katika Kanisa Kuu la mjini Bukoba hapo tarehe 6 Octoba mwaka huu. Na alieleza
sababu zilizochelewesha maziko hayo kwamba, ilitokana na ukarabati mkubwa uliohitajika
kukamilishwa katika kanisa Kuu la Bukoba Mjini. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa,
Mwili wa Marehemu Kardinali Laurian Rugambwa,tarehe Octoba 6, utasafirishwa kutoka
kanisa la Kashozi na kuzikwa siku inayofuatia katika Kanisa kuu la Bukoba Mjini. Marehemu
Kardinali Laurian Rugambwa, ni mwafrika wa kwanza kupata daraja la Kardinali katika
Kanisa Katoliki la Ulimwengu. Aliifariki dunia akiwa na Umri wa miaka 85, Desemba
8 1997, jijini Dar es salaam na kupewa maziko ya muda katika Kanisa la Kashozi Bukoba.
Kuteuliwa kwake kuingia katika Decania ya Makadinali , kulionyesha alama ya utambuzi
kwamba, Kanisa la Roma si kanisa la Magharibi, bali ni kanisa la Ulimwengu. Na hivyo
kuonyesha umuhimu wa mpanuko wa mashirika ya kanisa sehemu mbalimbali za dunia, ikifuta
muono wa nyuma wa kutawaliwa na wamisionari kutoka mataifa ya Magharibi. Kardinali
Rugambwa anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa wakati wa Mtaguso Mkuu wa pili
wa Vatican, ambamo alihimza umuhimu wa jumuiya za walei, kujihusisha katika kazi
na utume wa kanisa. Alisistiza, utendaji wa kazi za missioni kwamba hauwezi kutenganishwa
utendaji wa maisha ya kila siku ya muumini. Na aliwataka Wakatoliki, kuwa tayari
kushirikiana na wasiokuwa Wakatoliki, kutembea pamoja katika hija ya maisha ya hapa
duniani. Alisisitiza Kanisa lipaswa kuwa mwalimu wa maisha. Kati ya urithi ulioachwa
nae ni Hospitali ya Rubya na Mugana , pia seminari ya Ntungamo na Shule ya Wasichana
ya Rugambwa , vyote vikiwa mkoani Kagera.